Nafasi Ya Matangazo

June 25, 2024








Eleuteri Mangi, Mwanza
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) inalenga kuongeza usalama wa milki za Ardhi ili kuongeza usajili wa umiliki wa ardhi kwa wanawake na wanaume nchini.

Akifungua mafunzo kwa wataalamu wa Ardhi wanaosimamia mradi wa LTIP katika halmashauri mbalimbali nchini kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza Bw. Saidi Mtanda jijini Mwanza Juni 25, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi amesema mahitaji ya ardhi yanahitajika sasa kuliko wakati wowote ili kujenga nyumba za watu kuishi, shughuli za kiuchumi, kijamii na uwekezaji kwa tija kwa kuwa na mipango ya ardhi yenye uhalisia. Mafunzo hayo yanahusu uandaaji na usimamizi wa mipango ya ardhi vijijini.
“Tuijenge nchi yetu kwa pamoja, kama wataalamu tuendelee kufanya maboresho katika Sekta yetu ya Ardhi na kuleta mabadiliko ya kitaalamu na kiutendaji katika mradi wa uboreshaji wa usalama wa milki ili hatimaye ardhi yote ipangwe, ipimwe na kumilikishwa kwa wananchi”.

“Mliopata fursa ya kushiriki moja kwa moja katika utekelezaji wa mradi huu na sasa kushiriki mafunzo; muishauri vizuri serikali kwa uaminifu na uadilifu wa hali ya juu na kwa kuzingatia uzalendo, Taifa kwanza” ameongeza Makilagi.
Makilagi amesema kuwa Serikali imelenga kuongeza usalama wa milki za Ardhi nchini kwa wanawake na wanaume kwa kuongeza usajili wa umiliki wa ardhi na kuimarisha usalama wa milki za Ardhi kwa kutoa Hati miliki za kimila 500,000, Leseni ya makazi 1,000,000 na Hati milki 1,000,000 katika halmashauri 67.

Akitoa taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Bw. George Pangawe amesema mwaka 2022 Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliingia mkataba na Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

Mradi huo unathamani ya Sh. Bilioni 346 sawa na Dola za Kimarekani milioni 150 na unatekelezwa kwa miaka mitano kuanzia 2022/2023 hadi 2026/2027 katika halmashauri 67 nchini ili kuimarisha usimamizi na utawala wa ardhi na kuimarisha usalama wa milki za ardhi kwa kupima, kusimamia na kumilikishwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Kwa kuzingatia Tanzania ina rasilimali za mifugo, wanyamapori, misitu, vyanzo vya maji na vivutio vingi vya utalii, zinaathiwa na ongezeko la idadi ya watu ambalo linaenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii. 

Wataalam hao wanawajibu wa kutumia maarifa waliyoyapata kuaandaa mipango ya matumizi ya ardhi yenye uhalisia na inayokubalika kwa wanachi wote na itakayokidhi mahitaji ya nchi ili kuendana na kasi ya ukuaji wa miji na vitovu vya vijiji vinayobadilika kuwa miji.
Posted by MROKI On Tuesday, June 25, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo