Tanzania na Visiwa vya Comoro zimesaini Hati nne za Makubaliano kwenye kilele cha Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Comoro uliofanyika tarehe 24 Julai,2024 jijini Dar es Salaam.
Hati zilizosainiwa katika kikao hicho zinazojumuisha nyanja za; Ushirikiano wa Kidiplomasia, Afya, Biashara na Viwanda na Teknolojia ya Habari. Utiaji saini hati hizo umeshuhudiwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro anayeshughulikia Nchi za Kiarabu, Nchi zinazozungumza Kifaransa, Diaspora na Mtangamano wa Afrika Mhe. Mohamed Mbae.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa kihistoria, Waziri Tax ameelezea umuhimu wa kusainiwa kwa hati hizo kuwa itawezesha pande hizo mbili kuwa na ushirikiano ulio katika mpangilio mzuri katika nyanja husika na hivyo kuleta tija zaidi.
"Pamoja na kutia saini Hati za Makubaliano pia tumekubaliana kuendelea kushirikiana katika maeneo mengine mengi ikiwemo miondombinu, nishati, ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, utalii, utamaduni, sanaa na michezo na Maendeleo ya vijana". Ameeleza Dkt. Tax
Naye Mhe. Mbae ameeleza kufurahishwa kwake na kufanyika kwa mkutano huo wa JPC na kuongeza kuwa mkutano huo ni kiungo muhimu katika kuendelea kukuza na kuimarisha uhusiano na kati ya Tanzania na Comoro.
Ameipongeza Tanzania kwa kuandaa mkutano huo na hivyo kuonesha dhamira ya dhati ya Tanzania katika kuendelea kushirikiana na Comoro.
Mbali na kusainiwa kwa Hati hizo Mawaziri hao wameridhishwa na kupongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa makubaliano na maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa kwa pamoja kati ya pande hizo mbili tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Jumla wa Ushirikinao mwaka 2009.
Vilevile mkutano huo umejadili na kuweka mikakati ya namna ya kuendelea kukuza biashara baina ya pande hizo mbili. Mikakati hiyo pamoja na mambo mengine italenga kuwahimiza sekta binafsi kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili na kuchangamkia fursa za kibiashara zilizopo na zile zinazotokana na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na Eneo Huria la Biashara la SADC.
Akizungumzi kuhusu mkutano huo Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu ameeleza kuwa, Comoro ni mshirika muhimu wa Tanzania katika biashara, ambapo kwa mwaka 2023 Tanzania iliuza nchini humo bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 148.
Ameongeza kusema kuwa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo sio tu yataongeza ushirikiano wa kidiplomasia bali yanatarajiwa kuongeza kiasi cha bidhaa ambazo Tanzania inaingiza nchini humo.
Katika mkutano huo ujumbe wa Tanzania umejumuisha wataalamu na watendaji kutoka sekta mbalimbali na umeongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax, ambaye pia aliongoza mkutano huo kwa kushirikiana na mwenyekiti mwenza Waziri Mbae wa Comoro.
0 comments:
Post a Comment