Nafasi Ya Matangazo

December 12, 2025





Rombo- Kilimanjaro
Serikali imeeleza kujivunia hatua kubwa zinazopigwa na Wachimbaji Wadogo nchini, wakiwemo wanaochimba Madini ya Pozzolana pamoja na wakataji wa matofali ya volcano (volcanic blocks) katika Kata ya Holili, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, hatua inayoendelea kuonesha kasi ya ukuaji wa Sekta ya Madini siku hadi siku.

Kauli hiyo imetolewa leo Desemba 11, 2025 na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji wilayani Rombo, ambapo amesisitiza kuwa Sekta ya Madini imekuwa mhimili unaochochea na kuunganisha sekta nyingine kama ujenzi, viwanda, biashara, kilimo, maji na maeneo mengine ya uchumi.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeanzisha Programu ya Mining for A Brighter Tomorrow – MBT yenye lengo la kuwawezesha vijana na wanawake wanaojihusisha na uchimbaji mdogo kwa kuwapatia leseni za uchimbaji pamoja na vifaa vya kisasa ili kuboresha uzalishaji wao na kuongeza tija.

 “Programu hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapiga hatua na kuwa sehemu pana ya uchumi wa taifa,” amesema Dkt. Kiruswa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kufuta leseni za uchimbaji na utafiti ambazo hazifanyiwi kazi, ili kuhakikisha rasilimali madini zinawanufaisha Watanzania kikamilifu na kuondoa vizuizi vinavyochelewesha maendeleo ya sekta.

Kwa upande, Mkuu wa Wilaya ya Rombo,  Mhe. Raymond Mwangwala amesema kuwa uwepo wa madini ya Pozzolana umesaidia kutangaza Wilaya hiyo sambamba na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo huku vijana wakinufaika na ajira kupitia uwepo wa madini hayo yatokanayo na volcano na miamba ya volcano inayotumika kutengenezea matofali imara.

Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa Mkoa Kilimanjaro Mhandisi Abel Madaha ameeleza kuwa makusanyo ya maduhuli kutoka Sekta ya Madini katika Mkoa wa Kilimanjaro yamefikia shilingi bilioni 1.63 kuanzia Julai hadi Novemba 2025, ikiwa ni asilimia 45 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 4.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hatua imayoashiria mwitikio mzuri wa wachimbaji na usimamizi madhubuti unaoendelea kufanywa na Wizara ya Madini ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinachangia kikamilifu kwenye maendeleo ya taifa.

Pozzolana ni aina ya madini ujenzi yenye asili ya udongo au majivu ya volkano ambayo, ikichanganywa na chokaa na maji, huunda saruji yenye uimara mkubwa na hutumika kwa wingi katika viwanda vya saruji hapa nchini.
Posted by MROKI On Friday, December 12, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo