Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Mhe. Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu amesema Watanzania wanapaswa kuendelea kuunga mkono juhudi za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuchangamkia fursa mbalimbali za nishati ambazo zinazotolewa ikiwemo fursa ya mkopo nafuu wa uwezeshaji wa ujenzi wa uendeshaji wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta (Petroli na Dizeli) vijijini.
Mhe. Balozi Kingu ameongeza kuwa duniani kote Sekta ya Nishati ni kichocheo cha ukuaji wa Sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo Sekta ya Viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kuwa uzalishaji wa malighafi unategemea na upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na inayopatikana kwa wakati wote.
“Natoa wito kwa Watanzania wote, kuendelea kuchangamkia fursa kama mikopo ya ujenzi na uendelezaji wa vituo vidogo vya mafuta vijijini lakini pia na fursa nyingine ikiwepo ya upatikanaji wa umeme vijijini na hasa kwenye maeneo ambayo hawajajiunga na huduma ya umeme licha ya kuwa umeme umefika”. Amesema Balozi Kingu.
“Natumia nafasi hii, kuipongea Menejimenti ya REA kwa kuendelea kutekeleza maelekezo ya Bodi ipasavyo, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muunguno wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu Sekta ya Nishati vijijini tunayatekeleza na kuyasimamia ipasavyo”. Amekaririwa Balozi Kingu.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia Balozi Kingu amesema REA imeanza kutekeleza kwa vitendo matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Tumesaini makubaliano ya kushirikiana na Jeshi la Magereza, tumeanza na Taasisi hii kwa sababu inatumia mkaa na kuni kwa kiasi kikubwa kama chanzo cha nishati na kwa kuwa inahudumia zaidi ya Watu 100, ndani ya kipindi cha miaka miwili, tarajieni mabadiliko makubwa kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia”. Amalizia Balozi Mstaafu, Jacob Kingu.
0 comments:
Post a Comment