Nafasi Ya Matangazo

June 20, 2025

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) akimkabidhi zawadi Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohammed Janabi kumtakia utumishi mwema wa majukumu anayoenda kuyaanza hivi punde. Hafla hiyo fupi ilifanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili sambamba na kuwafungulia Akaunti ya Junior Jumbo Watoto 76 waliozaliwa hospitalini hapo.
Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohammed Janabi (kushoto) akimsikiliza kwa umakini Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kumuaga na kumtakia kazi njema katik amajukumu yake mapya anayotaraji akuyaanza hivikaribuni.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) na Balozi wa Akaunti ya Junior Jumbo ya Benki ya CRDB, Paula Masanja (kushoto) wakimkabidhi mmoja wa wanawake (katikati) waliojifungua katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zawadi kwa ajili ya mtoto wake kuadhimisha Wiki ya Mtoto wa Afrika.

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam. Tarehe 19 Juni 2025: Katika kusherehekea Siku ya Mtoto wa Afrika inayoadhimishwa Juni 16 kila mwaka, Benki ya CRDB imetembelea wodi ya watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwapongeza wazazi kwa kujifungua salama.

Licha ya ziara hiyo iliyofanyika katika wodi ya watoto njiti hospitali hapo, Benki ya CRDB pia imetumia nafasi hiyo kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi kwa kushinda kiti cha Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

Akizungumza kwenye ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema siku zote wamekuwa wakitoa elimu ya fedha na kuwahamasisha wananchi kutumia huduma za benki tangu wakiwa wadogo ili kujenga msingi imara wa uchumi binafsi siku zijazo.

“Katika wiki hii ya kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika tumeona ni vyema kuja kuzungumza na wazazi hapa Muhimbili. Tunasisitiza elimu ya fedha ianze kutolewa tangu kwa watoto wadogo na ili kuliweka suala hili kwa vitendo, watoto wote waliopo hapa tutawafungulia Akaunti ya Junior Jumbo yenye shilingi 10,000 ya kuanzia ili mzazi akitoka hapa akaendeleze utaratibu wa kumtunzia mwanaye fedha zitakazomsaidia siku zijazo,” amesema Nsekela.

Kwa akiba yoyote iliyomo kwenye Akaunti ya Junior Jumbo, Benki ya CRDB hutoa riba ya mpaka asilimia 5 kwa mwaka hivyo kumpa uhakika mzazi au mlezi uhakika wa fedha za uhakika pindi mwanaye atakapoanza shule au atakapokuwa na mahitaji mengine yanayohitaji fedha.

“Akiba inawekwa kidogokidogo ingawa matumizi yake huwa makubwa pale yanapojitokeza. Ni vizuri kujenga utamaduni wa kuhifadhi fedha kidogo ambazo kadri muda unavyoenda zitazidi kuongezeka hivyo kutosha kwa ada na matumizi mengine ya shule au kwa jambo jingine ambalo mzazi atahitaji kulifanya kwa ajili ya mtoto wake,” amesema Nsekela.

Akimuaga Profesa Janabi anayetarajia kuondoa wiki ijayo kwenda kuanza majukumu yake mapya na Shirika la WHO hivi karibuni, Nsekela amemsifu kwa mikakati makini aliyonayo na kumuahidi kwamba Benki ya CRDB ipo tayari kushirikiana naye huko na anakokwenda na itaendeleza uhusiano mwema uliopo na Hospitali ya Taifa Muhimbili hata baada ya yeye kuondoka.

“Nilikusikiliza wakati wa kampeni za kuomba uchaguliwe kuiongoa WHO. Ulikuwa na mikakati 10 lakini mimi nimevutiwa na tatu ambazo ni utafiti na ubunifu, ubia pamoja na ufadhili wa huduma za afya kwa vyanzo vya ndani. Naamini vipaumbele hivi sio tu vitazifaa nchi zote 47 utakazokuwa unazihudumia bali vinato anafasi kwetu sekta binafsi kushiriki zaidi kuimarisha huduma za afya katika mataifa yetu. Benki ya CRDB itashirikiana nawe katika maeneo haya yote,” amesema Nsekela.

