Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiongoza ujumbe wa Tanzania katika
Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika unaofanyika Addis Ababa
tarehe 15 – 16 Februari 2023
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini
Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo wakati wa Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la
Umoja wa Afrika unaofanyika Addis Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana
na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini,
Mhe. Deng Dau Deng Malek katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa
Afrika unaofanyika Addis Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya
Nje wa Ethiopia, Mhe. Demeke Mekonnen akijadili jambo na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax kabla ya kuanza
kwa Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika unaofanyika Addis
Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukiongozwa
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Stergomena Tax katika picha ya pamoja
Mawaziri mbalimbali walioshiriki Mkutano
wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika wakiwa katika picha ya pamoja.
Mkutano huo unaofanyika Addis Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023.
************
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) ameongoza
ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 42 wa Baraza la
Mawaziri la Umoja wa Afrika unaofanyika Addis Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023.
Mkutano huu ni sehemu ya
maandalizi ya Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika
utakaofanyika tarehe 18-19 Februari 2023.
Pamoja na mambo mengine,
mkutano wa Mawaziri utajadili masuala ya kimkakati yanayohusu Bara la Afrika ikiwemo
utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika-AfCFTA, uhakika wa
chakula, hali ya ulinzi na usalama, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na masuala
ya kiutawala na usimamizi wa rasilimali za Umoja wa Afrika.
Akichangia katika mkutano huo,
Dkt. Tax alisisitiza umuhimu wa Kamisheni na Taasisi za Umoja wa Afrika
kusimamia vyema rasilimali za Umoja wa Afrika kwa kuchukua hatua za kuondoa
mapungufu yaliyobainika kwenye taarifa ya ukaguzi wa rasilimali za Umoja wa
Afrika.
Mhe. Waziri pia alieleza hatua ambazo Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inachukua katika kutekeleza Mikataba ya
Uenyeji ya Taasisi za Umoja wa Afrika zilizopo Tanzania ambazo ni Mahakama ya
Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Umoja wa Posta Afrika na Bodi ya Umoja wa
Afrika ya Ushauri dhidi ya Rushwa.
Awali akiwasilisha hotuba yake
ya ufunguzi, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Mhe. Moussa Faki
Mahamat alisisitiza umuhimu wa Umoja wa Afrika kuendelea kutoa kipaumbele
kwenye masuala yanayowagusa wananchi wa Afrika ikiwa ni pamoja na kutatua
changamoto mbalimbali za mabadiliko za kijamii, kiuchumi na kiusalama.
Alisisitiza umuhimu wa Afrika kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje kwa
kuongeza uzalishaji wa bidhaa za vyakula ndani ya bara la Afrika pamoja na
kutumia fursa za mkataba wa AfCFTA katika kukuza Mtangamano wa Kiuchumi.
Bw. Faki aliongeza kuwa Umoja wa Afrika
umeendelea kusimamia masuala ya amani na usalama katika bara la Afrika katika
nchi za Ethiopia, Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Libya
ambapo jitihada zilizofanyika zimelenga zaidi kupata suluhisho la amani kwa
mataifa hayo.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mhe. Demeke Mekonnen amesema Ethiopia ameshukuru
Umoja wa Afrika kwa mchango na ushirikiano wake ambao umewezesha kupatikana
amani na utulivu nchini Ethiopia na kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda wa miaka
miwili.
“Ethiopia inaamini kuwa kupitia Umoja wa Afrika amani, ulinzi na
usalama vitailetea Afrika maendeleo zaidi,” alisema Mhe. Mekonnen.
0 comments:
Post a Comment