Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Massauni akimkabidhi Kombe la Ubingwa kwa nahodha
wa timu ya KVZ baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano Kombe la Muungano mpira wa
Pete, yaliyomalizaka Januari 24,2026 katika Uwanja wa New Amaan Complex.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Massauni akimkabidhi cheti, Sophia Shaban
Mkebure mchezaji wa timu ya KVZ baada ya kuibuka mchezaji bora wa mashindano
Kombe la Muungano mpira wa Pete, yaliyomalizaka Januari 24,2026 katika Uwanja
wa New Amaan Complex.
Naibu Waziri wa Habari Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Ali Abdulgulam Hussein akimkabidhi cheti cha ushiriki mashindano Kombe la Muungano mpira wa Pete, nahodha wa timu ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Anna Akwilini yaliyomalizaka Januari 24,2026 katika Uwanja wa New Amaan Complex.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Massauni akimkabidhi tuzo ya mfungaji bora
mchezaji wa KVZ, Tupege Lazaro kwenye mashindano Kombe la Muungano mpira wa
Pete, yaliyomalizaka Januari 24,2026 katika Uwanja wa New Amaan Complex.
Na Mwandishi Wetu, Unguja.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Maendeleo ya michezo
yamechangiwa na juhudi kubwa za viongozi wakuu wa nchi Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambao wameweka vipaumbele
katika sekta hiyo.
Amezungumza hayo Januari 24,
2026 wakati akifunga Mashidano ya mpira wa Pete ya Kombe la Muungano Zanzibar
ambapo timu ya KVZ imeibuka bingwa baada ya kushinda michezo yote 10.
"Kupitia mpango wa
"Goli la Mama", tumeshuhudia ongezeko la Bajeti, ujenzi wa viwanja
vipya na mazingira bora kwa wanamichezo wetu, matokeo ya jitihada hizi ni wazi
na tumeshuhudia Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ‘Taifa stars’ imefika hadi
hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON pale Morocco na ni kwa mara ya kwanza
tangu kuanza kushiriki mashindano hayo," amesema Mhe. Masauni.
Amesema ujenzi pamoja na uboreshaji
wa Viwanja vya michezo vimewezesha mashindano mbalimbali kufanyika yakiwemo
mashindano ya CHAN yaliyohusisha nchi za Kenya, Uganda na Tanzania. Huu ni
ushahidi kuwa Tanzania, kupitia Muungano wake, inainuka kisoka Afrika na
Duniani.
Ameeleza Maendeleo haya
yamewekewa chachu ya ushirikiano kati ya serikali zetu mbili chini ya wizara
husika za michezo na taasisi zetu za ZFF, TFF, CHANEZA NA CHANETA ambazo
zinasimamia michezo hii ya mpira wa miguu na Pete kwa weledi mkubwa sana.
“Nawapongeza viongozi wa
wizara hizi na wasaidizi wao pamoja na viongozi wa ZFF, TFF, CHANEZA NA CHANETA
kwa kuhakikisha wanasimamia maendeleo ya michezo nchini," ameongeza
Masauni.
Aidha katika hatua ingine
Waziri Masauni amewashukuru waandaji wa Mashindano haya CHANEZA na CHANETA na Ofisi
ya Makamu wa Rais kwa kutekeleza agizo la Rais la kuimarisha Muungano kupitia
michezo alilolitoa Aprili 13, 2024 wakati akipokea taarifa ya Kamati Maalum
iliyowasilisha maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHANEZA
Bi. Nasra Juma ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushiriki na kudhamini mashindano hayo ambayo
yamekuwa ya ushindani mkubwa.
Amesema mashindano hayo ni
muhimu kwa kuwa yamekuwa yakitoa wawakilishi wa Tanzania katika mashindano
makubwa kwa Bara la Afrika na jumuiya ya Afrika Mashariki. Mashindano haya
yalishirikisha timu 11, tano kutoka Zanzibar na sita kutoka Tanzania Bara.
0 comments:
Post a Comment