Kwa upande wake, Profesa Janabi ambaye ameimarisha ufanisi huduma hospitalini hapo tangu alipoteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji mwaka 2022, ameishukuru Benki ya CRDB kwa kwenda kumuaga akisema ni kampuni ya kwanza kufanya hivyo jambo linaloonyesha heshima kubwa ambayo taasisi hiyo kubwa ya fedha imempa.

“Uhusiano wangu na Benki ya CRDB ni wa muda mrefu. Tangu nilipokuwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tulikuwa pamoja mkitusaidia kugharimia matibabu ya watoto. Nafurahi mmenikumbuka leo na kuja kuniaga,” amesema Profesa Janabi.

Akitarajiwa kuondoka wiki ijayo, Profesa Janabi anaiacha Tanzania akikumbukwa kwa utoaji wake wa elimu kupitia mitandao ya kijamii jambo lililoongeza hamasa ya kuepuka ulaji usiozingatia mahitaji ya kiafya unaoweza kumsababishia mtu magonjwa yasiyoambukiza.

Katika kuendeleza elimu hiyo, Profesa Janabi aliwaeleza wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwamba wangepata chakula cha mchana pamoja na akasisitiza: “Mlo wetu leo utakuwa tunda moja la apple (tufaa).”

Akiwa mkurugenzi mtendaji mwanzilishi wa JKCI, Profesa Janabi alifanikiwa kuifanya kuwa taasisi mahiri inayohudumia wagonjwa wa ndani na watokao nje ya nchi hivyo kuacha mchango ambao hautosahaulika.

Balozi wa Akaunti ya Junior Jumbo, Paula Masanja aliwatia moyo wazazi waliojifungua watoto njiti na kuwahamasisha kuitumia akauniti hiyo kwa ajili ya watoto yao akisema ni muhimu kuwa na akiba kwa ajili ya matumizi yatakayojitokeza wakati wowote.

“Nami ni mzazi mwenye mtoto mdogo kama ninyi. Akaunti ya Junior Jumbo ni nzuri, itumieni kwa ajili ya watoto wenu,” alihamasisha Paula.
Posted by MROKI On Friday, June 20, 2025 No comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa Daraja la John Pombe Magufuli (Kigongo–Busisi) sio tu ni ndoto ya mtangulizi wake iliyotimia, bali pia ni alama ya uhuru wa kiuchumi wa Tanzania na chachu ya maendeleo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani.





 
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa daraja hilo, Rais Dkt. Samia amesema daraja la J.P. Magufuli ni mkombozi mkubwa kwa wananchi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya vivuko kwa miongo kadhaa, na sasa wamepata suluhu ya kudumu kwa usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma.
 
Daraja hilo kubwa lenye urefu wa kilomita 3.0 na barabara unganishi ya kilomita 1.66 limejengwa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 700 ambazo ni fedha za ndani na ni daraja refu zaidi Afrika Mashariki na la sita kwa urefu barani Afrika.
 
Rais Dkt. Samia ameeleza ujenzi wa daraja hilo kama kielelezo cha uwezo wa Taifa kupanga na kutekeleza miradi mikubwa kwa kutumia rasilimali zake na ni hatua ya kujivunia kama nchi inayojitegemea.
 
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema daraja hilo ni kiungo muhimu kwa Kanda ya Ziwa na kuzifikia nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda, huku akiwaasa wananchi kuhakikisha wananufaika nalo kwa kuongeza uzalishaji, kusafirisha bidhaa, pembejeo na kufikia masoko kwa urahisi.
 
Rais Dkt. Samia pia amepongeza juhudi za vijana Watanzania waliopata fursa ya kushiriki katika ujenzi wa daraja hilo, akiwataka kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata katika ujenzi wa miradi mingine ya kimkakati nchini.
 
Vilevile, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa wananchi kulitunza daraja hilo na kulitumia kwa uangalifu kwa kuwa ni rasilimali kubwa ya Taifa, huku akizielekeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha linafanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara na kuimarishwa ulinzi dhidi ya vitendo vya uharibifu.
 
Hali kadhalika, Rais Dkt. Samia amesema Serikali imekamilisha madaraja mengine makubwa tisa kote nchini tangu mwaka 2021, na ipo katika hatua mbalimbali za kukamilisha miradi mingine saba katika maeneo tofauti nchini, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara zinazounganisha maeneo muhimu ya kiuchumi.
 
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alizindua rasmi Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Mji wa Lamadi katika Wilaya ya Busega, sambamba na kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi mkoani Simiyu.
 
Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi unahusisha sekta za maji, kilimo, mifugo na uhifadhi wa mazingira, ukiwa na lengo la kuiwezesha jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
 
Rais Dkt. Samia amewapongeza wananchi waliotoa maeneo yao kwa hiari ili kupisha utekelezaji wa mradi wa maji, na kuhimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika awamu inayofuata ya utekelezaji wa miradi kama hiyo katika miji ya Maswa na Meatu.
Posted by MROKI On Friday, June 20, 2025 No comments

June 19, 2025

MDAU wa Maendeleo Mkoa wa Iringa, Wakili Sosten Mbendule amempongeza Chifu Adam Sapi Mkwawa II kwa kuwaleta pamoja katika kuadhimisha tamasha la utamaduni la  Wahehe.

Wakili Mbedule amesema tamasha hilo la Wahehe lililoanza Juni 16 na kufikia kilele chake leo Juni 19, 2025 katika kijiji cha  Kalenga mkoani Iriga linasaidia  kudumisha utamaduni wa kabila la Wahehe na kukemea mmomonyoko wa maadili hususani katika suala la mavazi.

Amesema, kuanzishwa kwa tamasha hilo mila, desturi za tamaduni za wahehe zitahimarika kwani zilishaanza kupotea ikiwa ni pamoja na kuhamasisha elimu ya kulinda utu wa mtu.

“Tamasha hili ni lizuri limeleta chachu ya matumizi  ya biadhaa za uzalishaji wa kilimo, utalii na huduma mbalimbali za usafirishaji fedha na bima,” amesema.

Pia limesaidia kuwaleta pamoja vijana, wanawake na wazee  katika kulinda na kuendeleza urithi  wa tamaduni za wahehe nchini.

Katika maadhimisho hayo yamefanyika matambiko ya kimila katika maeneo ya kihistoria ya mto Mkwawa na wahehe kwa ujumla, kutatembelea maeneo ya kihistoria  lengo ni kukuza utamaduni wao.
Posted by MROKI On Thursday, June 19, 2025 No comments
Taswira ya Daraja la J.P Magufuli (Kigongo-Busisi) lenye urefu wa km 3.0 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa km 1.66 ambalo limefunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika eneo la Kigongo, Misungwi mkoani Mwanza tarehe 19 Juni, 2025. Daraja hilo ambalo ni sehemu ya barabara ya Usagara-Sengerema-Geita ni sehemu ya barabara kuu inayoanzia Sirari hadi Mtukula na ujenzi wake ulianza rasmi mwezi Februari, 2020.






Posted by MROKI On Thursday, June 19, 2025 No comments
Wataalamu wa Wakala wa Vipimo wakitoa elimu ya vipimo kwa wadau mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Uwanja wa Chinangali jijini Dodoma. Taswira hizi zilizchukuliwa Juni 18, 2025.



Wakala wa Vipimo (WMA) unaendesha zoezi la kuhakiki mita za umeme zilizofungwa katika viwanda mbalimbali nchini ili kuhakikisha Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inapata mapato stahiki na wenye viwanda wanalipa gharama stahiki kulingana na huduma ya umeme wanaotumia.
Hayo yalibainishwa Juni 18, 2025 na Meneja wa WMA Makao Makuu, Albogast Kajungu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika uwanja wa Chinangali, Dodoma.
Kajungu alisema kuwa hadi sasa WMA imekagua mita za umeme zaidi ya 2,000 huku lengo likiwa ni kuhakiki mita zote zilizo kwenye matumizi katika viwanda vyote nchini katika zoezi lililoanza Mei mwaka huu.
“Hali inaonesha kwamba mita nyingi zilizo kwenye matumizi viwandani ziko vizuri. Chache ambazo tumekuta zina mapungufu, tumewasiliana na Mamlaka husika kwa ajili ya kuzirekebisha na nyingine kuzibadilisha ili kuhakikisha vipimo viko sahihi kwenye eneo hilo,” alisema Kajungu.
Akieleza zaidi, alisema kuwa zoezi hilo la uhakiki linahusisha mita zote za umeme zilizo katika matumizi lakini Wakala imeona ianze na zile zilizoko viwandani kwakuwa zinatumia umeme mkubwa hivyo ikiwa haziko sawasawa, kuna uwezekano wa TANESCO au wenye viwanda kupata hasara.
Aidha, alieleza kuwa zoezi la uhakiki linahusisha pia bidhaa za chuma hususan zinazotumika katika ujenzi kwani kumekuwa na malalamiko katika eneo hilo.
Akifafanua, Kajungu alisema kuwa sekta ya ujenzi hapa nchini inakua kwa kasi ambapo miradi mingi ya ujenzi inayotekelezwa na serikali inatumia bidhaa za chuma hivyo WMA imeona iongeze nguvu kuhakiki bidhaa hizo hususani zinazozalishwa kwenye viwanda vya ndani ili kuhakikisha zina vipimo vilivyo sahihi.
Alisema kuwa wazalishaji wanajitahidi kuzalisha kwa kuzingatia viwango lakini lengo la Wakala hiyo ni kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi zinaendelea kuwa na vipimo sahihi ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara ambayo yanaweza kutokea kwa kutumia bidhaa za chuma ambazo hazikidhi vipimo vinavyokubalika kisheria.
Sambamba na uhakiki wa mita za umeme na bidhaa za chuma, Kajungu alieleza kuwa zoezi hilo la uhakiki pia linahusisha dira za maji zilizo kwenye matumizi kwakuwa ndizo zenye malalamiko yanayohusiana na bili na mengineyo.
Hata hivyo, alibainisha kuwa pamoja na kuhakiki bidhaa zilizo kwenye matumizi, WMA kupitia Kituo cha Vipimo Misugusugu kilichopo mkoani Pwani, pamoja na kazi nyingine, huhakiki mita mpya za umeme na dira mpya za maji ili zinapokwenda kufungwa kwa wateja ziwe zimeshathibitishwa kuwa vipimo vyake ni sahihi.
Kajungu alitumia fursa hiyo kuwaalika wananchi wafike kwa wingi kwenye Banda la Wakala wa Vipimo ili kujipatia elimu kuhusiana na vipimo mbalimbali vinavyotumika ili kuwalinda kwa maana ya kupata thamani ya fedha wanazotoa wanapokwenda kununua bidhaa.
Wakala wa Vipimo ni mojawapo ya Wakala za Serikali yenye dhima ya kutoa huduma za kumlinda mlaji kupitia uhakiki wa vipimo, usimamizi wa vipimo na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Majukumu yake ni kumlinda mlaji na umma kwa ujumla kupitia uhakiki na uthibiti wa vipimo vinavyotumika katika biashara na huduma nyingine ili kuhakikisha kuwa vipimo hivyo ni sahihi na vinatumika kwa usahihi kulingana na Sheria ya Vipimo Sura 340, mapitio ya mwaka 2002 na maboresho yake ya mwaka 2026 pamoja na kanuni zake.
Posted by MROKI On Thursday, June 19, 2025 No comments


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisogeza kitambaa kuashiria ufunguzi wa mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Lamadi, Wilayani Busega wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu tarehe 19 Juni, 2025.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisikiliza taarifa ya mradi wa maji na usafi wa Mazingira wa Lamadi, Wilayani Busega wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu tarehe 19 Juni, 2025.
Shamrashamra za ufunguzi wa mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Lamadi, Wilayani Busega mkoani Simiyu tarehe 19 Juni, 2025.

