Washiriki takribani 3000 wa michezo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) wamechangia mahitaji yenye thamani ya zaidi ya Tshs Mil. 15 na kupeleka kwa vituo sita vya wahitaji vilivyopo jijini Mwanza.
Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Alex Temba amesema ni utaratibu wa shirikisho hilo kutenga siku moja kwenye kalenda yao kipindi cha mashindano kwenye mkoa husika, kwa ajili ya kutembelea vituo vya wahitaji na kuwapelekea mahitaji muhimu ya kibinadamu.
Temba amesema anaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuruhusu watumishi wa umma kushiriki kwenye michezo hii, ambayo inasaidia kuweka watumishi katika hali njema ya kiafya na kiakili.
“Kama inavyoelezwa katika dini na jamii zetu kunawahitaji wanaohitaji msaada wetu, kwani hata sisi watumishi tunapaswa kurudisha fadhila kwa wenzetu wenye kuhitaji, ila natoa rai kwa makundi mbalimbali tunapokuwa kwenye shughuli mbalimbali wawe na tabia za kufanya matendo ya huruma ili kuisaidia serikali,” amesema Bw. Temba.
Naye Mratibu wa zoezi la kurejesha kwa jamii, Bi.Itika Mwankenja amesema watumishi wametembelea gereza la Butimba, kituo cha wazee cha Bukumbi, kituo cha watoto Tawfiq, Kituo cha watoto cha Console, Watoto Afrika na Fonelisco.
Bi., Itika amesema watumishi wamejichangisha kutoka kwenye mifuko yao fedha hizo na kununua vyakula, sabuni za aina mbalimbali, viatu aaina ya yeboyebo vya watoto na watu wazima, nguo za ndani za watoto wa kike na kiume, taulo za kike, mafuta ya kula na ya kujipaka, kalamu, penseli, madaftari, mabegi ya shule, mashuka, soksi, vitabu vya maandiko matakatifu Biblia, Misahafu, juzuu na tezi za rohoni.
Bi. Itika amesema mbali na mahitaji maalumu pia kila kituo kimepewa fedha taslim kwa ajili ya kununua umeme.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Elikana amewashukuru washiriki wa michezo ya 39 ya SHIMIWI kwa matendo ya huruma waliyofanya, pamoja na kwamba nao wanashirikisha vikundi mbalimbali kutoa misaada ya vyakula, nguo kwa wahitaji na kuchangia damu kwa wagonjwa.
Afisa Ustawi wa Jamii na Meneja wa kituo cha watoto wenye uhitaji cha Fonelisco, Bw. Amos Mashauri ameshukuru watumishi kwa mahitaji waliyowaletea ambapo kuna watoto 55 kati yao 28 ni wa kiume na wakike 27.
“Tunawashukuru sana tena mno wanamichezo wa SHIMIWI kwa kutushika mkono na kurudisha tabasamu kwa watoto, tunawaombea kwa Mungu akajaze pale mlipopunguza, na tunawakaribisha wakati mwingine tena,” amesema Bw. Amos.
Naye mtoto Prince Martin ameshukuru kwa zawadi zilizowasilishwa kwenye kituo chao, na ameomba watumishi wasichoke waendelee kuwasaidia.
Mkurugenzi wa kituo cha Watoto cha Console, Bi. Rosemary Minja amesema kituo hicho kinawatoto 24 ambao wanapatikana kutoka Ustawi wa Jamii, na ameshukuru na kufarijika kwa kuona kundi la wanamichezo wanawakumbuka wenye uhitaji.
“Tunashukuru kwa kutimiza maneno ya Mungu kwa kumtolea kupitia sadaka mbalimbali ikiwemo ya kuwapa wahitaji na mmetoa kwa upendo,” amesema Bi. Rosemary.
Naye Bi. Lucy Katemkola afisa wa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Ilemela, amesema kituo cha Watoto Afrika kina idadi ya watoto 105 kati yao 68 ni watoto wa kiume na 37 ni wa kike, ambao wote wanapatikana kutoka kwenye mazingira hatarishi.














0 comments:
Post a Comment