Nafasi Ya Matangazo

May 24, 2024

 
Mkuu wa Wilaya Siha, Kilimanjaro Mhe. Dkt. Christopher Timbuka, leo tarehe 23 Juni, 2024 amezindua rasmi msimu wa nne wa tamasha la West Kili Tour Challenge na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kujiandikisha ili waweze kushiriki tamasha hilo litakalofanyika tarehe 22-23 Juni, 2024.
Tamasha la West Kili Tour Challenge 2024 litakalofanyika ndani ya Shamba la Miti la West Kilimanjaro, linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania -TFS.
Akizindua tamasha hilo katika viwanja vya Shamba la Miti West Kilimanjaro, Dkt. Timbuka amesema tamasha hili ni fursa ya kujionea vivutio vya asili na kujifunza umuhimu wa uhifadhi wa misitu.

"West Kili Forest Tour Challenge inalenga kukuza utalii endelevu, kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, na kuleta pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali ili kujifunza na kushirikiana kwa manufaa ya jamii na mazingira yetu. Aidha inachangia miradi na maendeleo ya jamii na ni fursa kwa wafanyabiashara na wawekezaji" Dkt. Timbuka

Dkt. Timbuka aliwaongoza Wadau na Waandishi wa Habari kukagua njia za Msituni zitakazotumika wakati wa mashindano.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo, Meneja wa Uhusiano Johary Kachwamba amesema TFS imepata mafanikio katika utalii ikolojia ikiwa ni pamoja na shughuli za matamasha kama la West Kili.

"Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika uhifadhi na utalii, na sasa mapato yameongezeka maradufu, mfano mwaka 2021 kwenye Utalii Ikolojia TFS tulipata laki 6 lakini hadi kufikia mwaka 2023 tulifanikiwa kukusanya bilioni 1.5,"
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la West Kilimanjaro, PCO Robert Faida amesema, West Kili Forest Tour Challenge ni hafla ya kila mwaka inayowakutanisha wapanda milima, wapenzi wa mazingira, na wadau mbalimbali kutoka sehemu tofauti za dunia kushiriki katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, utalii wa ndani, kufanya mtoko wa nyika, kufanya matembezi hifadhini, kukimbia msituni, kuendesha baiskeli, pikipiki pamoja na maonyesho ya magari na kufurahia uzuri wa misitu ya West Kilimanjaro.

Akielezea tukio la mwaka huu alisema kutakuwa na Matembezi, riadha na Utalii amnapo Washiriki wataweza kuchagua matembezi/mbio katika umbali tofauti (21.1km, 10.2km, 5km) wakifurahia mandhari nzuri ya msitu wa West Kilimanjaro.

Aidha, alisema kutakuwa na michezo kama vile mbio za baiskeli, moto cross, maonyesho ya mavazi ya asili, na sanaa za mazingira bila kusahau michezo ya Watoto na burudani mbalimbali.

Akielezea jinsi ya kushiriki alisema kuna njia mbili za kujisajili ambazo ni ya mtandao (westkili.co.tz) na kulipa kwa lipa namba (Tigo 7878284 jina west kili run and bike, lipa kwa Mpesa 5362338 jina pedal Tz)

Aliongeza kuwa washiriki wanaweza kupata maelezo zaidi juu ya jinsi ya kujiunga kwa kupiga namba 0783823609 au 0767970071.

Anasema ili kushiriki mtu atatakiwa kulipa ada ya ushiriki ambapo Watanzania watalipa TZS 35,000 kwa wanaoshiriki kwenye riadha na michezo ya baiskeli huku wasio Watanzania kwenye raidha na baiskeli wakitakiwa kulipa USD 35.

Aliongeza kuwa michezo ya pikipiki italipiwa TZS 30,000 kwa bodaboda na TZS 65,000 kwa wabobezi (Pro riders).

“Ada hizi zinajumuisha kiingilio hifadhini, kupata medali na t-shirt pamoja na matunda, maji na soda. Nisitize washiriki kulipa ada kupitia njia zilizotajwa kwenye tovuti,” alisema mhifadhi Robert Faida.
"West Kili Forest Tour Challenge inalenga kukuza utalii endelevu, kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, na kuleta pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali ili kujifunza na kushirikiana kwa manufaa ya jamii na mazingira yetu. Aidha inachangia miradi na maendeleo ya jamii na ni fursa kwa wafanyabiashara na wawekezaji" Dkt. Timbuka.
Posted by MROKI On Friday, May 24, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo