Nafasi Ya Matangazo

April 30, 2025









WAZIRI wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde (MB) ametoa maelekezo matano kwa Menejimenti ya  Tume ya Madini hasa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuzingatia na kusimamia  sheria katika utekelezaji wa majukumu yao na kufikiri nje ya boksi ili kuwa na kitu cha ziada katika kuendeleza Sekta ya Madini.
 
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Aprili 30, 2025 jijini Dodoma kwenye ufunguzi wa kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini ambapo  amewataka watendaji kuwa wabunifu katika maeneo yao, washirikiane, mkoa mmoja na mkoa mwingine pamoja na kushauriana.
 
“Kwenye Sekta ya Madini  ukiweka sheria pembeni utaivuruga sekta,  kuna wakati matumizi ya busara huwa yanahitajika lakini sheria kwanza, kaisimamieni, kesho keshokutwa mtu atakuuliza jambo lingine lolote dhamira yako ilikuwa nini na sheria inasema nini, kasimamie sheria kwanza na kama kuna maelekezo tofauti yasitokane na wewe, wewe katimize  wajibu wako wa kusimamia sheria ni muhimu sana,”amesema Waziri Mavunde.
 
Agizo la pili ambalo amelitoa Mheshimiwa Mavunde ni kutaka ubunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
 
“Nataka mkawe wabunifu, tumenunua magari 101 mengine yanakuja pikipiki 140  Rais Daktari Samia Suluhu Hassan ametupatia nyenzo, nataka mfikiri nje ya boksi  nini ufanye kwenye eneo lako ili sekta  iweze kushamiri zaidi, isiwe ‘business as usual’ tunatamani kuona kila mtu katika eneo lake anajitahidi,”amesema.
 
Katika  hatua nyingine Mheshimiwa Mavunde amewapongeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa ukusanyaji wa maduhuli na kuwataka kutorudi nyuma  na kuhakikisha kila mmoja anavuka lengo alilopangiwa na kuongeza kuwa,
 
“Mjitahidi kutafuta njia za kuongeza makusanyo pasipo kuleta athari kwa watu mnaowasimamia. Zipo njia nyingi za kufanya simamieni hilo, sisi tunaingiza fedha nyingi sana katika mfuko mkuu wa Serikali, miradi inayokuja mikubwa naamini tutafanya vizuri zaidi.
 
Katika agizo la nne la uadilifu Waziri Mavunde ameeleza kuwa hivi karibuni Sekta ya Madini imekuwa na utulivu pasipo kuwepo na malalamiko yoyote na kuwataka Maafisa  Madini Wakazi wa Mikoa kuendelea kutenda haki pasipo kuonea wadau wa madini na kutatua migororo na changamoto zinazowakumba wadau wa madini.
 
Amewasisitiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanatatua migogoro kwa kufuata haki ili kujenga imani na wachimbaji wa  madini na kuendelea kutoa elimu kuhusu Sheria na Kanuni za  Madini ili kupunguza migogoro kabisa.
 
Akitoa agizo la Tano Mheshimiwa Mavunde amesema kuwa ili kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini, imeundwa kamati maalum ya kuwajengea uwezo watanzania kushiriki kikamilifu katika Sekta ya Madini ili baadaye wawe wachimbaji wakubwa wa madini na kuelekeza Watendaji wa Tume ya Madini kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo.
 
“Wanapokuwepo wachimbaji wakubwa ambao ni wazawa faida lukuki zinapatikana ikiwa ni pamoja na ajira, mapato na ongezeko la manunuzi ya bidhaa na huduma za ndani ya nchi,” amesema  Waziri Mavunde.
 
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani madini nchini ambapo mpaka sasa wawekezaji wengi wamejitokeza kwenye ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani katika mikoa ya kimadini ya Chunya, Dodoma, Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Rukwa na Lindi.
 
Amesema kutokana na utendaji mzuri wa Sekta ya Madini hasa mchango wake kwenye Pato la Taifa kufikia asilimia 10.1 nchi ya Kenya kupitia Waziri wa Madini na Uchumi wa Bluu, Mheshimiwa Ali Hassan Joho wameomba kuja kujifunza nchini Tanzania.
 
Aidha, amewataka wachimbaji wa madini waliopewa leseni kuzifanyia kazi na kwa ambao hawajazifanyia kazi hatua mbalimbali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuandikiwa hati za makosa na kufutwa kwa mujibu wa sheria.
 
 
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba akizungumza katika mkutano huo amewataka Viongozi wa Tume ya Madini kuendelea kuimarisha upendo sambamba na kushirikiana ili Sekta ya Madini iendelee kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.
 
Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha akielezea hali ya makusanyo ya maduhuli katika Tume ya Madini amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 753.8 sawa na asilimia 85.45 ya lengo kilikusanywa.
 
Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 kuanzia mwezi Julai hadi Aprili 29, 2025 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Bulioni 862.64 ambacho ni sawa na asilimia 86.53 ya lengo la Shilingi Trilioni Moja.
 
“Tunaamini kiasi kilichobaki tutakikamilisha ifikapo Juni, 30 mwaka huu kwa kuongeza nguvu na ubunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli na udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato,” amesisitiza Kamishna Mwasha.
Posted by MROKI On Wednesday, April 30, 2025 No comments






NAIBU Waziri wa Madini, Mhe.  Dkt. Steven Kiruswa amesema chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Sekta ya Madini imepiga hatua kubwa.

Dkt. Kiruswa ameyasema hayo leo Aprili 30, 2025 wakati akifunga Kikao cha Manejimenti ya Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma.

Amesema, kutokana na usimamizi mzuri wa Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Naibu Katibu Mkuu, Msafiri Mbibo mafanikio makubwa yamepatikana katika Sekta ya Madini yaliyopelekea mchango wake kufikia asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa.

Katika hatua nyingine, amewapongeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa kasi ya ukusanyaji wa maduhuli na kuwataka kuimarisha ushirikiano kati yao na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika Sekta ya Madini na kutatua kero za wadau wa madini. 

"Nitumie nafasi hii kuwakumbusha  umuhimu wa kushirikiana kutekeleza mikakati ya Usimamizi wa Sekta ya Madini ili sote kwa pamoja tuweze kufurahia ushindi wa kufikia malengo tuliyojiwekea,"amesema Dkt. Kiruswa na kuongeza,

*Nitoe rai kwenu kuongeza ushirikiano, mshikamano na upendo katika utendaji wa kazi ili tujenge nguzo imara itakayoendelea kutoa matokeo bora kwa Wizara yetu na kwa manufaa ya Taifa letu," amesema.

Aidha, amewapongeza Menejimenti na Watumishi wa Tume kwa juhudi za ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025  ambapo kuanzia kipindi cha mwezi Julai 2024 hadi Aprili 29, 2025 Tume imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 862.64 ikiwa ni asilimia  86.53 ya lengo la mwaka 2024/2025.
Posted by MROKI On Wednesday, April 30, 2025 No comments






Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)  kuongeza kasi ya uendelezaji wa Vitalu vya utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia ikiwemo Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi Wembere, Songo Songo Magharibi na Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) ili nchi iendelee kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati kwa ajili ya soko la ndani na nje.

Ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizindua Mkakati wa Muda Mrefu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wa miaka 25 (2024/25 hadi 2049/50) ambao umeweka mipango na malengo makubwa ya kuleta uhakika wa upatikanaji wa nishati nchini, mkakati ambao utaisaidia nchi kutumia kikamilifu rasilimali za mafuta na gesi zilizopo katika maeneo mbalimbali. 

”Tunapozindua Mpango Mkakati huu wa miaka 25, ni muhimu tutambue kuwa  jukumu muhimu la TPDC ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati nchini. Ni muhimu sisi sote hapa tukumbuke kuwa Sekta ndogo ya Mafuta na gesi ina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya Taifa hili.” Amesema Dkt. Biteko

Aidha, Dkt. Biteko ameiagiza TPDC kuimarisha mtandao wa mabomba na mifumo ya usambazaji wa gesi nchini ikiwemo kupitia teknolojia za Mini-LNG na CNG ili kuwafikia wananchi wengi ambao wapo mbali na Bomba la Usafirishaji wa Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ili kusaidia kuwafikishia watanzania manufaa yatokanayo na matumizi ya gesi asilia.

