Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Maharage Chande akiongea na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) kuhusu maboresho ya kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 220 kwa kilovoti 33 cha Tagamenda Iringa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipotembelea kituo hicho, siku ya Jumanne, 14 Machi 2023.Mha. Timothy Mgaya, Meneja Miradi vituo vya kupoza umeme kwa miradi ya Zambia, Tanzania na Kenya (ZTK) akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa kituo cha umeme mkubwa wa kilovoti 400 cha Tagamenda Iringa kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) walipotembelea mradi huo siku ya Jumanne, 14 Machi 2023. Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Japhet Hasunga (Mbunge) akiongea na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) katika kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 220 kwa kilovoti 33 cha Tagamenda Iringa wakati Kamati hiyo ilipokitembelea kituo hicho siku ya Jumanne, 14 Machi 2023.
*********
Na Mwandishi wetu - Iringa
Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mhe.
Japhet Hasunga (Mbunge) siku ya Jumanne, tarehe 14 Machi 2023 ilifanya ziara ya
kukagua mradi wa upanuzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme
mkubwa cha Tagamenda Iringa ujulikanao kama “Backbone Transmission Investment
Project (BTIP)” awamu ya pili na kujionea namna mradi huo utakavyotekelezwa.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Japhet Hasunga (Mbunge)
amesema Kamati yake imefanya ziara hiyo ili kuona na kutaka kujiridhisha juu ya
kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa “BTIP” ambao unahusisha kuviongezea uwezo
vituo vya kupokea na kupoza umeme mkubwa katika mikoa ya Iringa, Singida,
Dodoma na Shinyanga kutoka umeme mkubwa wa Kilovoti 220 kwenda umeme mkubwa wa
kilovoti 400.
“Leo hii
tumekuja kama Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa ajili ya
kutembelea huu mradi ambao unajulikana kama mradi wa “Backbone” lengo hasa la Kamati
ni kutaka kujiridhisha ni lini mradi huu utaanza kujengwa na kukamilika. Sasa
tumekuja kujionea kwamba mradi ulishaanza kutekelezwa na nguzo zilishasimikwa
na vyuma vimeshasimikwa kila mahali na vimekamilika na tayari sasa wanaanza
kujenga ile substation kubwa ambayo itapokea kilovoti 400 kwa hiyo tulikuwa
tunajiridhisha ni sehemu gani umeme wa kilovoti 400 itajengwa na tumeshajionea
na tumeona lakini pia nyuma yetu tumeona kwamba kuna umeme ambao ni kilovolti
220 ambao tayari umeshakamilika” alisema Mhe. Hasunga.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Maharage Chande amesema
mradi wa “Backbone Transmission Investment Project (BTIP)” umekamilika kwa
awamu ya kwanza iliyohusu ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti
400 kutoka Iringa hadi Shinyanga yenye urefu wa Kilomita mia sita na sabini
(670km) na upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoza umeme mkubwa wa kilovoti 220
kwenye mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga ambapo mpaka sasa kituo
kinapokea umeme kutoka katika mabwawa ya Kidatu, Kihansi na Mtera.
“Mradi huu
umekamilika kwa awamu ya kwanza kwa maana ya kituo cha kilovoti 220 na kinapokea
sasa umeme kutoka katika vituo vya kuzalisha umeme kwa maji vya Mtera, Kidatu,
na Kihansi. Kituo hiki kina manufaa makubwa ya kuwezesha nchi yetu kuwa na
umeme wa uhakika na wenye ubora kwani kituo hiki kikikamilika kitaweza kupeleka
umeme kwenye zaidi ya mikoa 18 ambayo sasa hivi inapata umeme kutoka kwenye
kituo hiki” alisem Bw. Chande
Bw. Chande
aliongeza kuwa mradi huu wa upanuzi utakapokamilika utawezesha kupeleka umeme
katika nchi zilizopo Kusini mwa bara la Afrika (SADC) ambapo kwa sasa kuna
fursa kubwa ya kuuza umeme.
“Lakini
vilevile kituo hiki ni kitovu cha kupeleka umeme katika nchi za “Southern
African Power Pool (SAPP)” kupitia nchi ya Zambia ambapo kwa sasa hivi kuna
fursa kubwa sana za kuuza umeme kwa sababu umeme kwa upande huo umepungua
lakini pia kuunganisha nchi za upande wa Mashariki “Eastern African Power Pool
(EAPP)” kupitia nchi za Kenya, Uganda na Ethiopia. Kwa hiyo awamu ya pili ya upanuzi
wa kituo hiki ambapo sasa kitapelekwa kwenye kilovoti 400 kitawezesha kupeleka
umeme katika nchi za Kusini mwa bara la Afrika (SADC)” alifafanua Bw. Chande.
Bw. Chande
aliendelea kufafanua kuwa mradi huu unategemewa kuanza kutekelezwa hivi
karibuni.
“Mradi huu unategemewa
kuanza kutekelezwa hivi karibuni kwani tupo katika hatua za manunuzi ambapo
tunategemea mpaka mwezi wa nne au wa tano zitakuwa zimeshamilika na kuanza
kupata mkandarasi wa kuanza kujenga kituo hiki cha upanuzi na njia kuu za
kupeleka katika kituo kinachofuata cha Kisada,
na Iganjo, ili umeme uweze kusafiri na kuweza kufika ,” alihitimisha Bw. Chande.
Mradi huu wa “Backbone
Transmission Investment Project (BTIP)” awamu ya pili unahusisha kukiongezea
uwezo kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa cha Tagamenda -Iringa kwa kusimika
mashine umba (transfoma) mbili zenye uwezo wa MVA 250 kila moja. Hapo awali,
utekelezaji wa mradi huu ulikuwa sehemu ya mradi wa “backbone” awamu ya pili na
ulikuwa ufadhiliwe na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (The European Investment Bank
- EIB) kwa dola za marekani milioni 60 lakini kwa sasa mradi huu unatekelezwa kupitia mradi
wa Tanzania-Zambia (TAZA) kwa ufadhili
wa Benki ya Dunia.
0 comments:
Post a Comment