Fainali ya michezo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) itakayofanyika tarehe 16 Septemba, 2025 kwenyeuwanja wa CCM Kirumba, Jijini Mwanza inatarajiwa kuwa ya kihistoria kutokana na timu zilizofuzu kwa michezo ya kuvuta kamba, mpira wa miguu na netiboli baadhi kuingia hatua hiyo kwa mara ya kwanza.
Katika fainali za michezo hiyo, timu mpya ni pamoja na Tume ya Umwagiliaji kwa mpira wa miguu, nao Ukaguzi katika netiboli na RAS Tanga na TAKUKURU kwa kamba wanawake na wanaume.
Hatahivyo, mechi hizo zinatarajiwa kutoa burudani safi kutoka kwa mabingwa watetezi wa mpira wa miguu timu ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, huku netiboli na kamba wanaume ni timu ya Ofisi ya Rais Ikulu.
Katika michezo ya nusu fainali iliyofanyika uwanja wa CCM Kirumba kwa mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake timu ya RAS Tanga waliwavuta Mahakama kwa 2-0; nao TAKUKURU waliwashinda RAS Geita 2-0; wakati kwa wanaume Ikulu wamewavuta Wizara ya Mifugo na Uvuvi 2-0; na TAKUKURU waliwashinda Wizara ya Uchukuzi kwa 2-0.
Katika mchezo wa mpira wa miguu uliootoa burudani safi kwa watazamaji, Klabu ya Utumishi waliwafunga TAKUKURU kwa bao 1-0; nao timu ya Tume ya Umwagiliaji waliwashinda Wizara ya Katiba na Sheria kwa bao 1-0.
Kwa mchezo wa netiboli Ikulu waliwashinda ndugu zao Utumishi kwa magoli 53-26. Washindi waliokuwa wakicheza kwa kurusha pasi ndefu waliweza kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 30-16.
Timu nyingine iliyoingia fainali ni Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi waliowafunga Wizara ya Maliasili na Utalii kwa magoli 47-42, hatahivyo timu hizo zilikwenda mapumziko wakiwa nguvu sawa ya magoli 22-22.











0 comments:
Post a Comment