Pia ameitaka kujiimarisha kifedha ili kuweza  kutekeleza miradi mbalimbali kwa kubuni mifumo ya ubunifu ya utekelezaji wa miradi, kuboresha shughuli za kibiashara, na kuendelea kupunguza utegemezi kwa ufadhili wa Serikali ambapo ameipongeza kwa kuanza kujilipa mishahara kwa kutegemea fedha za Shirika.

Vilevile ameitaka TPDC kudumisha uwazi, uwajibikaji, na kuzingatia kanuni za mazingira, jamii, na utawala (ESG) na kufanya kazi kazi kwa karibu na kampuni za kimataifa za nishati, wawekezaji binafsi, na wadau wa maendeleo ili kuvutia mtaji, utaalamu, na teknolojia inayohitajika kwa mafanikio ya mpango uliozinduliwa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameendelea kusisitiza kuhusu miradi ya Mafuta na Gesi Asilia kutopuuza jamii zinazozunguka miradi hiyo kwani jamii hizo zinapaswa kuona manufaa ya rasilimali zilizopo katika maeneo hayo na wao wakiwa ndio walinzi wakuu wa miradi hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi.

Dkt. Biteko amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuendeleza Sekta ya Nishati ambapo kupitia uongozi wake, ametekeleza miradi mingi ikiwemo kukamilisha Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati ya mafuta na gesi asilia hapa nchini na hivyo kuleta maendeleo endelevu ya Taifa na wananchi kwa ujumla. 

Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko ameiagiza TPDC kuhakikisha wanalipa kipaumbele suala la nishati hiyo  kwa kuendelea kusambaza gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya kupikia na hivyo kupunguza hewa ukaa na uchafuzi wa mazingira kutokana na matumizi ya mkaa na kuni.

Pia ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TPDC pamoja na Kampuni zake tanzu kwa juhudi za kuhakikisha Tanzania inaenda kujipambanua kama kitovu cha nishati ya mafuta na gesi asilia ndani na nje ya Tanzania.

Kwa  upande wake, Waziri wa Maji, Nishati na Madini  katika Serikali ya Mapiduzi Zanzibar, Shaib Kaduara ameeleza kuwa mkakati huo unatoa mwanga wa kukua kwa uchumi wa watanzania na kielelezo cha mafanikio yanayopigwa katika Sekta ya Nishati akisisitiza kuwa amani na umoja ndiyo msingi wa maendeleo.

Aidha, amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dkt. Doto Biteko kwa maendeleo yanayofanyika na kuisimamia vyema Sekta ya Nishati.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuwa, kuzinduliwa kwa mpngo huo kunaonyesha jinsi nchi nchi inavyopiga maendeleo kwani mipango ya muda mrefu haiishii katika ngazi ya kitaifa tu bali hata katika ngazi za Taasisi ili kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake.

Amesema kuwa kuzinduliwa kwa mpango huo kunatoa mwanga kwa miradi ya Gesi Asilia kufika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Dodoma akieleza kwamba Mkoa upo tayari kupokea miradi ya gesi asilia kwa ajili matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia na kuendesha vyombo vya moto ikiwemo magari.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Balozi Ombeni Sefue alisema kuwa Mpango Mkakati huo wa muda wa miaka 25 unakwenda sambamba na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuhusu masuala ya nishati, unalingana kwa karibu na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hasa katika maeneo ya kuimarisha sekta ya nishati kama kichocheo kikuu cha uchumi wa viwanda, maendeleo ya miundombinu, kukuza matumizi ya teknolojia bunifu, kuongeza ajira na mapato ya Serikali, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, safi na nafuu kwa Watanzania wote.

