Nafasi Ya Matangazo

October 22, 2024

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) unaendelea na jitihada zake za kupunguza umaskini kwa kaya zilizo chini ya kipato, ambazo baada ya kufanyiwa utafiti, zimeonekana kuwa zinahitaji msaada. Kupitia miradi mbalimbali, TASAF inalenga kusaidia kaya hizo kuondokana na hali ya umasikini kwa kuzihawilisha fedha kama chachu ya maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 22, 2024, katika Viwanja vya Nzovwe, Mbeya, Afisa Habari wa TASAF, Melekizedeki Nduye, alielezea kuwa moja ya jukumu kubwa la TASAF ni kutoa elimu kwa walengwa kuhusu mbinu za kuondokana na umaskini. Tukio hilo lilifanyika katika Wiki ya Huduma za Kifedha, inayobeba kauli mbiu "Elimu ya Fedha ni Msingi wa Maendeleo kwa Jamii Yoyote."

Nduye alieleza kuwa taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya kifedha zinashiriki katika maonyesho hayo, lengo likiwa ni kushirikiana katika kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi. "Kazi yetu kubwa ni kuwaelimisha walengwa namna ya kuondokana na umaskini. Tunawafundisha kwamba kufanya kazi kwa kushirikiana ndani ya vikundi ni njia ya haraka zaidi ya kujiinua kiuchumi, kuliko kufanya kazi peke yako," alisema.

Akiongeza zaidi, Nduye alifafanua kuwa kupitia vikundi, walengwa wanaweza kuchangia fedha zao na kuzikopa kwa ajili ya kufanya shughuli za uzalishaji. "Ukiwa na shilingi mbili, unachanganya na ya mwenzako, kisha mnakopa kiasi kikubwa zaidi cha fedha kama vile elfu 50 ili kuwekeza katika shughuli itakayokuza kipato," alieleza.

TASAF inatoa elimu kwa walengwa wake kuhusu sekta mbalimbali kama kilimo, ufugaji, uvuvi, na biashara. Hili linawapa fursa ya kuchagua shughuli wanayopenda kushiriki, kwa kuzingatia hali ya kaya yao. "Walengwa wetu wanapata elimu ya vikundi na kisha wanaamua ni aina gani ya shughuli watafanya, kama ni kilimo, biashara au ufugaji," aliongeza Nduye.

Walengwa wa TASAF ambao wamejiunga kwenye vikundi wamefanikiwa kuzalisha bidhaa mbalimbali, ambazo zinapatikana kwenye maonyesho hayo. Nduye alisema kuwa bidhaa zinazozalishwa ni pamoja na mikeka, sabuni za mwani kutoka Pemba, unga wa mwani, na maziwa freshi. Bidhaa hizi zinauzwa na walengwa wa TASAF, wakionesha matunda ya elimu waliyopata.

"Banda la TASAF limesheheni bidhaa nyingi ambazo zimetengenezwa na walengwa wetu. Tunaonyesha matokeo halisi ya kazi zao, na fedha ambazo wamepewa zimewawezesha kupiga hatua kubwa katika maisha yao," alisisitiza Nduye.

Nduye aliwataka wakazi wa Mbeya kufika kwa wingi kwenye banda la TASAF ili kujionea bidhaa zinazozalishwa na walengwa wenzao, na kuona jinsi wanavyopiga hatua kiuchumi. Pia, alisema kuwa TASAF ipo tayari kupokea malalamiko, kero, na maswali yoyote kutoka kwa wananchi kuhusu shughuli zake.

"Tuko hapa kuonyesha kwamba walengwa wetu wakiuza kwenye maonyesho kama haya, wanapata fursa ya kuonyesha bidhaa zao na kupata masoko. Wananchi wanakaribishwa kuuliza maswali na kupata majibu sahihi kuhusu TASAF," alihitimisha Nduye.

Posted by MROKI On Tuesday, October 22, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo