Sasa hii siku nayo naikumbuka. Ni moja ya zile siku ambazo kwa bahati unakutana na mazunguzo yanayodumu, na baadaye yanakushangaza. Kama si kwamba yanakupa wivu wa kujaribu, basi yanakupa changamoto ya kupiga hatua moja.
Tuko shambani sasa, na tunapalilia mazao. Kwa kawaida tulikuwa tunachanganya upandaji wa mazao. Wakati mwingine Mahindi na maharagwe na wakati mwingine kuna viazi. Basi ili mradi tu kwamba, maisha ya kijijini hatukosi mazao shambani.
Siku hii, tukipalilia kila mmoja anataka kale kajembe anakotumia Bibi (…tulikaita kahonga).Tunaona kale ni kakali na kanafanya kazi haraka na vyema zaidi. Lengo ni kwamba, kila mmoja amalize kipande chake (Ngwe) mapema aende nyumbani. Japokuwa hii ilikuwa haitokei mara kwa mara, kwakuwa hata ukimaliza mapema utaelekezwa na Bibi kusaidia wenzako ili muende nyumbani pamoja. Unaweza kuondoka mapema iwapo tu umetumwa utangulie nyumbani uandae chakula, au ukachote maji, au ukashughulikie ng’ombe au yafananayo na hayo.
Zaidi ya hapo, ukimaliza kipande chako utapewa kazi nyingine mpaka wengine nao wawe tayari kuondoka kurudi nyumbani. Lakini kiukweli, kwani unawaacha wengine shambani ili nini! Hekima ya Bibi ilikuwa kubwa. Lazima kujali na kuchukuliana na wenginge.
Juhudi za kuwahi jembe la Bibi ni asubuhi wakati tunaenda shambani. Kumbe juhudi hizi Babu anaziangalia tu kimya kimya. Bibi yeye, wala hana habari. Jembe litakalotua mkono mwake, ndilo hilo hilo atakalotumia. Kwa umahiri wake katika kupalilia, hakukuwa na tofauti ya majembe yetu au lile ambalo tuliliita la kwake. Japo kiukweli, lile jembe la Bibi, lilikuwa la zamani kidogo. Kwakuwa limetumika kwa muda, lilikuwa limenoleka sana. Hivyo lilikuwa na ukali katika kukata majani kuliko yale mapya.
Nadhani Bibi aliamini kwamba, hata hayo mapya, yakitumika yatakuwa kama yale ya zamani. Yumkini, jembe lake nalo kuna wakati lilikuwa jipya. Sisi wakulima wapya wakati huo hatukuwa na hiyo hekima. Si ajabu kutukuta tukinoa majembe kwa tupa au mawe kama tulivyonoa visu na mapanga. Yaani kuna mambo mengine ukikumbuka unabaki unacheka tu!
Basi sasa, muda wa mazungumzo na Babu ukafika. Hii ni baada ya shughuli za shamba. Ilikuwa ni nadra kidogo Babu kuanza kutusimulia hadithi huku bibi naye yupo ametulia zake pamoja nasi. Mara nyingi Bibi atakuwa kwenye shughuli zake nyingi kuandaa mambo mbalimbali na kuelekeza kazi hizi na zile. Nikudokeze tu jambo. Babu yangu alikuwa mtoto wa mwisho kuzaliwa kwa mama yake, na Bibi yangu alikuwa Mtoto wa kwanza katika familia yao. Sina uhakika kama kuna maana yeyote kwenye hili. Lakini Tutaliangalia wakati mwingine. Ninachojua ni kwamba ilikuwa ‘Kapo’ ya pekee sana (Usicheke bwana we..!).
Babu anatuangalia kidogo na mapozi yake ya kichungaji. Anasema zamani kulikuwa na kijiji fulani (sikumbuki kama alitaja jina wala kilipokuwa). Katika kijiji kile, kulitokea njaa kubwa sana. Nadhani ni kutokana na ukame. Zamani njaa ilikuja kwa sababu nyingi. Mojawapo ni ukame, mafuriko, au hata vita. Katikati ya njaa ile, watu wakasikia kwamba, kijiji kingine mbali kidogo kuna neema. Chakula kipo na watu wanauza vyakula sokoni. Kila familia ikapanga kutuma watu kwenda kwenye soko la Kijiji kile ili kununua na kuleta chakula nyumbani (Kushuma).
Familia mbili zinaingizwa kwenye simulizi. Familia moja ikamtuma na kijana wao kwenda kuleta chakula. Kijana yule akajiandaa na kuondoka kwenda kijiji chenye neema ili kuleta chakula. Kwa wakati huo, walisafiri kwa miguu. Basi kijana akaondoka na kuanza safari yake. Hatua moja, hatua nyingine, mwendo na jasho hata kufika. Sina uhakika kama alibeba mfuko, gunia, au kikapu cha kubebea, au alivikuta huko. Haya maswali ningeuliza wakati huo. Lakini, mwendo ulianza.
