Raia Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Rais wa Ethiopia Taye Atske Selassie, Rais Mstaafu wa Nigeria Goodluck Jonathan, Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger Ibrahim Mayaki, na Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn katika kongamano la kimataifa kuhusu umwagiliaji na uzalishaji wa kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, lililofanyika siku ya Jumatano mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Raia Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Rais wa Ethiopia Taye Atske Selassie, Rais Mstaafu wa Nigeria Goodluck Jonathan, Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger Ibrahim Mayaki, na Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn katika kongamano la kimataifa kuhusu umwagiliaji na uzalishaji wa kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, lililofanyika siku ya Jumatano mjini Addis Ababa, Ethiopia. **************
Addis Ababa, Februari 13, 2025
- Rais Mstaafu Dkt. Jakaya mrisho Kikwete ameungana na viongozi mbalimbali wa
Afrika katika kongamano la kimataifa kuhusu umwagiliaji na uzalishaji wa kilimo
himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, lililofanyika siku ya Jumatano mjini
Addis Ababa, Ethiopia.
Katika mkutano huo, viongozi
hao walijadili changamoto zinazokumba sekta ya kilimo barani Afrika, ambapo
asilimia 80 ya watu wa bara hili wanategemea kilimo kama chanzo cha kipato na
chakula.
Washiriki wengine wa kongamano
hilo walikuwa Rais wa Ethiopia Taye Atske Selassie, Rais Mstaafu wa Nigeria
Goodluck Jonathan, Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger Ibrahim Mayaki, na Waziri Mkuu
Mstaafu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn.
Katika mjadala ulioongozwa na
Mhe. Hailemariam Desalegn, viongozi hao walibainisha kuwa mabadiliko ya
tabianchi yameathiri sekta ya kilimo, huku ukame, mafuriko, vimbunga, na mvua
zisizotabirika vikisababisha kushuka kwa uzalishaji wa chakula. Hali hii
inazidi kuhatarisha usalama wa chakula barani Afrika.
Kwa upande wake, Dkt. Kikwete
alisisitiza kuwa Afrika inahitaji mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwa kuwekeza
katika Kilimo cha kisasa kinachotegemea umwagiliaji, Mbegu zinazohimili ukame
na mabadiliko ya tabianchi, Mbolea bora na pembejeo za kisasa pamoja na
kuongeza idadi ya mabwana shamba ili kuwasaidia wakulima kuachana na kilimo cha
mazoea.
Kuhusu uzalishaji duni wa
Chakula katika Afrika, Dkt. Kikwete alitaja changamoto nyingine zinazokwamisha
maendeleo ya sekta ya kilimo kama ukosefu wa mikopo kwa wakulima, masoko ya uhakika,
na kiwango kidogo cha usindikaji wa mazao.
Alisisitiza kuwa serikali peke
yake haiwezi kutatua matatizo haya, bali inahitaji kushirikiana na sekta
binafsi ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula unakuwa endelevu.
Akitoa mfano wa mafanikio
nchini Tanzania, Dkt Kikwete alitaja mradi kama wa Ushoroba (corridor) wa
Kukuza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) na Jenga Kesho iliyo Bora kupitia
Kilimo (BBT), ambazo zinalenga kuimarisha sekta ya kilimo nchini.
Akifungua kongamano hilo, Rais
wa Ethiopia Taye Atske Selassie, alieleza jinsi nchi yake ilivyojitegemea kwa
asilimia 100 katika uzalishaji wa ngano kutokana na mipango madhubuti ya kilimo
cha umwagiliaji.
Alisisitiza kuwa ushirikiano
kati ya nchi za Afrika ni muhimu ili kubadilishana uzoefu wa kuboresha
uzalishaji wa chakula.
Katika kipindi hiki ambapo
mataifa yaliyoendelea yamepunguza misaada yao kwa Afrika, viongozi hao
walikubaliana kuwa Afrika haina budi kuwekeza katika teknolojia za kilimo na miradi
ya uzalishaji wa chakula kwa njia endelevu.
Na kwa kutambua umuhimu wa
mijadala kama hii, kongamano hili linatarajiwa kufanyika kila mwaka ili
kuimarisha mshikamano wa Afrika katika kupambana na changamoto za tabianchi na
usalama wa chakula.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh_p8nnoeFe-sRviz5aNRNYZ_E2fWlSOOZ8CI2fKm73mDVHFue1aoniJ_TxjJd127bJJpO8km-n6zo-qIy1Rl0jYZi3XNNLD1ETAGzy8iiA4irQPc-3ou2vQkzsy9b-UIWAadAHbGDnZCsnjjgo1LzjGdpwQgLLRPhvWVqLL82znO1B30YeUpGxFrjRAs0/w640-h556/ad1.jpeg)
Raia Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akishiriki katika kongamano la kimataifa kuhusu umwagiliaji na uzalishaji wa kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, lililofanyika siku ya Jumatano mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Posted by MROKI
On Thursday, February 13, 2025
No comments
0 comments:
Post a Comment