

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuenzi maisha ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kufanya kazi kwa bidii ili kujenga Taifa na kujiletea maendeleo.
Rais Dkt. Samia amesema hayo leo wakati akizindua kitabu cha ’Mwalimu Julius Nyerere: Photographic Journey’ katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino. Uzinduzi wa
kitabu hiki ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.
Rais
Dkt. Samia amesema kitabu hiki kimebeba masuala mengi kuhusu maisha ya Hayati
Mwalimu Nyerere ambae aliacha alama isiyofutika kwenye historia ya nchi kwa
kuwahimiza Watanzania kuwa wamoja, kushikamana na kufanya kazi kwa bidii kwa
maendeleo ya nchi yetu.
“Nilipotakiwa
kuandika dibaji na maneno ya kufunga ya kitabu hiki sikusita. Nimefurahi
kuzinduliwa leo sambamba na kutoa nishani kwa viongozi walioutumikia Muungano
wetu ... Mwalimu alikuwa kinara wa falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea na
Maendeleo Jumuishi au Maendeleo ya Watu. Falsafa hiyo imeendelea kuwa msingi wa
uongozi wetu”. amesema Rais Dkt. Samia.
Rais
Dkt. Samia pia amesema Hayati Mwalimu Nyerere aliamini kuwa nguvu ya Tanzania
ipo kwenye umoja na mshikamano wa watu wake na alisimamia kwa uthabiti mkubwa
yale aliyoyaamini. Kitabu kinatukumbusha
namna alivyojenga Taifa jumuishi bila ubaguzi wa rangi, kabila au majimbo hivyo
kuwezesha watu tofauti kutoka sehemu tofauti kufanya kazi pamoja.
Kipekee
Rais Dkt. Samia amemtaja Mwalimu Nyerere kuwa ni kiongozi aliyeamini katika
wanawake katika kipindi ambacho wanawake hawakuthaminiwa, aliamini wanawake
wanapopata nafasi na kutoa mchango wao wanafanya mambo makubwa kwa jamii.
Katika
hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amegusia umuhimu wa kutunza kumbukumbu za
viongozi kwa mustakabali wa kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ulioasisiwa na viongozi wawili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid
Amani Karume, ambapo aliweka wazi kuwa changamoto za Muumgano zimetatuliwa kwa
kuenzi falsafa za waasisi wake walioamini katika umoja na mshikamano.
Kitabu
hiki ni sehemu ya juhudi ya Serikali ya Awamu ya Sita kuenzi na kutunza
kumbukumbu za viongozi waliolitumikia taifa kwa nyakati tofauti.
Akizungumzia
utekelezaji wa maono ya Mwalimu Nyerere, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Mwalimu
Nyerere alitaka kuwawezesha wahitimu kujitegemea, ndiyo maana Serikali ya Awamu
ya Sita imeanza kutekeleza Sera ya Elimu iliyoboreshwa ili wahitimu waweze
kuajiriwa na kujiajiri.
Katika
hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amewaasa Watanzania kudumisha amani kwani
migogoro na uvunjifu wa amani na mivutano haitaleta maendeleo ya kweli, hivyo amewataka
wananchi washikamane kujenga Taifa ili kuleta ustawi.
Awali,
Rais Dkt. Samia alitunuku Nishani za Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Pili na Nishani za Kumbukumbu ya Muungano Daraja
la Tatu kwa Viongozi 8 ambao katika kipindi cha
uongozi wao walijitoa bila kusita kudumisha Muungano na wameendelea kuonesha
maadili bora na kuwa mfano wa kuigwa hata baada ya utumishi wao.
Viongozi waliotunukiwa Nishani ya Kumbukumbu
ya Muungano Daraja la Pili ni: Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe.
Dkt. Mohamed Ali Shein; Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd;
Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa; Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.
Mizengo Kayanza Peter Pinda; Spika Mstaafu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhe.
Pandu Ameir Kificho; Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Profesa Ibrahim Hamisi
Juma na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Hayati Balozi John William Kijazi.
Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano Daraja la
Tatu imetunukiwa kwa Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania
Bara, Ndg. Philip Japhet Mangula.
0 comments:
Post a Comment