Sheha wa Kojani, Hamad Ali Bakari akizungumza wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri waliozuru kisiwa cha Kojani hivi karibuni |
Wanatuambia serikali italeta
nyenzo.
Kojani ni kisiwa cha wavuvi. Hatufanyi shughuli nyingine hapa. Ni uvuvi miaka nenda, miaka rudi. Maisha yetu ni samaki, watoto wanasoma shule na tunajitibu kwa mapato ya samaki. Tunasubiri kuona wataleta nini.
Nasikia kuna vyombo vitakuja. Tutaweza kwenda kwenye bahari kubwa. Tunasubiri, wakati wao ukifika tutaambiwa. Tukipata yote hayo kama ambavyo wanasema, patakuwa na mabadiliko makubwa ya maisha ya hapa.
Hapa kama mlivyoona maisha ni pesa. Ukitaka embe, kama ambazo mmekula kule ng’ambo, ni pesa. Kojani hakuna mashamba, kila kitu kinaletwa, utakila kama una pesa. Kama serikali itatufanya tuondokane na uvuvi huu mdogo itakuwa imetusaidia sana”.
Nukuu hizi ni za Sheha wa Kojani, Hamad Ali Bakari. Kisiwa cha Kojani, kiko pembeni mwa kisiwa kikubwa cha Pemba. Kina Shehia mbili, Kojani anakoongoza Bakari na Mpambani kwa Sheha Omary Ali Omary.
Bakari alikuwa akijibu swali kama amepata kusikia/anaujua mpango mkubwa wa Uchumi wa Buluu, wa Rais Dk. Hussein Mwinyi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, unaolenga kubadili maisha ya Wazanzibar kwa kuifanya Bahari na mazingira yake kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya nchi.
Ni wavuvi kama hawa wa Kojani walioenea katika maeneo mbalimbali ya nchi ambao Dk. Mwinyi na timu yake wamedhamiria kuwafikia na kubadili maisha yao.
Serikali ya Dk. Mwinyi imetenga shilingi bilioni 36.5 zitakazotumika kuwezesha makundi mbalimbali ndani ya jamii kushiriki katika mpango mzima wa Uchumi wa Buluu.
Na kwa wavuvi kama Sheha huyu, yaani wale wavuvi wadogowadogo wapatao 5,770, watapatiwa maboti yapatayo 577 na nyenzo mbalimbali za uvuvi ili kuwawezesha badala ya kuvua kilo chache tu za samaki kama walivyozowea, wakipata vyombo sasa waende kwenye kina kikubwa zaidi cha bahari na wavue samaki kwa tani na tani.
Anasema Dk. Mwinyi kwamba wamekusudia kuitumia Bahari kujenga Uchumi wa Buluu ulio endelevu kuwafanya wavuvi na makundi mengine kama ya Wanawake kushiriki katikia kujiletea maendeleo.
“Badala ya mvuvi kupata kilo mbili kwa sababu hawezi kufika kwenye kina kirefu, sasa awezeshwe kwanza kwenda kwenye kina kirefu cha bahari na awe na nyavu stahiki za kuvua samaki.
Tunasema shughuli hii iwe endelevu kwa maana kwamba ule uvuvi wa nyavu zisizostahiki au wa kupiga mabomu unaoharibu mazingira unaachwa," anasema Dk. Mwinyi.
Katibu Mkuu, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Dk. Aboud Jumbe |
“Unaleta faida za kijamii na kiuchumi kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo kwa kuchangia katika upatikanaji wa chakula, kuondoa umasikini, kuongeza ajira, kuimarisha afya, kuleta usawa na utulivu wa kisiasa, ” anasema Dk. Jumbe kwenye sehemu ya mada yake ya Uchumi wa Buluu aliyowasilisha katika Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Wahariri, mwezi huu, Zanzibar.
Kwa mujibu wa Dk. Jumbe,
ukiacha wavuvi wadogowadogo watakaofikiwa, Mpango huu unawalenga pia Wanawake
wapatao 5,000 ambao hushiriki kwenye ukulima au ufugaji wa mazao ya baharini
kama Mwani. Kundi hili nalo litanufaika na maboti yapatayo 500 na nyenzo zake.
Dk. Jumbe anasema kwa ujumla kwa Zanzibar Uchumi wa Buluu utakuwa ni shirikishi ukilenga kupata ushiriki wa kila mmoja.
Ziara ya kisiwani Kojani imeisha, Wahariri wanarudi Chakechake, Pemba. |
Dk. Jumbe anasema katika
ujumla wake Sera ya Uchumi wa Buluu ya Zanzibar imeweka maeneo kadhaa ya
kipaumbele ambayo ni pamoja na Uvuvi na Kilimo cha mazao ya baharini, Mafuta na
Gesi, Utaalii Endelevu, Nishati Mbadala, Uwezeshaji wa Wanawake na
Usafi/utunzaji wa Mazingira.
0 comments:
Post a Comment