Shamrashamra za ufunguzi wa mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Lamadi, Wilayani Busega mkoani Simiyu tarehe 19 Juni, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisogeza kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Nyashimo, Busega mkoani Simiyu tarehe 19 Juni, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan 
Posted by MROKI On Thursday, June 19, 2025 No comments
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Leonardo da Vinci Jijini Roma nchini Italia leo tarehe 19 Juni 2025. Makamu wa Rais anatarajiwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Ubia wa Maendeleo kati ya Afrika na Serikali ya Italia (Mattei Plan) utakaofanyika tarehe 20 Juni 2025.





Posted by MROKI On Thursday, June 19, 2025 No comments
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Mkuu wa Idara wa kiwanda cha uchenjuaji madini ya Shaba cha MAST Elimwaria Muro, wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa kiwanda hicho cha MAST, kilichopo Chunya mkoani Mbeya, Juni 18, 2025.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akioneshwa mashine ya kupimia ubora wa madini ya shaba na Mhandisi wa Madini wa kiwanda cha uchenjuaji madini ya Shaba cha MAST Hassan Kondo, wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa kiwanda hicho cha MAST, kilichopo Chunya mkoani Mbeya, Juni 18, 2025. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa Mbeya Juma Homera.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi kuzindua kiwanda cha uchenjuaji madini ya Shaba cha MAST, wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa kiwanda hicho, kilichopo Chunya mkoani Mbeya, Juni 18, 2025. Kutoka kushoto ni Rais na Mtendaji Mkuu Mkuu wa kiwanda hicho Dkt. Glendon Archer, Mkuu wa Mkoa Mbeya Juma Homera na kulia ni Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipeana mkono na Rais na Mtendaji Mkuu Mkuu wa kiwanda cha uchenjuaji madini ya Shaba cha MAST, Dkt. Glendon Archer, wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa kiwanda hicho cha MAST, kilichopo Chunya mkoani Mbeya, Juni 18, 2025.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kuzindua kiwanda cha uchenjuaji madini ya Shaba cha MAST kilichopo Chunya mkoani Mbeya, wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa kiwanda hicho, Juni 18, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
**************
RAIS DKT. SAMIA AMEDHAMIRIA KUIENDELEZA SEKTA YA MADINI-MAJALIWA
 
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa uzinduzi wa kiwanda cha kwanza cha kisasa cha kuchenjua shaba ni ishara ya dhamira ya dhati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuisimamia na kuendeleza sekta ya madini.
 
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchenjua tani 31,200 za mashapo ya shaba kwa mwezi kitaleta manufaa kwa Wana-chunya na Taifa kwa ujumla.
 
Amesema hayo jana (Jumatano Juni 18, 2025) alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia katika uzinduzi wa kiwanda cha Mineral Access Systems Tanzania Ltd (MAST), kilichopo katika kata ya Mbugani, Chunya mkoani Mbeya.
 
“Uthubutu na ubunifu wa Rais wetu Dkt. Samia ndio uliochagiza kwa kiasi kikubwa maendeleo katika Sekta ya Madini, wawekezaji hawa wamekuja kwasababu ya mazingira mazuri ya uwekezaji”.
 
