Nafasi Ya Matangazo

January 25, 2025

Na Mwandishi wetu, Dar Es Salaam.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion na promota wa kwanza wa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Goodluck Gozbert, Bw. Alex Msama, amemtaka mwimbaji huyo kuomba radhi kwa Nabii Mkuu Geordevie kufuatia kitendo cha kuchoma gari aliyopewa na mtumishi huyo wa Mungu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Bw. Msama alisema kuwa kitendo hicho ni cha kusikitisha na kinaonyesha ukosefu wa busara. Alieleza kuwa hatua ya Goodluck kuchoma gari hiyo kwa madai ya kuona "mauzauza" na kushuka kiuimbaji, haikuwa sahihi hata kidogo.

"Kama alikuwa halihitaji gari hiyo, angechukua hatua ya kumrudishia mtumishi wa Mungu badala ya kulichoma moto. Kitendo hicho si cha kiimani na kinaonyesha kuwa halijui neno la Mungu," alisema Msama.

Aidha, Bw. Msama alieleza kuwa kuna waimbaji wengi ambao wamewahi kupewa magari na hawajawahi kulalamika au kuchukua hatua za ajabu kama hiyo. Alisisitiza kuwa kuchoma gari ni ishara ya kushuka kiimani na kutokuelewa thamani ya baraka zinazotolewa na watumishi wa Mungu.

"Badala ya kuomba msaada wa maombi kwa matatizo anayodai kuyaona, alichukua uamuzi wa ajabu ambao hauwezi kufafanuliwa kiimani. Giza hukimbia nuru, na sio nuru kukimbia giza. Asimsingizie mtumishi wa Mungu wala kutumia hatua hiyo kuchafua watumishi wa Mungu," aliongeza.

Msama alihitimisha kwa kumtaka Goodluck Gozbert kuonyesha unyenyekevu na kuomba msamaha kwa Nabii Geordevie kutokana na kitendo hicho kibaya ambacho si tu kinaumiza imani ya watu bali pia kinatoa taswira mbaya kwa wasanii wa Injili.

Habari hii ni ya kipekee na inaangazia umuhimu wa maadili na busara kwa watu maarufu, hususan wale wa tasnia ya Injili.
Posted by MROKI On Saturday, January 25, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo