Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Methew Nhonge amesema kikao kazi cha viongozi na watendaji wa sekta ya ardhi alichokiitisha Waziri wa Ardhi Mhe. Deogratius Ndejembi kimewarudisha watumishi wa sekta hiyo katika misingi ya utumishi na maadili ya utendaji kazi kwenye sekta ya Ardhi.
Kamishna Mathew amesema hayo Novemba 12, 2024 mara baada ya kukamilika kwa kikao kazi cha viongozi na watendaji wa sekta ya ardhi kutoka mikoa yote nchini kilichofanyika jijini Dodoma.
"Maudhui makuu ya kikao hiki ilikuwa ni Mhe.Waziri kuwasikiliza watendaji wa sekta ya ardhi, ametueleza tunatakiwa tufanye nini kama watumishi wa Umma"amesema Kamishna Mathew.
"Kikubwa ilikuwa ni kuturudisha kwenye maadili ya utendaji na utumishi wa Umma kama watumishi wa sekta ya ardhi," ameongeza Kamishna Mathew.
Kwa mujibu wa Kamishna huyo wa ardhi nchini, wao kama watumishi wa sekta ya ardhi wanatambua wanachangamoto nyingi ambazo watumishi wanalalamikiwa,lakini ilikuwa ni muhimu kuwarudisha watumishi kwenye utendaji kazi wenye tija kuwahudumia watanzania maeneo mbalimbali nchini.
Hata hivyo, ameongeza kuwa kikao hicho kimekuwa na mafanikio makubwa kutokana na namna watumishi walivyoshiriki na hatimaye kutoka na maazimio yanayoenda kuboresha utendaji kazi ikiwemo kutoa Hati Miliki za Ardhi kwa wananchi waliokamilisha taratibu za umilikishaji ndani ya siku saba.
Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Lindi Bw. Geofrey Martin amesema kuwa, ushiriki wao katika kikao hicho umechochea ari ya utendaji kazi wenye tija kwa viongozi na watendaji wa wizara na taasisi zake huku akielezea baadhi ya fursa zinazopatikana kwenye mkoa wake.
"Kwa mfano sasa hivi kuna mradi wa upimaji viwanja eneo la mto mkavu ambao ni mradi mkubwa wa kimkakati wa Serikali sambamba na ule NLG ambao ni mradi mkubwa wa uchimbaji gesi na Wizara ya Ardhi imetoa zaidi ya fedha Bilioni 1.5"amesema Bw. Martin
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam Mwendwa Mgulambwa amesema wamejifunza mambo mengi katika kikao kazi hicho na watayafanyia kazi katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imehitimisha Kikao Kazi cha viongozi na watendaji wa sekta ya ardhi kutoka mikoa yote nchini amabcho kilichofanyika kwa siku mbili kuanzia Novemba 11 na 12 mwaka huu jijini Dodoma.
0 comments:
Post a Comment