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Wizara ya Madini na Taasisi mbalimbali nchini ziendelee kusimamia wawekezaji ili wanapofanya shughuli zao wazingatie Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi ikiwemo kulipa kodi stahiki, kutunza mazingira katika maeneo wanapofanya shughuli zao. “Hakikisheni pia wanzingatia Usalama wa wafanyakazi na raia wanaozunguka maeneo ya uwekezaji”.
 
“Ninyi pia wamiliki wa viwanda na wawekezaji wote hakikisheni mnaendesha shughuli zenu kwa kuzingatia matakwa ya sheria na hasa kwenye utunzaji wa mazingira mkishirikiana na halmashauri wenyeji, kijiji na Wilaya”.
 
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wawekezaji kuweka kipaumbele cha ajira kwa wakazi wanaozunguka maeneo ya uwekezaji ikiwemo za kitaalamu na hata ambazo sio za kitaalamu.
 
 “Ametuambia mkurugenzi mtendaji ameanza na vijana takribani 200 lakini wapo pia ambao wanakuja kila siku na tunaamini atapanua wigo kuajiri, tunataka kuona vijana wa Chunya wakifanya kazi hapa”.
 
Naye, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ni sehemu ya utekelezaji wa sera na sheria ya madini inayotaka kuhakikisha madini ya Tanzania yanachimbwa, yanachakatwa na yanaongezwa hapa hapa nchini kabla ya kuuzwa nje ili kupanua wigo wa fursa za kiuchumi.
 
Ameongeza kuwa kiwanda cha MAST ni moja kati ya viwanda tisa vilivyowekwa kwenye mpango wa kujengwa kwa ajili ya kuongeza thamani ya madini kabla ya kuuzwa nje. “Kiwanda hiki bado hawajafikia hatua ya kutengeneza bidhaa za mwisho lakini ndio mpango wao, watatengeneza mpaka chuma za kutengenezea waya za umeme na nyama zilizopo kwenye magari”.
 
Juhudi hizi ni sehemu ya mpango wa taifa wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji wa madini barani Afrika, na kuongeza uwezo wa kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani badala ya malighafi.
 
Kwa upande wake Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya MAST Dkt. Glendon Archer amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ni mwanzo wa uchimbaji n uendelezaji wa sekta ya madini nchini Tanzania na kwamba kampuni hiyo inampango wa kujenga viwanda vingine Dodoma na Arusha.
 
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania, Viongozi wa Serikali wametupa ushirikiano mkubwa sana na ndio maana tumefika hapa leo”.
 
Kiwanda hicho ni matokeo ya uwekezaji wa zaidi ya dola za marekani milioni 10.
Posted by MROKI On Thursday, June 19, 2025 No comments





Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete amefungua 
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama Cha Waajiri (ATE) mjini Dar Es Salaam.

Mkutano huo ulifunguliwa Juni 18,2025 ambao ulitanguliwa na taarifa za kiutendaji za mwaka na kongamano kujadili mabadiliko ya sheria za kazi na athari yake kwa Waajiri na Waajiriwa katika kuleta Tija. 

Waziri Kikwete alipata nafasi ya kushiriki na kusikia mafanikio na changamoto zilizomaliza na haswa hali ilivyokuwa kabla na baada ya mabadiliko ya sheria. 

Aidha, alitumia mkutano huo kueleza  nafasi ya serikali katika utatu wa mashirikiano baina ya wadau wakuu watatu wa Kazi ambapo katika hotuba yake ameeleza nia ya mabadiliko hayo na kuwashukuru sana ATE kwa ushiriki wao katika kuhakikisha tunakuwa na sheria nzuri za kazi na kusimamia utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya Kimataifa ya Wafanyakazi ambayo Tanzania ni Mwanachama wa Mikataba hiyo.

Pia nilitumia nafasi hiyo kuwashukuru sana wadau wetu wa maendeleo shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kuendelea kushirikiana nasi na pia kuwapa salamu za hongera toka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa ILO Cde. Gilbert F. Houngbo.
Posted by MROKI On Thursday, June 19, 2025 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo