Akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano wa siku mbili wa Kamati ya Utatu leo tarehe 11 Julai, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Mhe. Siyani amesema kuwa ni wajibu wa kila upande kuhakikisha kuwa unatimiza wajibu wake kwa mujibu wa matakwa ya kisheria huku wakizingatia umuhimu wa kuhakikisha kuwa kuna amani na utulivu katika maeneo ya kazi.
“Hakikisheni waajiriwa wanapewa mikataba ya kazi na kuongeza tija na uzalishaji utakaowezesha ukuaji wa uchumi, na vilevile mhakikishe mnatatua migogoro na madai yanayohusu stahili au haki za msingi za wafanyakazi kwa kufuata taratibu zilizowekwa,” amesema Jaji Kiongozi
Mhe. Siyani amewasisitiza pia wadau hao wa Kazi kutosahau kuheshimu sheria kwa kufanya kazi kwa umakini na uadilifu na kutokuwa sehemu ya dhuluma ama usumbufu kwa wale wanaowawakilisha.
Kwa upande mwingine, Jaji Kiongozi amewakumbusha Wadau wa Mahakama kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Tanzania ili kutekeleza ipasavyo Dira ya Mahakama ya Tanzania ya ‘Utoaji Haki sawa kwa wote na kwa wakati’.
Mhe. Siyani ameongeza kuwa ili
kufikia dira hiyo, Mahakama inategemea ushiriki wa wadau wote na vilevile nguzo
ya pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/2022-2024/2025) unasema:
Upatikanaji wa haki sawa kwa wote na kwa wakati na kujenga Imani ya wananchi
kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau. Hivyo ni muhimu kuzingatia ili azma ya
Mahakama ya kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati iweze kufikika.
“Naomba niendelee kuwakumbusha wadau wote kuendelea kushirikiana na Mahakama kwa kuhudhuria mahakamani kwa tarehe zilizopangwa na kutokuwa na kikwazo cha uondoshaji wa mashauri mahakamani kwa wakati.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi amesema kuwa, katika Divisheni hiyo mashauri yaliyobaki hadi kufikia Desemba 2021 yalikuwa 1,526, huku mashauri yaliyosajiliwa toka Januari, 2022 hadi Juni mwaka huu ni 726, mashauri yaliyoamriwa kuanzia Januari mpaka Juni mwaka huu yalikuwa 1,391 sawa na asilimia 195 ya mashauri yaliyofunguliwa.
“Mhe. Jaji Kiongozi, kumekuwa na kasi kubwa ya uondoshaji wa mashauri katika Divisheni yetu, na hii ni kutokana na jitihada si tu za Maafisa na Watumishi wa Mahakama bali wadau wote waliopo hapa kwani wametoa ushirikiano na kila mmoja kwa nafasi yake amehakikisha mashauri ya kazi yanamalizika kwa kasi kupisha shughuli za kiuchumi kuendelea, kama ilivyokuwa lengo la uanzishwaji wa Mahakama hii ya kazi pamoja na Taasisi zingine za kazi,” alieleza Mhe. Salma.
Naye, Bw. Maridadi Fanuel,
Mratibu Taifa Sheria za Kazi na Viwango vya Kazi vya Kimataifa kutoka Shirika
la Kazi Duniani (ILO)-Tanzania ameipongeza Divisheni ya kazi kwa kasi nzuri ya
uondoshaji wa mashauri na kusema kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na
Divisheni hiyo kwa kuiwezesha katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutoa Mafunzo
kwa watumishi wake.
“Takwimu zinaonyesha kuwa
utendaji wa Mahakama ya Kazi ni mzuri sana hali hii inatupa moyo sisi ILO wa
kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na Mahakama ya Kazi maana tunaona
ufanisi wa kazi unatekelezeka kiuhalisia,” amesema Bw. Fanuel.
Mkutano huu wa watumiaji wa Kamati ya Utatu hufanyika kila mwaka na unajumuisha sio tu uwakilishi wa utatu yaani ‘TUCTA’, ‘ATE’ na Serikali kupitia Wizara ya Kazi pamoja na Kamishna wa Kazi, Majaji pamoja na wadau wengine wakiwemo ‘CMA’ Mwanasheria Mkuu na Wakili Mkuu wa Serikali, Mawakili wa kujitegemea, wawakilishi binafsi na kadhalika unalenga kujadili mafanikio pamoja na changamoto mbalimbali ili kupata maoni ya pamoja ili kuboresha huduma hususani utatuzi wa migogoro ya kazi.




0 comments:
Post a Comment