“Kwetu sisi, hili siyo andiko tu kama maandiko mengine ya awali bali ni mwongozo madhubuti wa kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Nishati ya kufanikisha upatikanaji na usalama wa nishati na hivyo kuboresha maisha ya watanzania na kukuza uchumi endelevu.” Amesema Balozi Sefue

Ameeleza kuwa, kupitia Mpango mkakati huo, TPDC inakusudia kuongeza matumizi ya gesi asilia nchini kutoka matumizi ya kawaida kama uzalishaji wa umeme, viwandani, kupikia majumbani  na nishati mbadala kwa magari kwenda kwenye matumizi ya kuongeza thamani kama vile kutumia gesi asilia kama malighafi katika viwanda vya petrokemikali, ikiwemo uanzishaji wa kiwanda cha mbolea.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, Wawakilishi wa Wakuu wa Mikoa ya Tanga na Tabora, Wajumbe Kamati mbalimbali za Bunge wakiongozwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo,  Watendaji kutoka kampuni zinazofanya uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia pamoja na Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini ya Wizara.
Posted by MROKI On Wednesday, April 30, 2025 No comments
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza jambo wakati aliposhiriki mjadala ulioandaliwa na Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na masuala ya usawa wa kijinsia (UN  Women), uliojikita kujadili namna ya kupata fedha kwa ajili ya kupunguza na kuondoa kabisa pengo la kijinsia katika uchumi na kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi wenye kauli mbiu isemayo “Kutoka Beijing hadi FfD4: Kuunganisha Ahadi Kupitia Ushirikiano wa Wadau kwa Usawa wa Kijinsia, Uwezeshaji wa Kiuchumi wa Wanawake na Maendeleo Endelevu”, uliofanyika Jijini NewYork nchini Marekani.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (Kushoto) na Mkurugenzi wa Sera, Programu, Divisheni ya ushirikiano wa Kimataifa wa UN Women, Bi. Sarah Hendriks wakifuatilia mjadala ulioandaliwa na Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na masuala ya usawa wa kijinsia (UN  Women), uliojikita kujadili namna ya kupata fedha kwa ajili ya kupunguza na kuondoa kabisa pengo la kijinsia katika uchumi na kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi wenye kauli mbiu isemayo “Kutoka Beijing hadi FfD4: Kuunganisha Ahadi Kupitia Ushirikiano wa Wadau kwa Usawa wa Kijinsia, Uwezeshaji wa Kiuchumi wa Wanawake na Maendeleo Endelevu”, uliofanyika Jijini NewYork nchini Marekani.


Na Benny Mwaipaja, New York
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kutafsiri kwa vitendo ahadi za Beijing+30 kuelekea Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FFD4), utakaofanyika kuanzia tarehe 30 Juni hadi 3 Julai 2025, Sevilla nchini Uhispania.

Dkt.Nchemba ameyasema hayo Jijini NewYork nchini Marekani, aliposhiriki mjadala ulioandaliwa na Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na masuala ya usawa wa kijinsia (UN Women), uliojikita kujadili namna ya kupata fedha kwa ajili ya kupunguza na kuondoa kabisa pengo la kijinsia katika uchumi na kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi wenye kauli mbiu isemayo “Kutoka Beijing hadi FfD4: Kuunganisha Ahadi Kupitia Ushirikiano wa Wadau kwa Usawa wa Kijinsia, Uwezeshaji wa Kiuchumi wa Wanawake na Maendeleo Endelevu”.

Alizitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuwawezesha wananwake na makundi mengine kiuchumi kuwa ni pamoja na kuwekeza katika elimu bora kwa wasichana hasa wa maeneo ya vijijini, kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF).

Dkt. Nchemba kuwa Serikali inatoa msaada wa kisheria bure kupitia kampeni kama Mama Samia Legal Aid Campaign ambayo hadi Februari 2025 ilikuwa imetoa msaada wa kisheria kwa wanawake 681,326.

“Tunatoa mafunzo ya elimu ya kifedha na ya kidijitali kwa wanawake na vijana kupitia huduma za uendelezaji wa biashara, tunatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu na kukuza bajeti jumuishi kijinsia na kuhakikisha uchambuzi wa kijinsia unajumuishwa katika upangaji na utekelezaji wa bajeti ya umma” alisema Dkt. Nchemba.

Alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna vikwazo vya kimfumo vinavyozuia wanawake kufikia uwezo wao kamili wa kiuchumi na kubainisha kuwa mchakato wa FfD4 ni fursa muhimu ya kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali za kifedha, sera jumuishi, na ushirikiano wa kibunifu unaoipa kipaumbele usawa wa kijinsia, kwa ajili ya kasi zaidi ya maendeleo.

“Tanzania inaipongeza UN Women kwa kuandaa nyaraka ya rasilimali (resource paper) inayotoa mwongozo wa kisera wa kifedha kwa mtazamo wa kijinsia. ambayo ni nyenzo muhimu  itakayosaidia kuhakikisha kuwa uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake unakuwa kiini cha majadiliano na matokeo ya FfD4”. Aliongeza Dkt. Nchemba

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera, Programu, Divisheni ya ushirikiano wa Kimataifa wa UN Women, Bi. Sarah Hendriks, alisema kuwa suala la kuwawezesha wanawake kiuchumi linapaswa kuwa agenda ya kudumu ya mataifa mbalimbali hususan ya kiafrika ili kujenga jamii yenye nguvu ya kiuchumi kupitia uwekezaji wa mitaji, elimu, biashara na kuwawezesha kufikia masoko kwa njia ya kidigiti.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban na uliwashirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali
Posted by MROKI On Wednesday, April 30, 2025 No comments
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko amesema dhamira ya Serikali ni kutekeleza mradi mkubwa wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) kutokana na faida zake kiuchumi ila kwa sasa kuna maeneo ambayo Serikali inayafanyia kazi kwa kina kupitia majadiliano na Wawekezaji ili mradi husika uwe na tija kwa nchi na wananchi.

Ameyasema hayo tarehe 29 Aprili 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge kuhusu Hotuba ya Bajeti ya  Wizara ya Nishati ya shilingi Trilioni 2.2 kwa mwaka 2025/2026 kabla ya kupitishwa kwa kishindo na Bunge hilo kwa asilimia 100.

“ Mradi wa LNG umeanza kusemwa kwa muda mrefu na kila mmoja angetamani mradi huu ukamilike jana lakini lazima tukubaliane kuwa lazima tujadiliane kwa kina na wawekezaji ili kupata kilicho bora na kuleta tija, ninachotaka kuwahakikishia ni kuwa timu ya majadiliano ya Serikali na Wawekezaji wanaendelea na majadiliano na tunatarajia kuwa ndani ya mwaka huu 2025 kama tutakuwa tumemaliza masuala matatu yaliyosalia kujadiliwa, mkataba huo utasainiwa ili mradi uanze mara moja.” Amesema Dkt.Biteko

Ameongeza kuwa, Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ana kiu ya kuona mradi huo  unaanza na alishatoa maagizo kwa Wizara ya kuhakikisha kuwa mradi unaanza kutekelezwa.

Akijibu hoja kuhusu vituo vya mafuta vinavyoongezeka na kujengwa kwa kukaribiana, Dkt.Biteko amesema kuwa Wizara ya Nishati imeanza mazungumzo na Wizara ya Ardhi ili kuongeza umbali kati ya kituo kimoja na kingine kutoka mita 200 za sasa kwa lengo la kuleta usalama wa watu, mazingira na shughuli za kijamii.

Kuhusu msamaha wa kodi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa gesi inayotumika kwenye vyombo vya moto kama vile magari (CNG), Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali ilishatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa vifaa na mashine mbalimbali zinazotumika katika mnyororo wa thamani kwa miradi ya CNG kama vile mitungi ya CNG pamoja na vifaa vya kuwezesha kufunga mfumo kuwezesha magari kutumia gesi hiyo.

Ameongeza kuwa, katika mwaka 2024/2025 Wizara ya Nishati imewasilisha Wizara ya Fedha mapendekezo ya maboresho ya kodi katika gesi asilia inayotumika kwenye magari ili kuzidi kuhamasisha matumizi ya CNG na wawekezaji wanaowekeza kwenye miradi hiyo wapate faida na kurudisha gharama wanazowekeza kwa haraka.

