KAMATI ya Amani na Jumuiya ya
Maridhiano Tanzania imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka
miwili madarakani na kusema katika kipindi hicho kwa kiasi kikubwa ameifungua
Tanzania katika mambo mbalimbali ikiemo uhusiano wa kimataifa, Demokrasia na
ukuaji wa Uchumi kupitia ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Akizungumza Dar es Salaam,
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sheikh Alhad Mussa Salumu amesema kwa aliyoyafnya
katika kipindi hicho cha miaka miwili kinapaswa kupongezwa na watanzania wote
kwani kimeiletea Tanzania matunda kiasi cha kumfanya kila mtu kijivunia uwepo
wake huku akiamini kuwa katika kipindi cha uongozi wake kinachoendelea atazidi
kufanya mambo makubwa Zaidi.
Kuhusu kuifungua nchi
Kidemokrasia, Sheikh Alhad amesema tofauti na huko nyuma kwa sasa wanasiasa
wote wana furaha baada ya uwepo wa
maridhiano ya kisiasa na kuwafanya kuwa na amani na kuondoa uoga uliokuwepo wa kufanya siasa zao
katika maeneo mbalimbali ya nchi kama watanzania.
“Kwa hilo hana mpinzani, sote
tumeshuhudia Mheshimiwa Rais amefungua
eneo la siasa na kuifanya Demokrasia kwamba sasa imekuwa pana huu ni ukomavu wa
kisiasa, hata alipoudhuria mkutano wa Bawacha alipangua hoja baada ya hoja ya
Mbowe na kuwasisitiza kila mmoja kushiriki kuijenga nchi, hizi ndizo habari
ambazo kila mtanzania anapenda kuisikia” amesema Sheikh Alhad
Amesema katika suala zima la
haki, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kiasi kikubwa amewezesha kuwaonyesha
watanzania ukomavu wa kisiasa ikiwemo kurahisisha utatuzi wa kesi mbalimbali
zikiwemo za wanasiasa na watu wengine waliokuwepo katika vifungo magerezani
jambo ambalo limewafanya watanzania wengi kufurahia na kurudi kuijenga nchi
yao.
Kuhusu ushirikiano wa Tanzania
kimataifa amesema ndani ya miaka miwili imeshuhudiwa Tanzania ikitembelewa na viongozi
wa kimataifa na idadi kubwa ya watalii ambao wengi wao wamevutiwa na filamu ya
‘Royal Tour’ ambayo yeye mwenyewe Rais Samia Suluhu Hassan ameshiriki kuicheza
jambo ambalo kiongozi huyo amesema kuwa halijawahi kufanywa na viongozi wengine
waliopita katika Taifa hili.
Mbali na hayo kiongozi huyo wa
juu wa Kamati ya Amani na Jumuiya ya Maridhiano amesema katika kipindi cha
miaka miwili cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania imeshuhudiwa
ikiwa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo Reli ya kisasa (SGR),
Barabara, Bwawa la kufua Umeme la Nyerere, Madaraja, Shule, Hospitali na
miundombinu mingine.
Aidha amewataka watanzania
wote wakiwemo wanasiasa kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha Rais Samia ili
kumuwezesha kutimiza malengo yake ya
kulijenga Taifa na kuwaletea maendeleo watanzania katika kipindi chote
atakaloliongoza Taifa hili na kwamba kwa kufanya hivyo kutaiwezesha Tanzania
kupiga hatua zaidi za kimaendeleo.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na Jumuiya ya Maridhiano Tanzania Mchungaji
Geogre Fupe amesema uongozi wa miaka miwili wa Rais Samia Suluhu Hassan
madarakani umegusa nyanja zote zinazopaswa kuwa kama msingi kwa Taifa lolote
ikiwemo uwepo wa demokrasia imara, maendeleo ya ukuaji wa uchumi pamoja na uhusiano
wa kimataifa.
Amesema katika kipindi hicho
cha miaka miwili, Rais Samia Suluhu Hassan ameweza kuyasimamia hayo yote na
kuifanya Tanzania kama nchi kufungua mipaka yake tofauti na ilivyokuwa hapo
nyuma na hivyo kuwavutia watu kutoka mataifa mengine kwa kuiona Tanzania sasa
kama kimbilio lao.
Naye Katibu wa Jumuiya hiyo
Askofu Islael Gabriel Masa, pamoja na mambo mengine pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa
hatua yake ya kusimamia haki ya Mungu kwa kupinga ndoa za jinsia moja na kudai
kuwa kama viongozi wa dini wanamuunga mkono katika hilo na kuahidi kuendelea
kumpa ushirikiano wa kutosha wakati wote anapoliongoza Taifa hili.
March 14, 2023
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment