Nafasi Ya Matangazo

April 25, 2023



Na Mwandishi Wetu, Morogoro
IDADI ya majeruhi katika mchezo wa riadha kwenye michezo ya Kombe la Mei Mosi imepungua kutoka 20 na kuwa tisa kwa mwaka 2023, imeelezwa.

Dkt. Msimamizi wa michezo ya Mei Mosi inayofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoa Morogoro, Nassoro Matuzya amesema kuwa wachezaji walioshiriki mbio za mita 100, 200, 400, 800, 1,500, 3,000 na kupokezana vijiti mita 100x4 wamepata majeraha machache hususan ya kushikwa na misuli na kushindwa kuendelea na mbio.

Amesema sababu za majeruhi hao ni kutokuwa na mazoezi ya mara kwa mara na kutokunywa maji ya kutosha, ambayo yanasaidia kuboresha afya baada na kabla ya mazoezi mbalimbali.

“Tunashukuru sana michezo ya mwaka huu hasa upande wa riadha ambayo wengi wa wachezaji wanapata majeraha sio makubwa kwa mwaka huu tumepata majeruhi wachache, tofauti na mwaka jana tulipata majeruhi wengi na wengine walikuwa wamezidiwa zaidi na kukimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi,” amesema Dkt. Matuzya.

Dkt. Matuzya amewashukuru taasisi na wizara zilizoleta madaktari ambao wanasaidia kutoa huduma kwenye michezo mbalimbali, endapo wachezaji wataumia.

Hatahivyo, ametoa ushauri kwa washiriki wote kuanzia viongozi na wachezaji wanaoshiriki michezo hii na mingine kuhakikisha wanafanya mazoezi kwa bidii na kunywa maji kwa wingi.

Pia amewataka waajiri kuhakikisha watumishi wake wanashiriki michezo mahali pa kazi ili kujiimarisha afya ya mwili na akili, ambapo inasaidia kuongeza ufanisi wa kazi.
Posted by MROKI On Tuesday, April 25, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo