Nafasi Ya Matangazo

February 17, 2023

Mtandao wa https://earthquaketrack.com umeripoti matukio matatu  ya matetemeko yaliyotokea katika bonde la Ufa na kunakiliwa katika senta ya Ikungi na Kintiku, Mkoani Singida ambayo mtikisiko wake umepita hadi jijini Dodoma. 

Tukio la kwanza kuripotiwa ni la siku ya Alhamisi Februari 16,2023 saa 06:13 jioni ambalo lilikua na ukubwa wa 4.9 na lilitokea kilometa 38 kutoka Ikungi, mkoani Singida. Aidha leo Februari 17, Saa 7:45 asubihi tetemeko lingine lenye ukubwa wa 4.3 na lilitokea umbali wa kilometa 41 kutoka Ikungi. 

Aidha mchana huu majira ya saa 12:26 tetemeko lingine la tatu limepiga kwa sekunde kadhaa likiwa na ukubwa wa 4.9 na lilitokea umbali wa kilometa 29 Kaskazini mwa Kintinku mkoani Singida ambapo lilitikisa jiji la Dodoma na viunga vyake. 

Hakuna madhara yeyote yaliyoripotiwa kutokea kutokana na Matetemeko yote haya na yametokea umbali wa kilometa 10 kutoka ardhini. 

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imethibitisha kuwepo kwa matukio hayo ya matetemeko ya ardhi katika
maeneo ya Wilaya ya Manyoni kwenye mpaka kati ya Mkoa wa Singida na Dodoma yakiwa na ukubwa wa 4.3 na 4.9 katika kipimo cha Richter.

Matukio hayo yalisikika katika maeneo ya mkoa wa Dodoma na Singida. Hata hivyo, pamoja na
matetemeko hayo kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na maeneo ya jirani, GST haijapata taarifa zozote za kutokea kwa madhara kutokana na matetemeko hayo.

Ikumbukwe kwamba mikoa ya Dodoma na Singida imepitiwa na ukanda wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki mkondo wa mashariki. 

Mikoa mingine katika mkondo wa mashariki ni Manyara, Arusha, Mara, Iringa na Njombe ambapo mkondo wa Magharibi una mikoa ya Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma. 

Maeneo ya ukanda wa bonde la ufa kwa kawaida ni maeneo tete ya mabadiliko ya kijiolojia ambayo hukumbwa na matetemeko ya ardhi na milipuko ya volkano.

Matetemeko ya ardhi hutokana na nguvu za asili ambazo husababisha mgandamizo katika matabakaya miamba. Hadi hivi sasa hakujagunduliwa teknolojia ya kuweza kutabiri kutokea kwa tetemeko la ardhi, hivyo GST inatoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari muda wote kama ambavyo imekuwa ikishauri ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na majanga asili ya Jiolojia ikiwemo matetemeko ya ardhi. 

Mojawapo ya hatua za tahadhari dhidi ya tetemeko la ardhi ni kama
zifuatazo:

Kabla ya tukio; kujenga nyumba bora na imara kwa kuzingatia viwango halisi vya ujenzi, kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa kujengwa kulingana na jiolojia ya eneo husika, kuepuka ujenzi wa nyumba katika miinuko yenye kuambatana na mawe/miamba na mipasuko ya miamba.

Wakati wa tukio; kama uko nje ya jengo unashauriwa kubaki nje, simama mahali pa wazi mbali na majengo marefu, miti mirefu, nguzo na nyaya za umeme na ujikinge kichwani kadri inavyowezekana; endapo tetemeko litatokea ukiwa ndani ya nyumba unashauriwa kubaki ndani na ukae sehemu salama kama vile chini ya uvungu wa meza imara, kitanda ama simama kwenye
makutano ya kuta mbali na madirisha, makabati ya vitabu, vyombo au fenicha ili kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo;

Usitangetange muda mrefu kutafuta mahali salama kwa sababu tetemeko la ardhi hutokea ghafla na huchukua muda mfupi sana; jihadhari na moto kwakuwa tetemeko la ardhi linaweza kusababisha matukio ya moto kwa kutokea hitilafu ya umeme au kupasuka kwa mabomba ya gesi; usiendeshe chombo cha moto wakati wa tukio la tetemeko; toa taarifa kwa uongozi wa eneo husika au kwa vyombo vya uokoaji ili kupata msaada zaidi; Baada ya tukio: 

Kagua majengo kwa uangalifu ili kuhakikisha kama hayakupata madhara na kama ikilazimu unashauriwa kuwaita wataalamu wa majengo kufanya ukaguzi kuona kama ni salama majengo hayo kuendelea kutumika.

Posted by MROKI On Friday, February 17, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo