Timu ya mchezo wa netiboli ya Ofisi ya Makamu wa Rais nchini Tanzania Bara, imeibuka kidedea kwa kutwaa ubingwa wa ligi ya daraja la tatu baada ya kushinda mechi zake zote kwenye ligi hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mabingwa hao walidhihirisha umahiri wao baada ya mchezo wa kwanza kuwafunga timu ya Chamwino HQ, na katika mchezo wa pili waliwashinda JKT Makutupora kwa magoli 41-24.
Awali Katibu Msaidizi wa Chama cha Netiboli Mkoa wa Dodoma (CHANEDO), Bi. Maimuna Kitete, amesema ligi hiyo ilishirikisha timu tatu pekee baada ya nyingine kushindwa kushiriki kutokana na changamoto mbalimbali, ambapo bingwa ajikusanyia magoli mengi ya kufunga 103 na kufungwa 33; huku mshindi wa pili JKT Makutupora alimaliza kwa magoli ya kufunga 48 na kufungwa 50 na mshindi wa tatu Chamwino HQ alifunga 18 na kufungwa 103.
Bi. Maimuna amesema timu mbili ya Makamu wa Rais na JKT Makutupora zimefanikiwa kupanda daraja hadi la pili, na watashiriki kwenye mashindano hayo yanayotarajia kufanyika mkoani Tanga baadaye mwezi Oktoba.
Akifunga ligi hiyo mgeni rasmi, Bi. Itika Mwankenja, Mjumbe kutoka Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), pamoja na uchache wa timu amewapongeza washiriki wote walioshiriki kwenye ligi hiyo, ambapo wamecheza kwa amani, nidhamu na upendo mkubwa tofauti na mashindano mengine.
Bi. Itika amezitaka timu zilizopanda daraja kuhakikisha wanapeperusha vyema bendera ya CHANEDO kwa kufanya vizuri katika mashindano ya daraja la pili, kwa kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii, kujifunza mambo mapya na kusikiliza mafunzo kutoka kwa makocha wao.
“Ninawapongeza sana wachezaji mmecheza kwa nidhamu kubwa, tofauti kabisa na mashindano mengine tuendelee na nidhamu hii, mmemaliza mechi mkakumbatiana na kupeana mikono, hadi na makocha wenu wamefanya vivyo hivyo, nawapongeza viongozi wa CHANEDO kwa kuandaa ligi hii, maana mchezo wa netiboli hauchuji tuendelee kuuenzi, na ninatamani sana kuona mkoa wa Dodoma unatoa wachezaji wengi wa timu ya Taifa, najua mpo na mkifanya vizuri mtatokea na mnawalimu wazuri pia” alisisitiza Bi. Itika.
Hatahivyo, amezitaka timu zijitokeze kwa wingi kushiriki kwenye kombe la CHANEDO litakalofanyika baadaye mwezi Juni 2026














0 comments:
Post a Comment