Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) wakifurahia kuona medali ya
dhahabu aliyoivaa Mwanaridha Alphonce Simbu ambayo aliinyakuwa katika
mashindano ya Mumbai Marathon nchini India na tuzo aliyoipata hivi
karibuni baada ya kushika nafasi ya tano katika mashindano ya London
Marathon. Waziri Mkuu alikutana na mwanariaha huyo kwenye viwanja vya
bunge mjini Dodoma Aprili 27, 2017.
*************
BUNGE la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, leo Aprili 27,2017 limezizima kwa nderemo na shangwe pale
alipotambulishwa rasmi mwanariadha Alphonce Simbu, Mshindi wa medali ya dhahabu
wa Mumbai Marathon, na moja ya washindi wa London Marathon.
Mwanariadha huyo ambaye pia ni
balozi maalum wa DStv, alilitembelea Bunge kama mgeni maalum wa Waziri wa
Habari, Utamaduni na Michezo Harison Mwakyembe akiambatana na muwakilishi wa
DStv Johnson Mshana na maafisa kadhaa waandamizi wa Jeshi la kujenga Taifa
akiwemo Kanali K.J Mziray – Mkuu wa Utawala na Mafunzo wa JKT
Mara baada ya naibu spika wa
Bunge Dk. Tulia Akson kumtaja Simbu, bunge lilizizima kwa shangwe kwa muda hali iliyoashiria kuraha kubwa kwa wabunge
kuweza kumshuhudia mwanariadha huyo ambaye ni tegemeo kubwa la Tanzania katika
mashindano ya riadha ya Dunia yatakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu jijini
London.
Baada ya ziara hiyo, Simbu
alipata fursa ya kusalimiana na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kassim Majaliwa na kisha kuwa na mazungumzo mafupi na Waziri Mwakyembe.
Akiongea wakati wa kupiga
picha ya pamoja na Simbu, Waziri mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza sana
mwanariadha huyo na kusema kuwa Serikali
inatambua na kuthamini sana jitihada zilizofanywa na wadau wote katika
kufanikisha ushindi wa Simbu. Pia alimtakia kila la heri katika maandalizi na
kisha ushiriki wake katika mashindano ya Dunia yanayomkabili mwishoni mwa mwaka
huu.
Naye Waziri mwenye dhamana ya Michezo Harison
Mwakyembe ambaye ndiye aliyemualika Simbu Bungeni, alisema kuwa wizara imekuwa
ikishirikiana na wadau kwa karibu ambapo hata wakati wa Safari ya Simbu kwenda
London, wizara ilihakikisha safari hiyo inafanikiwa. Ameonyesha kufurahishwa
kwake na vipaji vilivyopo na kusema nguvu za ziada zitawekwa ili kuhakikisha
kuwa vipaji hivyo vinaibuliwa na kukuzwa kwa manufaa ya taifa zima.
Kwa upande wake, Simbu alisema
kitendo cha yeye kualikwa bungeni kimempa faraja kubwa na pia alifurahi sana
kuona jinsi wabunge walivyomshangilia na kumpongeza. “Kwakweli ujio wangu
bungeni umenipa faraja kubwa kuona ni jinsi gani wabunge wote walivyofurahishwa
na mafanikio niliyopata na sifa niliyoiletea nchi. Hii imenipa sana moyo na
uzalendo kwani ni dhahiri kuwa taifa zima liko nyuma yangu na linanunga mkono
kikamilifu” alisema Simbu
Alitoa shukrani za pekee kwa
wadhamini wake DStv, pamoja na Waziri Mwakyembe kwa jitihada kubwa anazofanya.
Amesema anaamini kwa mwenendo huu yeye, wanariadha wengine na wanamichezo wote
wa Tanzania watafika mbali na hatimaye Tanzania itakuwa kinara katika ulingo wa
michezo duniani. Pia alilishukuru Jeshi la Kujenga Taifa JKT kwa kumruhusu
kufanya mazoezi na kushiriki katika mashindano mbalimbali.
Simbu ambaye ni miongoni mwa
wanariadha bora wa Tanzania alivunja rekodi yake aliyoiweka mwaka jana nchini
Japan ya muda wa 2:09:19 na hatimaye katika mashindano ya London Marathon mwaka
huu alitumia muda wa 2:09:10 ambao ndio muda wake bora zaidi.
Simbu ni miongoni wa wachezaji wa timu ya
taifa ya riadha watakaoshiriki mbio za Dunia mwezi Agosti mwaka huu jijini
London.
0 comments:
Post a Comment