Familia nyingine nayo ikaamua kumtuma kijana wao kwenda kuleta chakula. Ikamuelekeza kusafiri safari ile ili kuleta furaha nyumbani. Nyumba yenye chakula bwana, mna uhakika wa usingizi kama hakuna makandokando menginge. Tuachane na hilo. Basi kijana naye akakubali kusafiri safari ile.
Pamoja na ukubali wake, Kijana wa familia hii ya pili, akatulia kidogo na kuanza kujenga hoja. Hoja yake ilikuwa na mantiki. Akawakumbusha wanaomtuma kwamba, safari ile ni ndefu na inabidi kusafiri kwa miguu. Lakini kwa bahati mbaya, hana viatu. Akifanya safari ile, bila viatu huenda miguu itachubuka, itachomwa na miiba, atajikwaa, au hata miguu yake itaota magaga (sina uhakika kama hiki ni Kiswahili sanifu).
Hivyo, akaweka ombi mbele yao kwamba, wamtafutie viatu ili safari yake isikwame na huenda isiwe ya taabu kiasi cha kuikosea raha. Hoja ikajadiliwa, na mfano ukatolewa wa namna ambavyo kijana wa jirani alivyokwenda bila kujali kwamba ana viatu au la. Lakini kijana akaendelea kusihi kwamba, viatu ni muhimu. Hoja ikashamiri na kushikiliwa.
Sasa wazee wafanyeje? Wenyewe hawana nguvu kusafiri kwenda safari ile. Lakini wanahitaji chakula. Ikabidi wakubaliane na kijana na viatu vikatafutwa. Sijui walivipata wapi. Nami sikuwa na hekima yakumuuliza msimulizi wangu maswali mengi. Kwanza naanzaje kuhojiana naye yule rafiki yangu. Asije akakatisha simulizi akanituma majani ya ng’ombe bure! Basi lakini kwa simulizi, viatu vilipatikana.
Kijana sasa ana viatu mguuni, na mwendo ameukamata. Hatua moja, hatua nyingine, mwendo na jasho kuelekea kuleta chakula. Akiwa njiani, akakutana na kijana yule wa kwanza. Hao wawili wakasabahiana kama ilivyo ada ya watu wanaofahamiana na wasio na uhasama. Kijana wa kwanza alikuwa amebeba mzigo wake wa chakula na yu safarini kurudi nyumbani. Kijana wa pili akamuuliza hali ikoje utokako? Akajibiwa hali ni njema. Chakula kipo ila wanunuzi si wachache pia.
Basi wakaagana kila mmoja kwa mwelekeo wake. Kijana huyu wa pili akafika safari yake. Lakini jambo moja likajitokeza. Nalo ni hili…Chakula kimemalizika. Lahaula..! Kwakuwa kulikuwa na wanunuzi wengi basi waliokuwa na chakula sokoni waliuza chote. Hivyo, wakati kijana huyu anafika, wanunuzi wameshanunua na kumaliza chote. Sasa afanyeje? Basi, inabidi aanze safari ya kurudi nyumbani mikono mitupu akiwa amesheheni huzuni na hofu moyoni. Anajiuliza maswali, habari hii itapokelewaje nyumbani? Nini hatima ya familia yao kuhusiana na njaa?
Basi, hatua moja, hatua nyingine, mwendo na jasho hata kufika nyumbani. Hapa ndipo penye ugumu. Kwa kawaida ni furaha kufika nyumba, na pia ni furaha kupokea arudiye nyumbani toka safari ya mbali (Japo ni kweli kwamba hili si la wakati wote maana kuna yule Baba mmoja alitoka safari ya mbali akiwa amevimba yote mapaja na kutetemeka mwili)! Lakini kwa kijana huyu, hilo lilikuwa mbali na tofauti kwake na kwa familia yake. Badala ya kurudisha furaha nyumbani, alirudi na huzuni na hofu. Safari ilikamilika, lakini chakula hakikupatikana. Hili si jambo tamu nyumbani. Huenda, hata liliteta msongo wa mawazo, si kwake tu, bali na kwa wale waliokuwa na matarajio ya kushiba.
Katika simulizi hii, familia moja ina chakula lakini haina viatu. Kwao, shibe ni ya uhakika. Familia ile nyingine, viatu vipo lakini njaa nayo imekuwa mwanafamilia. Muda uliotumika kujadili hoja ya viatu, umegharimu neema ya shibe.
Basi, simulizi inaisha na kuleta tafakuri: Miguu yenye shibe na Viatu vyenye njaa.
Kumbe tufanyeje sasa? Basi, salaam ni hizi…anza na ulichonacho.
Nduguyo
Jim Yonazi
0 comments:
Post a Comment