Akijibu  hoja za Wabunge kuhusu gharama za kuunganisha umeme vijijini na mijini, Dkt.Biteko amesema kuwa imeundwa timu kwa ajili ya kuangalia namna gani gharama hizo zitapunguzwa lengo likiwa ni kuleta unafuu kwa wananchi.

Kuhusu usambazaji wa umeme Vijijini, Dkt.Biteko amesema kuwa, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anapaswa kupongezwa kwa kufikisha umeme katika Vijiji vyote 12,318 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 huku kazi ya kupeleka umeme vitongojini ikiendelea kwa kasi.

Akizungumzia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika wilaya zote nchini kupitia mradi wa gridi imara, Dkt. Biteko amesema kuwa tayari Serikali imeshanunua viwanja kwa ajili kujenga vituo hivyo na katika awamu ya kwanza vitajengwa vituo 14 huku utekelezaji ukiendelea na katika laini za umeme ambazo ni ndefu sana Serikali itaweka switching stations.

Aidha, kuhusu suala la kukatika kwa umeme nchini, Dkt.Biteko amesema kuwa  limepungua kwa asilimia 48 huku dakika za kukatika umeme zikipungua kwa asilimia 64 na kwa sasa umeme ukikatika ni kwa sababu tu ya matengenezo ya miundombinu. Hata hivyo amesema Serikali inaendelea kuimarisha kituo cha huduma kwa  Wateja TANESCO ili taarifa ziwafikie wananchi kwa wakati pale umeme unapokatika ikiwemo kila wilaya kuwa na kundi sogozi.
Awali, wakati wa kuhitimisha Hotuba hiyo ya Wizara ya Nishati, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alimpongeza Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya katika Taifa hususan kwenye Sekta ya Nishati akieleza kuwa moja ya misingi ya ukuaji wa kiuchumi na maendeleo katika Taifa lolote ni uwekezaji katika Sekta ya Nishati.

Akizungumzia mikoa ambayo bado haijaunganishwa katika gridi ya Taifa ya umeme, Kapinga alisema kuwa kuna miradi mbalimbali inayoendelea ambapo katika Mkoa wa Rukwa kuna mradi mkubwa wa kusafirisha umeme unaoendelea wa kutoka Iringa-Tunduma hadi Rukwa na kipande kingine cha mradi kitakachounganisha gridi ya Tanzania na Zambia.

“Mhe.Spika  katika Mkoa wa Mtwara na Lindi tayari mkandarasi yupo eneo la kazi, mradi umeanza kwa kujenga njia ya umeme kutokea Songea-Tunduru-Masasi hadi Mahumbika na tumeshaanza kulipa fidia katika eneo la Tunduru hadi Masasi takriban shilingi bilioni 4.6 na eneo lililobakia la Songea kuelekea Namtumbo na Tunduru tutaendelea kulipa fidia ya takriban shilingi bilioni 2.7.” Alisema Kapinga

Kuhusu kupeleka gridi ya Taifa katika Mkoa wa Kagera alisema kuwa kazi inaendelea kupitia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya Benaco-Kyaka na katika Mkoa wa Katavi mradi wa kupeleka umeme wa gridi mkoani humo uko katika hatua za mwisho.

Akizungumzia kazi ya kupeleka umeme kwenye visiwa mbalimbali nchini, Kapinga alisema kuwa, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 9.89 ili kupeleka mifumo ya umeme jua katika visiwa 118 ambavyo vipo katika mikoa zaidi ya mitano hususan Wilaya ya Ukerewe.

Kuhusu maboresho miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Kapinga alieleza kuwa kuna kazi zinaendelea kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika ikiwemo uboreshaji wa kituo cha Mbagala ambacho kilikuwa na transfoma yenye uwezo wa MVA 50 lakini sasa inawekwa transfoma mpya yenye uwezo wa MVA 120 ili kukiongezea uwezo kituo hicho ili wananchi wa Mbagala, Temeke, Yombo, Mkuranga na baadhi ya maeneo ya Kigamboni waendelee kupata umeme wa uhakika.

