Nafasi Ya Matangazo

May 09, 2026






Na Mwajdishi wetu, Geita,
Waziri wa Madini, *Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb)* atoa wito kwa benki zote nchini kuchangamkia fursa kwenye sekta ya madini kwa kubuni na kutengeneza bidhaa maalum ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kuwa na mitaji itakayoongeza tija kwenye shughuli zao.

Ameyasema hayo leo tarehe 09 Mei, 2026  alipokuwa akizindua Tawi la Benki ya Exim Mkoani Geita.

"Ninamshukuru kwa dhati *Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan* kwa namna anavyoendelea kuisimamia sekta ya madini. Maono na maelekezo yake ndiyo yanaifanya sekta ya madini kukua kwa kasi na kupelekea mchango wake kwenye Pato la Taifa kufikia asilimia 10.1"

"Nitoe wito kwa benki zote nchini, kufikiria kuwa na bidhaa maalum kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wadogo pasipo kuathiri masharti ya Sheria ya Fedha. Niwaombe mtoke ofisini na muende migodini, mkawatembelee wachimbaji na kujionea fursa kubwa iliyopo kwenye sekta ya madini nchini", alisisitiza Mhe. Mavunde.

Aidha, Mheshimiwa Mavunde aliipongeza Benki ya Exim kwa kufungua Tawi Geita na kusisitiza kwamba ni uamuzi sahihi kwani Mkoa wa Geita umeendelea kuwa kinara katika makusanyo ya maduhuli ya Serikali na biashara ya madini nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alibainisha kuwa Serikali  ina mpango wa kuwawezesha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kupitia mfuko wa dhamana ili kuwaongezea nguvu ya ushiriki wa kikamilifu kwenye sekta ya madini.

"Ni matamanio ya Serikali kuona kiasi kikubwa cha mzunguko wa fedha kwenye biashara ya madini zinabaki nchini ili kukuza uchumi wetu" aliongeza mhe. Mavunde.

Awali, akieleza maelezo mafupi ya benki, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, *Bw. Jaffar Matundu* alieleza kuwa benki ya Exim ina mkakati wa kuwezesha biashara, ambao unaendana na dira ya Serikali ya kuinua uchumi kupitia rasilimali madini, na kuongeza kuwa Exim ipo tayari kutoa suluhisho la changamoto ya mitaji kwa wachimbaji wadogo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, *Mheshimiwa Hashim Komba* alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweka mazingira wezeshi ambayo yamerahisisha ufanyaji wa biashara na kuvutia wawekezaji mkoani Geita.
Posted by MROKI On Saturday, May 09, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo