Rais Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wanahabari mara baada ya
kumaliza mazungumzo na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wanahabari mara baada ya
kumaliza mazungumzo na Gavana mteule wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Profesa
Florens Luoga (kushoto) na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) anayemaliza muda
wake Profesa Benno Ndulu Ikulu jijini Dar es Salaam.
*************
RAIS
John Magufuli amesema, mwezi ujao Serikali itatoa Sh bilioni 200 kwa ajili ya
kulipa madeni ya ndani yatakayokuwa yamehakikiwa yakiwemo ya wazabuni
mbalimbali waliotoa huduma katika taasisi za serikali, madai ya walimu na madai
ya wakandarasi.
Rais
Magufuli ametoa kauli hiyo leo, wakati alipokuwa akiagana na Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) anayemaliza muda wake, Profesa Benno Ndulu leo Ikulu,
jijini Dar es Salaam.
“Nasisitiza
madeni tutakayolipa ni ya ndani, na tutalipa madeni ambayo yamehakikiwa, kwa
hiyo maandalizi ya kutoa fedha hizo yaanze mara moja na ni matarajio yangu
fedha hizi zitasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wetu” amesema Rais Magufuli.
Aidha,
amempongeza Profesa Ndulu kwa utumishi wake wa miaka 10 na kazi nzuri
aliyoifanya ya kusimamia uchumi ambapo katika kipindi hicho kasi ya ukuaji wa
uchumi imeongezeka kwa wastani wa asilimia 5 hadi asilimia 7 na kuimarisha
usimamizi wa benki na maduka ya kubadilishia fedha.
Mengine ni
kusimamia ongezeko la akiba ya fedha za kigeni inayoiwezesha nchi kumudu
kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi sita na kuanza kwa utekelezaji wa miradi
mikubwa ya ujenzi wa reli, umeme, ununuzi wa ndege na mingine.
“Nakushukuru
sana Prof. Ndulu, umefanya kazi nzuri ya kusimamia uchumi wa Taifa letu, ndio
maana leo unamaliza muda wako lakini tayari Benki ya Dunia na kamisheni ya
dunia inayoshughulikia teknolojia na maendeleo shirikishi wanakuhitaji ufanye
nao kazi, na mimi nimeidhinisha uende ukatuwakilishe” amesema.
Prof. Ndulu
amemshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kufanya nae kazi tangu alipoingia
madarakani na amebainisha kuwa anafurahi kumaliza kipindi chake huku uchumi wa
nchi ukiwa mzuri.
Aidha,
amempongeza Rais Magufuli kwa miongozo muhimu iliyosaidia kuimarisha uchumi
ikiwemo kudhibiti mfumuko wa bei ambao mwezi Novemba 2017 ulifikia asilimia 4.4
na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.8
hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 6 hivi sasa, hali ambayo imeimarisha
uwezo wa Serikali kujiendesha na kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo.
“Nimekuja
kumuaga Mhe. Rais na kumshukuru, nafurahi kuwa naondoka wakati hali ya uchumi
ikiwa nzuri, Taifa linakopesheka na kuna mazingira mazuri zaidi ya uchumi
kuendelea kukua, nampongeza sana Mhe. Rais kwa kusimamia mambo mbalimbali
muhimu ya kuimarisha na kukuza uchumi katika kipindi chote nilichofanya nae
kazi” amesema Prof. Ndulu.
Rais
Magufuli pia amezungumza na kumpongeza Gavana Mteule Profesa Florens Luoga kwa
kupokea uteuzi wake na amemtaka kufanya kazi ya kusimamia uchumi wa Taifa kwa
ufanisi mkubwa zaidi ili nchi ipige hatua za maendeleo kwa kasi zaidi.
Baada
ya mazungumzo hayo, Prof. Luoga amemshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi huo na
kumhakikishia kuwa ataisimamia BoT ili iendelee kuwa chombo imara cha kusimamia
uchumi wa nchi, kuisimamia fedha ya Tanzania na kuhakikisha nchi inatekeleza
miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha
kisasa (Standard Gauge), ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius
Nyerere Jijini Dar es Salaam na mradi wa umeme katika maporomoko ya maji ya mto
Rufiji (Stiegler’s Gorge).
0 comments:
Post a Comment