Alieleza kuwa kazi hiyo imefikia mwishoni na muda wowote transfoma hiyo itaanza kufanya kazi. Kwa eneo la Kigamboni amesema maboresho pia yanaendelea kufanyika na kwamba wananchi tayari wameshaanza kuona mabadiliko ya upatikanaji umeme kupitia maboresho hayo.


Wabunge mbalimbali na mawaziri wakimpongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati , Dkt Doto Biteko kwa kuhitimisha Bajrti ya Wizara yake. 


Wabunge mbalimbali na mawaziri wakimpongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati , Dkt Doto Biteko kwa kuhitimisha Bajrti ya Wizara yake. 
Posted by MROKI On Wednesday, April 30, 2025 No comments

April 29, 2025

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka, uteuzi huo ni kama ifuatavyo:-
 
Arch Dkt. Fatma Kassim Mohamed ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) kwa kipindi cha pili;
 
Balozi Dkt. Jilly Elibariki Maleko ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).  Balozi Maleko anachukua nafasi ya Balozi Begum Karim Taj ambaye amemaliza muda wake;  
 
Prof. Eliakimu Mnkondo Zahabu ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (National Carbon Monitoring Center – NCMC); na
 
Bw. Lucas Abrahamani Mwino ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).  Bw. Mwino anachukua nafasi ya Dkt. John Kedi Mduma ambaye amemaliza muda wake.
Balozi Dkt. Jilly Elibariki Malek
Posted by MROKI On Tuesday, April 29, 2025 No comments
Na Mwandishi Wetu, JAB.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua kadhaa katika kuimarisha na kuboresha sekta ya habari nchini ikiwa ni pamoja na kuunda Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.

Waziri Mkuu amesema hayo leo tarehe 29 Aprili, 2025 wakati akifunga Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari lililofanyika jijini Arusha kwa siku mbili.
“Kwenye sekta ya habari na utangazaji, falsafa ya “4Rs” za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, alizozibainisha baada ya kuingia madarakani mwezi Machi 2021, imetekelezwa kwa vitendo hususani kwenye eneo la “Reforms” (Mageuzi),” amesema Waziri Mkuu na kuongeza;

“Serikali ya Awamu ya Sita katika kutekeleza falsafa hii imechukuwa hatua mbalimbali kuimarisha sekta ya habari na utangazaji nchini kwa kuunda chombo kipya cha kushughulikia usajili wa taaluma ya waandishi wa habari yaani Bodi ya Ithibati”.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari iliyozinduliwa mwaka huu ina jukumu la kusimamia viwango vya kitaaluma kwa wanahabari ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa matakwa ya kisheria chini ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.

Amesema hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kuhakikisha inawezesha shirika la Habari la utangazaji kuwepo kisheria pamoja na kuimarisha Idara ya Habari Maelezo kwa kununua vitendea kazi vikiwemo Magari na vifaa vya kurushia matangazo mbashara.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inayosema “Uhabarishaji kwenye Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba katika uhuru wa vyombo vya habari” inalenga kujadili athari za teknolojia ya akili mnemba katika uendeshaji wa vyombo vya Habari na uhuru wake.

Amesema Serikali katika kuhakikisha Akili Mnemba (AI) inatumika kwa njia inayowezesha badala ya kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari, imeanzisha mchakato wa kuandaa sera maalum ya AI na waandishi wanaowajibu wa kuchangia ili kupata sera nzuri.

“Sera hii itatoa mwongozo wa matumizi ya AI katika vyombo vya habari, ili kuhakikisha kwamba teknolojia mpya zinaendana na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari, uwazi, na uadilifu wa uandishi wa Habari, hivyo mtumie muda wenu hapa kujadili na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sera hiyo,” amesema Waziri Mkuu.
Posted by MROKI On Tuesday, April 29, 2025 No comments



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 29 Aprili, 2025.
Posted by MROKI On Tuesday, April 29, 2025 No comments

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameeleza kuwa wananchi wa Kata ya Ifumbo Wilayani Chunya watapewa leseni 2 kati ya 14 za uchimbaji madini zinazomilikiwa na Kampuni ya G & I  katika bonde la Mto Zira na kutambulika rasmi kama wachimbaji halali ili wafanye shughuli za uchimbaji bila usumbufu ikiwa ni hatua ya utatuzi wa mgogoro baina  ya wananchi hao na mwekezaji.

Alisema hayo jana Aprili 28, 2025 wakati akizungumza katika Mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata na Kijiji cha Ifumbo Wilayani Chunya ambapo aliambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.  Khamis Hamza Chilo.

“Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kushughulikia haya mambo kwa uharaka sana na tuko hapa kwa utekelezaji wa maelekezo yake.” Alisema Waziri Mavunde.

Alisema kuwa baada ya kusitisha shughuli za uchimbaji madini katika bonde hilo mwishoni mwa mwezi Desemba 2024 aliunda Kamati ya Wataalam ya kutathmini athari za mazingira yaliyotokana na shughuli za uchimbaji madini katika mto Zira.

“Kwa kuwa wananchi wa hapa shughuli zenu zinategemea Mto Zira, nimemwelekeza mwekezaji ili aendelee kudumisha ujirani mwema, tumekubaliana katika leseni 14 anazomiliki, atoe leseni 2 kwa ajili ya wananchi wa Ifumbo na Lupa Market ikiwa ni leseni moja kwa kila kijiji, ambako atafanya tathmini ya mazingira kabla hajakabidhi kwa serikali ya kijiji, tathmini hii ni kwa leseni 7 zilizopo Ifumbo kwa kuwa 7 zilizopo Lupa Market zimeshafanyiwa tathmini.” Alisisitiza Mavunde.

Waziri Mavunde aliielekeza Kampuni ya G & I ihakikishe kuwa mazingira yanarejershwa kama yalivyokuwa awali kabla uchimbaji huo haujaanza (restoration); iweke mipaka ya leseni zao zinapoishia; Uchimbaji wa eneo la ifumbo uendelee kusimama mpaka utaratibu wa kimazingira utakapokamilika.

Aidha, Waziri Mavunde alielekeza kuwa, kwa leseni zilizopo Kijiji cha Lupa Market, mwekezaji anaweza kuendelea na uchimbaji kwa kuwa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilishafanya tathmini ya mazingira lakini za Ifumbo zinaendelea kusimama mpaka ukaguzi wa mazingira utakapokamilika baada ya siku 21.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Khamis Hamza Chilo alielekeza kazi ya upandaji miti katika eneo hilo lifanywe haraka sambamba na kuzingatia utaratibu wa kufanya shughuli za kibinadamu umbali wa mita 60 kutoka kwenye ukingo wa mto kwa mujibu wa sheria.

“Nitoe maelekezo kwa NEMC itoe vibali vya ndani ya siku 21 baada ya wahusika kuomba vibali na kukamilsha utaratibu ili kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao kwa tija na bila kubughudhiwa lakini pia Mameja wa NEMC wa Kanda zote kufuatilia tathmini ya mazingira yote ambako shughuli za uchimbaji madini zinafanyika  hapa nchini” alisema Chilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Wilaya Chunya, Mbaraka Batenga, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Chunya Noel Chiwanga na Mbunge wa Jimbo la Lupa Mhe. Masache Kasaka walieleza kuwa wananchi wa Chunya wamenufaika sana na shughuli za madini katika kipindi cha uongozi wako katika sekta na kuwa wananchi wa Ifumbo wakushukuru sana kwa kulipa jambo hili uzito na kulifanya kwa uharaka na hatimaye leo wamepata mrejesho.

Desemba 30, 2024 Waziri Mavunde alitangaza kusitisha shughuli za uchimbaji madini katika bonde la mto Zira na kuahidi kuunda Kamati Maalum itakayofanya tathmini ya uharibifu wa mazingira uliotokana na shughuli za uchimbaji madini na baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi yake ataleta mrejesho.

Matukio katika picha, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Khamis Hamza Chilo wakikagua uharibifu wa mazingira katika Bonde la Mto Zira, katika Kata ya Ifumbo Wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya na kisha kuzungumza na wananchi wa Kata hiyo katika mkutano wa hadhara








Posted by MROKI On Tuesday, April 29, 2025 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo