Baada ya SALAAM YA LEO kutoka kwa Dkt. Jim J. Yonazi kuichapisha katika gazeti tando hili imemtafakarisha sana Nguli wa mashairi nchini Lwaga Mwambande almaarufu KiMPAB na kuamua kuandika shairi usiku kabla jua kuchomoza kutokana na kisa hicho alichosimulia Dkt. Yonazi J. J ambaye ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), ambapo alisimulia kisa alichosimuliwa na babu yake na kukipa jina "MIGUU YENYE SHIBE, NA VIATU VYENYE NJAA"
Kisa hicho kina funzo kubwa sana kwa mambo mengi ya kisiasa, uchumi na kijamii. Kwani maamuzi ya haraka ya jambo unalotakiwa kulifanya au kulitekeleza yanaweza kukupa mafanikio.
Tupate ujumbe wa LWAGA MWAMBANDE kupitia ushairi huu.
Nani kofi tumzabe, na aliyefanya waa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
La mgambo limelia, yatuandama balaa,
Njaa kubwa meingia, tuna shangaashangaa,
Wale wanafikiria, kitako hawakukaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Wakamtuma kijana, kwenda kukabili njaa,
Kwa jirani wameona, kwamba chakula chajaa,
Huko kinauzwa sana, nao pesa zimejaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Na nyingine familia, kikaoni walikaa,
Kijana wakamwambia, awaepushe balaa,
Chakula wanunulia, wasijekufa kwa njaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Kijana akafikiri, kiliko mbali balaa,
Asipokaa vizuri, miguu itachakaa,
Akajenga hoja nzuri, viatu aweze vaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Wazee jipigapiga, kutafuta vya kuvaa,
Njaa ilivyowaroga, wakapata akavaa,
Akaondoka kwa swaga, hapo wala hakukaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Anapokwenda njiani, kachoka amechakaa,
Aliyeenda zamani, anarudi amejaa,
Chakula kwenye gunia, nyumbani kitawafaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Naye kwa kuzungumza, hicho chakula cha njaa,
Kasema bila kukwaza, wanunuzi wamejaa,
Waweza kukimaliza, akimbie akipaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Wa viatu mbiombio, kijijini akajaa,
Lakini za kwake mbio, kakumbana na balaa,
Kama angue kilio, kimekwisha chote daa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Atarudije nyumbani, na viatu amevaa,
Wakati ni masikini, hana chakula cha njaa,
Kumwelewa hakuoni, na viatu amevaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Muda kusaka viatu, aliitisha balaa,
Sasa takula viatu, vile kabaki na njaa,
Nyumbani tayari kutu, vitu watu watakaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Kwa masuala mengine, sikae kujiandaa,
Nyumbani hakuna tone, watu wengi wachakaa,
Hebu jitume uone, itakavyokuwa waa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Utakapofanya kitu, uache kukaakaa,
Kiingie wewe mtu, giza itawaka taa,
Mara kutakuwa kwatu, mema kwako yakijaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Fikiri mgonjwa sana, unatapika balaa,
Wabaki wagunaguna, huku wazidi chakaa,
Utakufa wajiona, mzembe umezubaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Ukichukua hatua, sipitali kwenda shaa,
Shida wakaing’amua, na tiba iliyojaa,
Mara waweza tanua, na afya yako kung’aa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Kuna mambo ya haraka, si ya viatu kuvaa,
Wenda haraka haraka, hata wakikushangaa,
Kuna muda utafika, wataelewa ahaa,
Maamuzi ya haraka, aghalabu huokoa.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com
0767223602
BOFYA LINK HII HAPA KUSOMA KISA CHA DKT YONAZI J. J "MIGUU YENYE SHIBE, NA VIATU VYENYE NJAA"
0 comments:
Post a Comment