Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa Daraja la John
Pombe Magufuli (Kigongo–Busisi) sio tu ni ndoto ya mtangulizi wake iliyotimia,
bali pia ni alama ya uhuru wa kiuchumi wa Tanzania na chachu ya maendeleo kwa
mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani.
Akizungumza wakati wa hafla ya
uzinduzi wa daraja hilo, Rais Dkt. Samia amesema daraja la J.P. Magufuli ni
mkombozi mkubwa kwa wananchi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya vivuko kwa
miongo kadhaa, na sasa wamepata suluhu ya kudumu kwa usafirishaji wa watu,
bidhaa na huduma.
Daraja hilo kubwa lenye urefu
wa kilomita 3.0 na barabara unganishi ya kilomita 1.66 limejengwa kwa gharama
ya zaidi ya Shilingi Bilioni 700 ambazo ni fedha za ndani na ni daraja refu
zaidi Afrika Mashariki na la sita kwa urefu barani Afrika.
Rais Dkt. Samia ameeleza
ujenzi wa daraja hilo kama kielelezo cha uwezo wa Taifa kupanga na kutekeleza
miradi mikubwa kwa kutumia rasilimali zake na ni hatua ya kujivunia kama nchi
inayojitegemea.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema
daraja hilo ni kiungo muhimu kwa Kanda ya Ziwa na kuzifikia nchi za Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda, huku akiwaasa wananchi
kuhakikisha wananufaika nalo kwa kuongeza uzalishaji, kusafirisha bidhaa,
pembejeo na kufikia masoko kwa urahisi.
Rais Dkt. Samia pia amepongeza
juhudi za vijana Watanzania waliopata fursa ya kushiriki katika ujenzi wa
daraja hilo, akiwataka kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata katika ujenzi wa
miradi mingine ya kimkakati nchini.
Vilevile, Rais Dkt. Samia
ametoa rai kwa wananchi kulitunza daraja hilo na kulitumia kwa uangalifu kwa
kuwa ni rasilimali kubwa ya Taifa, huku akizielekeza Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS) na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha linafanyiwa ukaguzi wa
mara kwa mara na kuimarishwa ulinzi dhidi ya vitendo vya uharibifu.
Hali kadhalika, Rais Dkt.
Samia amesema Serikali imekamilisha madaraja mengine makubwa tisa kote nchini
tangu mwaka 2021, na ipo katika hatua mbalimbali za kukamilisha miradi mingine
saba katika maeneo tofauti nchini, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara
zinazounganisha maeneo muhimu ya kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Rais
Dkt. Samia alizindua rasmi Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Mji wa Lamadi
katika Wilaya ya Busega, sambamba na kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa
Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi mkoani Simiyu.
Mradi wa Kukabiliana na
Mabadiliko ya Tabianchi unahusisha sekta za maji, kilimo, mifugo na uhifadhi wa
mazingira, ukiwa na lengo la kuiwezesha jamii kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi.
Rais Dkt. Samia amewapongeza
wananchi waliotoa maeneo yao kwa hiari ili kupisha utekelezaji wa mradi wa
maji, na kuhimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika awamu inayofuata
ya utekelezaji wa miradi kama hiyo katika miji ya Maswa na Meatu.
0 comments:
Post a Comment