Nafasi Ya Matangazo

March 05, 2023

Uongozi wa Shirika la Reli nchini Tanzania (TRC) umepongeza maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) walipotembelea mradi huo siku ya Jumamosi, tarehe 04 Machi 2023. 

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Mitambo wa TRC Mha. Heriel Makange Emanuel aliyeambatana na mameneja wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme (SGR).

Akieleza umuhimu wa mradi wa JNHPP kwa Shirika la Reli, Mha. Makange alisema kuwa kukamilika kwa mradi wa bwawa la Julius Nyerere ambao unaenda sambamba na ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR kutasaidia sana kuendesha mitambo itakayotumika kwenye mradi wa SGR na hivyo kuridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa JNHPP.

"Mradi huu ni mradi mkubwa sana unaotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita kupitia TANESCO na hivyo tuna imani kubwa kukamilika kwake kutasaidia sana katika shughuli za uendeshaji mashine katika mradi wetu wa SGR na kukamilika kwa miradi hii kutaleta manufaa makubwa kwa taifa letu", ameeleza Mha. Makange. 

Akifafanua kuhusu maendeleo ya mradi, Mhandisi Mkazi wa mradi wa JNHPP, Mha. Lutengano Mwandambo ameeleza kuwa maendeleo ya kazi za mradi zinaenda vizuri na kuwa hadi kufikia mwezi Februari 2023, mradi umefikia asilimia 83.3% za ujenzi wake. 

Pia, ameongeza kuwa ujazaji maji ndani ya bwawa la Julius Nyerere umefikia mita 135 kutoka usawa wa bahari kutoka mita 71.5 wakati bwawa lilipoanza kujazwa maji mnamo tarehe 22 Disemba, 2022. 

"Tunashukuru maendeleo ya mradi yanaenda vizuri mpaka kufikia mwishoni mwa Februari 2023, mradi ulikuwa umefika asilimia 83.3%. Pia ujazaji maji unaendelea vizuri na kwa sasa tumefika mita 135 kutoka usawa wa bahari kutoka mita 71.5 tulipoanza kujaza maji mnamo tarehe 22 Disemba, 2022", alifafanua Mha. Mwandambo. 
Akielezea faida za mradi huu, Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa wadau TANESCO, Elihuruma Ngowi ameeleza faida za kukamilika kwa mradi huu ikiwemo kuwa na umeme wa uhakika, kilimo, utalii, uvuvi, miundombinu na usafirishaji pamoja na huduma ya maji safi na salama ambazo zote kwa pamoja zitawanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla wake.





Matukio mbalimbali ya viongozi wa TRC wakiwa katika ziara ya kutembelea mradi wa JNHPP.


Posted by MROKI On Sunday, March 05, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo