Naibu Waziri Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa mwezi mmoja kwa
wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Nayu wilayani Chamwino mkoani
Dodoma kufuata vibali vya kulinda mazingira.
Ametoa agizo hilo leo Agosti
10, 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua mazingira katika eneo
hilo kutokana na wachimbaji hao kudaiwa kufanya shughuli hizo bila taratibu na
kuhatarisha usalama wa mazingira na afya.
Alisema imebainika kuwa kuna
shughuli za uchimbaji na uchenjuaji zinafanyika bila kufuata taratibu zikiwemo
za utiririshaji ovyo wa maji yasiyo salama na kuelekea kwenye vyanzo vya maji
hivyo kuhatarisha afya za wananchi.
Mhe. Khamis alisema kuwa
Serikali inatambua shughuli halali za kujipatia kipato zinazofanywa na vijana
hususan katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu lakini ni lazima
ziendane na sheria za utunzaji wa mazingira.
Amewaelekeza wachimbaji hao
wadogo kufuatilia vibali katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Mamlaka ya Bonde la
Wami-Ruvu ili kupata vibali vya kufanya shughuli hizo.
“Kuna mto unapita hapa lakini
tunaona kuna shughuli za kibinadamu zikiwemo uchenjuaji zinafanyika hapa sasa
kemikali za sumu zinatoka hapa na kusambaa katika maji ya mto hali inayoweza
kuhatarisha afya za wananchi,” alisema Mhe. Khamis.
Pia, naibu waziri aliwataka
wananchi kutunza vyanzo vya maji na kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu
zikiwemo ufugaji na kilimo kwani ndio chanzo kikubwa cha uchafuzi wa maji na
mazingra kwa ujumla.
Sambamba na hilo alihamasisha
zoezi la upandaji na utunzaji wa miti katika maeneo yao kwani ndio chanzo cha
kunyesha kwa mvua na hivyo kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Meneja wa
Kanda ya Kati wa NEMC Dkt. Franklin Rwezamila alisema wachimbaji wadogo wa
dhahabu wanaojihusisha na shughuli za uchenjuaji wana wajibu wa kufuata
taratibu za kimazingira.
Alisema afya ya binadamu ni
muhimu kulindwa na pia mazingira yanayozunguka yanapaswa pia kulindwa hivyo ni
muhimu kutekeleza maelekezo ya wataalamu wa mazingira.
“Wananchi wanategemea maji
kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ili waweze kuyatumia kwa mahitaji yao lakini
wawekezaji nao wanapaswa kufuata taratibu za kimazingira,” alisema.
Naye Meneja Msaidizi
Rasilimali za Misitu Kanda ya Kati Bi. Patricia Manonga alisema pamoja na kuwa
wachimbaji hao kuwa na leseni za uchimbaji lakini wanapaswa kupata kibali cha
matumizi ya eneo hilo.
0 comments:
Post a Comment