Nafasi Ya Matangazo

September 27, 2024




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa maendeleo washirikiane kikamilifu na nchi zinazoendelea katika kusaidia utekelezaji wa mifumo jumuishi ya kifedha.
 
Ametoa wito huo jana (Septemba 25, 2024) wakati akifungua mjadala kuhusu  miaka 15 ya  mafanikio katika masuala ya Mfumo Jumuishi wa Fedha kwa Maendeleo kwenye mkutano ulioitishwa na Malkia wa Uholanzi, Mhe. Maxima ambaye ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Huduma Jumuishi za Fedha, Jijini New York, Marekani
 
Amesema kuwa uchumi jumuishi ni muhimu hasa katika utekelezaji wa mpango endelevu wa maendeleo na ufanikishaji wa ajenda 2030.  “Huduma jumuishi za kifedha ni kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi, kupunguza umasikini na kuleta maendeleo ya jamii kwa ujumla.”
 
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amempongeza Malkia Maxima kwa juhudi zake ambazo zimewezesha ongezeko kubwa la ufikiaji wa huduma za kifedha duniani, huku zaidi ya asilimia 50 ya watu wakiwa wamefikiwa na mpango huo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
 
“Umiliki wa akaunti duniani umeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 76 kwa mwaka 2021. Haya ni mafanikio makubwa, changamoto imebaki hasa kwa wanawake waishio katika nchi zinazoendelea ambapo wengi wao bado hawajaingizwa kwenye mfumo jumuishi wa kifedha.”
 
Mapema, Malkia Maxima wa Uholanzi alisema anafurahishwa na hatua iliyofikiwa sasa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa hapo awali.
 
"Wakati tunaanza hii kazi ya kuhimiza mifumo jumuishi ya kifedha hatukuwa na takwimu zozote. Tulipanda na kufikia asilimia 50 na sasa tunakaribia asilimia 80. Natambua asilimia 80 siyo sawa na asilimia 100, ni lazima nikiri kuwa kazi imefanyika," alisema.
 
Akionesha dhahiri kuwa bado kazi haijaisha, Malkia Maxima alisema mkakati uliopo ni kuwafikia watu bilioni 1.5 ambao bado hawajafikiwa na huduma jumuishi za kifedha.
 
Alisema anafarijika kuona watunwa rika mbalimbali wakitumia mifumo hii kwenye maeneo ambayo huduma za kifedha zinapatikana. "Mabibi wanaweka fedha na kusomesha wajukuu zao, vijana na mabinti wajasiriamali wanatumia huduma hizo kutunza fedha zao, kupata mikopo midogo midogo na kukuza mitaji yao," alisema.
Posted by MROKI On Friday, September 27, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo