TAARIFA YA MKURUGENZI MTENDAJI WA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) DKT. PETER KISENGE KATIKA MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI ULIOFANYIKA KWENYE UKUMBI WA IDARA YA HABARI - MAELEZO, DAR ES SALAAM TAREHE 18 JULAI 2023.
Ndugu Watumishi wa Umma,
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana,
NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA……
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha kuifikia siku hii ya leo tukiwa wazima wenye afya njema. Aidha, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philipo Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Ally Mwalimu, Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu kwa kuiwezesha Taasisi yetu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Nawashukuru Wafanyakazi wote wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kujitoa kwao kuwahudumia wananchi wenye matatizo ya moyo. Pia nipende kuwashukuru Waandishi wa Habari kwa kufanya kazi na Taasisi yetu bega kwa bega ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi za magonjwa ya moyo pamoja na huduma tunazozitoa.
Ndugu Waandishi wa Habari, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni hospitali maalumu inayotoa tiba ya magonjwa ya moyo, mafunzo na utafiti. Katika kutekeleza majukumu yake Taasisi imeendelea kuzingatia sera, mipango na mikakati yenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa ya moyo hapa nchini.
Taasisi yetu inafanya yafuatayo:
a) Wagonjwa wanaotibiwa kwa siku ni 500.
b) Wagonjwa wanaolazwa kwa wiki ni 130.
c) Wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua, upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu kwa siku ni sita.
d) Kupitia mitambo ya Cathlab (Catheterization Laboratory) wagonjwa wanaochunguzwa, kuzibuliwa mishipa ya damu ya moyo na kuwekewa vifaa visaidizi vya moyo kwa siku ni 14.
Ndugu Waandishi wa Habari, kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2022/23 Taasisi yetu ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 44.5 fedha ambazo zilitumika kufanya shughuli mbalimbali za utoaji wa huduma ya matibabu ya moyo pamoja na shughuli za maendeleo. Katika mwaka huo wa fedha Taasisi ilifanikiwa kufanya yafuatayo:
a) Tuliona wagonjwa 122,362 kati ya hawa watu wazima walikuwa 111,542 na watoto 10,820 wagonjwa waliolazwa walikuwa 4407 watu wazima 3286 na watoto 1121.
b) Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua na kubadilishwa Valvu za moyo moja hadi tatu, upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery –CABG), upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu walikuwa 714 kati ya hao watu wazima walikuwa 412 na watoto 305. Watoto tuliowafanyia upasuaji walikuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake na matatizo ya Valvu.
c) Kupitia mitambo ya Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba ya magonjwa ya moyo inayotumia mionzi maalumu wagonjwa 2046 kati yao watu wazima 1762 na watoto 284 walipata huduma za matibabu. Wagonjwa hawa walipata huduma za uchunguzi, matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo, matibabu ya mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa imeziba na kuwekewa vifaa visaidizi vya moyo.Uchunguzi huu pamoja na tiba unafanyika kwa njia ya upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja.
d) Gharama ya matibabu ya wagonjwa hawa 2,760 tuliowafanyia upasuaji mkubwa na mdogo wa moyo kama wangetibiwa nje ya nchi ni shilingi 62,340,000,000 lakini kwa kutibiwa kwao katika Taasisi yetu matibabu yao yamegharimu kiasi cha shilingi 31,170,000,000 fedha ambazo zimelipwa na bima za afya, ndugu wa wagonjwa, wafadhili na wengine kupata msamaha wa matibabu. Kwa wagonjwa hawa kutibiwa hapa nchini Serikali imeweza kuokoa kiasi cha shilingi 31,170,000,000 fedha ambazo zingelipwa kama wagonjwa hawa wangetibiwa nje ya nchi.
e) Kwa kipindi cha mwaka mmoja wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi yetu kutoka nje ya nchi walikuwa 301. Wagonjwa hawa walitoka katika nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Uganda,Zambia,Visiwa vya Comoro, Ethiopia, Burundi na wengine kutoka nje ya Afrika zikiwemo nchi za Armenia, China, India, Norway, Marekani na Uingereza.
f) Taasisi ilitumia shilingi bilioni 1,249,521,800 kwaajili ya kununua mashine mbalimbali zikiwemo za utasishaji wa vifaa vya Hospitali, Digital X-Ray na mashine tatu za kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography).
g) Tarehe 20/4/2023 Taasisi yetu ilisaini makubaliano ya miaka miwili na Hospitali za Taifa za nchini Rwanda na Zambia ya kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hizo. Pia tumesaini makubaliano ya kushirikiana katika utoaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa, kubadilishana ujuzi wa kazi, kufanya tafiti mbalimbali na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu na chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland, chuo cha madaktari wa upasuaji Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (COSESCA) nchi ya Malawi, Visiwa vya Comoro, Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
h) Kupitia kozi ya miezi sita ya mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na wa dharura inayotolewa kwa wauguzi kati ya wanafunzi 50 waliomaliza sita walitoka katika nchi za Rwanda na Zambia.
i) Katika kutoa huduma za tiba mkoba zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan Outreach Services tulifanya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo. Huduma hii imetolewa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Pwani, Arusha, Geita, Iringa, Mtwara, Lindi, Unguja, Manyara na Pemba. Wananchi 6309 walifikiwa na huduma hii kati ya hao 3239 walikutwa na matatizo ya moyo na waliopewa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI walikuwa 724.
j) Mwezi Mei mwaka huu wataalamu wetu walikwenda nchini Malawi katika Hospitali ya Queen Elizabeth kutoa huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo, huduma hii ilitolewa kwa watu 724. Waliokutwa na matatizo ya moyo walikuwa 537 kati yao 201 walipewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu.
k) Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma iliajiri wafanyakazi wapya 64 wa kada mbalimbali na wafanyakazi 98 walipandishwa vyeo katika madaraja tofauti. Wafanyakazi 50 walilipiwa ada za masomo katika kozi mbalimbali walizozifanya.
l) Tarehe 14 Novemba mwaka jana Serikali ilitupatia Hospitali ya Dar Group iliyopo wilayani Temeke kuwa sehemu ya JKCI. Kwa kutupatia hospitali hii kumetatua changamoto ya nafasi ambayo tulikuwa tunakabiliana nayo kwa muda mrefu na kutatusaidia kuboresha huduma za matibabu tunazozitoa kwa wananchi.
m) Tumechapisha matokeo ya tafiti za kisayansi (Publication) 12 katika majarida ya kimataifa (International scientific journals).
Ndugu Waandishi wa Habari, Kwa mwaka wa fedha 2023/24 Taasisi imetenga bajeti ya kiasi cha Shilingi Bilioni 66.3 fedha hizi zitatumika kwaajili ya utekelezaji wa kazi mbalimbali zilizoainishwa kwenye Mpango Kazi na Bajeti ya Mwaka 2023/24.
Taasisi itatumia fedha hizi kulipa mishahara ya wafanyakazi, uendeshaji wa gharama za Taasisi, manunuzi ya vifaa tiba na dawa, kusomesha wataalamu wetu kozi za muda mrefu na muda mfupi pia zitatumika kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo la vipimo vya uchunguzi wa magonjwa pamoja na ofisi za utawala, ujenzi wa jengo la kutolea huduma za matibabu kwa watoto katika Hospitali yetu ya Dar Group na ununuzi wa vifaa kazi.
Mchanganuo wa maeneo ambayo yamepewa kipaumbele katika bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 ni pamoja na yafuatayo:-
a) Kuimarisha tiba za moyo kwa kudhamini masomo ya muda mfupi na mrefu kwa wafanyakazi, kununua vifaa tiba vya kisasa zaidi, kuendeleza ujenzi mbalimbali, kutoa huduma za tiba mkoba kwa kuwafuata wananchi walipo.
b) Kuendelea kutoa elimu ya magonjwa ya moyo pamoja na lishe bora kwa wananchi kupitia luninga, magazeti na mitandao ya kijamii.
Ndugu Waandishi wa Habari, manufaa ambayo wananchi watayapata kupitia vipaumbele vya Taasisi kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni pamoja na:
a) Kuzidi kuimarika kwa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwani wataalamu wanazidi kuongeza ujuzi walionao kupitia kozi za muda mrefu na mfupi wanazosoma pia kununuliwa kwa vifaa tiba vya kisasa kutasaidia kutolewa kwa huduma bora kwa wananchi.
b) Kukamilika kwa jengo la utawala na vipimo ambalo limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.6 kutasaidia wagonjwa wengi zaidi kupata huduma za vipimo vya moyo kwa wakati pia wafanyakazi watakuwa na ofisi za kutosha na hivyo kupunguza msongamano katika ofisi walizopo.
c) Taasisi itaendelea kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo (Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan Outreach Services) kwa kufanya hivyo wenye matatizo ya moyo watapata huduma za matibabu mapema tofauti na ambavyo wangezifuata huduma hizo Dar es Salaam. Tunafanya hivi kwa kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa tunaowatibu mioyo yao huwa imechoka hii ni kutokana na kuchelewa kufika JKCI kwaajili ya kupata matibabu ya kibingwa ya magonjwa haya.
d) Kupitia vyombo vya habari Taasisi itaendelea kutoa elimu ya jinsi ya kuyaepuka magonjwa ya moyo kwa wananchi kwani magonjwa haya ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na mtu anaweza kuyaepuka akifuata mtindo bora wa maisha. Pia tutaendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya dawa za moyo pamoja na umuhimu wa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kwa wagonjwa wa moyo.
Ndugu Waandishi wa Habari, ninaomba nimalizie taarifa yangu kwa kuwakumbusha wananchi mambo yafuatayo:
a) Unaweza kuepuka kupata magonjwa ya moyo kwa kufanya mazoezi.
b) Kuzingatia lishe bora kwa kula matunda, mboga mboga, vyakula vyenye madini ya potassium vile vile kupunguza kula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta na chumvi.
c) Kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri, kutambua kiwango cha sukari katika mwili wako, kutambua msukumo wako wa damu na kiwango cha mafuta mwilini.
d) Kupima afya ya moyo japo mara moja kwa mwaka kunaweza kukakusaidia kujua kama una tatizo hili au la na kama unatatizo utaweza kupata matibabu mapema.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
“Afya ya Moyo Wako ni Jukumu Letu”.
0 comments:
Post a Comment