Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa Wanawake wanapata fursa na haki sawa katika nyanja zote za kijamii.
Hayo yamebainishwa leo Machi 8, 2028 na Mhe. Kassima Majaliwa aliyewakilishwa na Mhe. Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya jamii jinsia, Wanawake na makundi maalumu kwenye viwanja vya shule ya Msingi Chinangali 11 Wilaya ya Chamwino wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya Wanawake Duniani kwa Mkoa wa Dodoma.
"Katika kudhihirisha hili, Serikali imeendelea kuwezesha Wanawake kupitia Mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo, jumla ya Shilingi Bilioni 743.7 zimetolewa na kunufaisha watanzania 6,064,957, wakiwemo Wanawake 3,288,186 sawa na asilimia 54 na wanaume 3,556,359 sawa na asilimia 46.
"Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa mikopo ili kuwawezesha Wanawake kupata mitaji ya biashara. Hii ni pamoja na kuimarisha mikopo isiyokua na riba ya asilimia 10 inayotolewa kwa makundi maalumu kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa." Amesema Mhe. Majaliwa
Akitoa salamu za Mkoa kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule amesema Dodoma unafanya maadhimisho haya kila mwaka kwani mwaka 2023, yalifanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa ambapo Wanawake zaidi ya 10,000 waliweza kushiriki.
Aidha, ameongeza kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo mengi kwenye Mkoa wa Dodoma kwani Serikali ya Mkoa Ina viongozi Wanawake kwenye kila nyanja kwa asilimia kubwa. Hii inawapa shime Wanawake kugombea ngazi mbalimbali za uongozi Serikalini.
Sanjari na hayo, uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Jinsia na maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023 umefanyika.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani (SWD) yalianza mwaka 1911 kufuatia maandamano ya Wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani kupinga mazingira duni ya kazi kama vile ukosefu wa huduma za kijamii na uwepo wa vitendo vya unyanyasaji katika ajira.
Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine ilianza kuadhimisha siku hii mwaka 1997. Mwaka 2005, maadhimisho yameendelea kufanyika kila mwaka kwa ngazi ya Mkoa na yale Kitaifa hufanyika kila baada ya miaka mitano (5). Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kauli mbiu inayosema "Wekeza kwa wanawake: Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na ustawi wa Jamii".
0 comments:
Post a Comment