Nafasi Ya Matangazo

February 12, 2024

 






Watoa huduma ndani ya mabasi ya abiria yanayokwenda masafa marefu nchini, wanapatiwa mafunzo ya siku 5 ngazi ya Kanda ya kati yaliyoandaliwa na Chuo cha usafirishaji nchini (NIT) kwa udhamini wa Benki ya Dunia. Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi leo Februari 12, 2024 kwenye ukumbi wa Chuo kikuu cha Mipango kilichopo Jijini Dodoma na yanatarajiwa kuhitimishwa Februari 16, 2024.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ambaye ndiye mgeni rasmi wa hafla hiyo, ametoa Wito kwa wahudumu hao kutumia fursa hii kuleta mabadiliko kwenye sekta ya huduma ya usafirishaji.

"Serikali imeweka mkazo kwenye sekta ya usafirishaji kwa kujenga Barabara nyingi na zenye ubora. Rais ameimarisha kila Idara ya usafirishaji. Kuna uhusiano mkubwa kati ya usafirishaji na utoaji huduma na kundi hili mara nyingi halijatolewa mafunzo.

"Nitoe shime kuimarisha huduma kwa mteja kupewe kipaumbele na uzito unaostahiki. Wahudumu muwe na mawasiliano fasaha na lugha nzuri kwa wateja wenu. Tuna wajibu wa kulinda Mali na usalama wa abiria wetu hivyo, hakikisheni munatoa nzuri ili Serikali ione Fahari kwa juhudi zilizofanyika" Amesema Mhe. Senyamule.

Awali akielezea lengo la kufanya mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Usafirishaji Salama na uhandisi wa mazingira NIT Bw. Patric Msigwa, amesema mafunzo haya yamefuatia kulega lega kwa utoaji huduma kwa abiria wa mabasi kutoka kwa baadhi ya wahudumu.

"Mafunzo haya, yanayotolewa kwa ngazi ya Kanda ambapo kwa hapa Dodoma ni Kanda ya kati inayojumuisha Mikoa ya Dodoma, Tabora na Singida. Mafunzo yatawasaidia kuboresha utoaji huduma pamoja na ufanisi kwani hapa tuna watoa huduma 70 ambao wanashiriki kupata mafunzo haya na hii itasaidia kuboresha huduma kwani baadhi ya watoa huduma hawana mafunzo sahihi" Amesema Bw. Msigwa.

Hata hivyo, Afisa Mfawidhi kutoka Mamlaka ya Uthibiti wa usafiri Ardhini, LATRA Bw. Ezekiel Emmanuel, amesema Mamlaka yake iliingia makubalino na NIT kutoa mafunzo haya ambayo yataleta Mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji. Pia ametoa wito kwa wasafirishaji wa abiria kuhudhuria mafunzo haya kwa maslahi ya kukuza na kuleta tija kwenye biashara zao.
Posted by MROKI On Monday, February 12, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo