Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 27 Januari, 2022 ameshiriki kwa njia ya mtandao Mkutano wa Dunia wa kusherehekea mafanikio ya miaka 10 ya Tamko la London na kuzindua Tamko la Kigali la kujitoa kwa asilimia 100 kutokomeza Magonjwa ya Tropiki Yasiyopewa Kipaumbele (NTDs).
Katika Mkutano huo, Mhe. Rais
Samia amesema Tanzania ni moja ya nchi zilizoathirika kwa kiasi kikubwa na magonjwa
hayo ambapo zaidi ya watu milioni 29 duniani wanahitaji matibabu ya angalau ugonjwa
mmojawapo.
Mhe. Rais Samia amesema
magonjwa hayo hasa minyoo ya tumbo kwa watoto huathiri makuzi ya akili na huwafanya
kukosa fursa ya kupata elimu kwa wakati sahihi.
Mhe. Rais Samia amesema
kupambana na magonjwa hayo kunahitaji uwekezaji mkubwa ili kuhakikisha
upatikanaji endelevu wa huduma na ufuatiliaji wa kutosha.
Aidha, Mhe. Rais Samia
amebainisha kuwa uchache wa rasilimali na vipaumbele shindani vimekuwa vikizuia
jitahada za kupunguza na kutokomeza kasi ya ueneaji wa magonjwa hayo.
Vile vile, Mhe. Rais Samia
amesema licha ya changamoto zinazojitokeza, Tanzania imepiga hatua kubwa katika
mapambano dhidi ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutokana na mikakati
madhubuti ya Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
Pia, Mhe. Rais Samia ametolea
mfano Tanzania kwa baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na
magonjwa hayo kwa baadhi ya Wilaya ambapo maeneo husika yaliyohitaji matibabu
ya kinga dhidi ya ugonjwa wa matende imepungua kutoka wilaya 119 mwaka 2004
hadi kufikia wilaya 8 mwaka 2021.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema
Tanzania imepunguza idadi ya wilaya zinazohitaji matibabu ya kuzuia Trakoma
kutoka wilaya 71 mwaka 2012 hadi kufikia wilaya 9 mwaka 2021, na pia imepunguza
idadi ya watu wanaohitaji upasuaji wa Trakoma kutoka 167,000 mwaka 2012 hadi
27,000 Desemba 2021.
Mhe. Rais Samia amesema
anaamini kwamba, kupitia mkutano huo, maisha ya wananchi yatabadilika ikiwemo
mamilioni ya wasichana na wanawake nchini Tanzania ambao wapo katika hatari ya
kuambukizwa magonjwa hayo.
Pia Mhe Rais Samia amebainisha
kuwa dhamira walioahidi katika mkutano huo itasaidia kujenga usawa wa
upatikanaji wa huduma bora za afya, ambayo ni muhimu katika kupunguza
maambukizi ya magonjwa hayo yanayoweza kuzuilika.
Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia
amesaini Azimio la Kigali kuhusu Magonjwa ya Tropiki Yasiyopewa Kipaumbele (NTDs)
ili kujitoa kwa asilimia 100 kutekeleza Azimio hilo.






0 comments:
Post a Comment