Nafasi Ya Matangazo

January 30, 2024

Askofu mwijage (katikati) mwenye fimbo akiwa na baadhi ya maaskofu waliohudhuria ibada hiyo
Askofu Mwijage akikabidhiwa fimbo na Kardinali Rugambwa wa Jimbo Kuu la Tabora katika ibada hiyo.
Msemo wa kihaya usemeo “Tikiliwa Igamba”ambalo tafsiri yake ni “tukio ambalo litabaki simulizi” ulidhihirika wakati wa tukio kubwa la kihistoria la kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Jovitus Francis Mwijage, wa jimbo la Katoliki la Bukoba, lililofanyika mjini Bukoba mkoani Kagera.

Mikimiki na shamrashamra za maandalizi ya tukio hilo kubwa la kihistoria katika jimbo la Bukoba ilianzia kwenye ngazi za familia za wakristo, Vigango, Parokia mpaka jimboni ambako ilihitimishwa na misa takatifu iliyofanyika katika uwanja wa Kaitaba ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Naibu Waziri Mkuu wa Waziri wa Nishati, Mh. Doto Biteko, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh.Samia Suluhu Hassan.

Misa hiyo iliyoongozwa na Kardinali Protace Rugambwa, Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Tabora akisaidiana na aliyekuwa Msimamizi wa Kitume jimbo la Bukoba, Askofu Methodius Kilaini na Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo la Kayanga, ilihudhuriwa na maaskofu kutoka majimbo mbalimbali nchini, viongozi wa Serikali mkoani Kagera wakiongozwa na Mkuu wa mkoa Fatma Mwassa ,watawa wa kiume na kike, viongozi wa maadhehebu mbalimbali , maelfu ya waumini kutoka parokia mbalimbali za jimbo Katoliki la Bukoba na majimbo jirani waliojawa na bashasha na furaha ya kumpata Askofu mpya.
Kwaya mbalimbali zikitumbuiza wakati wa kumkaribisha Askofu Mwijage katika makazi yake yaliyopo Ntungamo Bukoba.

Pia ibada hiyo ilihudhuriwa na Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania, Askofu Mkuu Angelo Acattino.

Vikundi mbalimbali vya kwaya kuanzia za watu wazima mpaka za watoto zilizoimba katika ibada hiyo zingine kwenye maandamano kwenye sehemu za barabara alizopita Askofu Mwijage kutoka Rwamishenye hadi kanisa kuu la jimbo zilileta shamrashamra ya pekee katika mji wa Bukoba na vitongozi vyake bila kusahau wananchi wengi waliojipanga misururu barabarani kumshangilia bila kujali mvua iliyokuwa inanyesha katika maeneo mbalimbali mjini humo.

Pia kulikuwepo na tukio la mkesha wa ibada ya Masifu ya jioni iliyoongozwa na Askofu Flavian Kassala, wa Jimbo Katoliki la Geita, ambayo ulihudhuriwa na waumini wengi wakiwa wanasubiri tukio hili muhimu la kihistoria kwa shauku kubwa.
Askofu Mwijage akikaribishwa katika makazi yake yaliyopo Ntungamo Bukoba.
Askofu Mwijage akikaribishwa katika makazi yake yaliyopo Ntungamo Bukoba.

Akiwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh.Samia Suluhu Hassan, katika ibada hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mh.Doto Biteko, alisema Serikali itampa ushirikiano Askofu Mwijage na kanisa Katoliki ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Dk.Biteko, alisema Rais Samia amehimiza umuhimu wa kujenga Taifa lenye uhuru na haki kwa kuwa haki ulijenga Taifa na kusisitiza kuwa zipo changamoto zinazotukabili kama Taifa ambazo ili kuziondoa kunahitaji kuwepo na ushirikiano miongoni mwetu licha ya kutofautiana kwa mawazo na mitizamo.

Akizungumzia utendaji wa Akofu Mwijage, Dk. Biteko, alisema waumini wa Katoliki wa Bukoba wamempata kiongozi wa kiroho, Mchumi, mlezi na mbunifu anayetegemewa na wengi kuwafundisha na kuwaelekeza katika njia sahihi za kiroho na kimwili.

Awali akizungumza kabla ya kumweka wakfu, Kardinali Rugambwa, amemkubusha askofu Mwijage, kuzingatia nafasi aliyokabidhiwa kuwa ni mali ya Kristo hivyo aishi kwa wito kutekeleza utume wake kwa kumsikiliza Kristo.

“Wapende pia watawa wa kiume na wa kike ukiwaamini na kukuza mchango muhimu katika utume hapa Bukoba, wapende waamini na walei ukiwaalika na ukiwahamasisha kushiriki kikamilifu katika maisha, utume wa kanisa ili jimbo la Bukoba lipate sura ya kisinodi ya kutembea pamoja, ”alisema.

Akiongea katika ibada hiyo, Askofu Mwijage ambaye amechukua nafasi ya Askofu Desderius Rwoma aliyestaafu mwaka 2022 ,aliahidi kushirikiana na mapadri kuendeleza pale alipoacha mtangulizi wake “Kwa mapadri, watawa wa kike na wa kiume wote nawaita kuendeleza jimbo letu,watanguzi wetu walifanya kazi nzuri iliyotukuka ninawaomba tuunganishe vipaji vyetu kuendeleza jimbo kiroho na kiuchumi”,alisisisitiza.

Tukio hilo la kihistoria katika kanisa kwenye jimbo Katoliki la Bukoba liliambatana na habari ya kustaafu kwa aliyekuwa Msimamizi wa Kitume jimbo la Bukoba, Askofu Methodius Kilaini ambaye amelitumikia kanisa kwenye nafasi mbalimbali kwa uadilifu mkubwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50.
Kwaya mbalimbali zikitumbuiza wakati wa kumkaribisha Askofu Mwijage katika makazi yake yaliyopo Ntungamo Bukoba.
Askofu Mwijage akikaribishwa katika makazi yake yaliyopo Ntungamo Bukoba.

Askofu Mwijage alizaliwa Bukoba, Desemba 2, 1966, baada ya masomo ya kipadre, Julai 20, 1997 alipewa daraja takatifu la la upadre.

Amefanya kazi katika parokia mbalimbali katika jimbo la Bukoba ikiwemo kuwa mwalimu na mlezi katika seminari ndogo ya Rubya.

Kuanzia mwaka 2005 hadi 2011 alitumwa na jimbo la Bukoba kwa ajili ya kujiendeleza kwa masomo ya juu na hivyo kupata shahada ya uzamivu kwenye historia ya kanisa mwaka 2011.

Kati ya mwaka 2011-2012 alikuwa jaalimu wa historia ya Kanisa Seminari Kuu ya Segerea. Mwaka 2012 hadi 2023 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, Tanzania.

Kuanzia mwaka 2012 hasi uteuzi wake Oktoba 19 mwaka jana,alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja waMapadre Wazalendo Tanzania (UMAWATA) na kuanzia mwaka 2020 ni Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Uchumi ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS.
Posted by MROKI On Tuesday, January 30, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo