Maafisa
Habari na Tehama kutoka Halmashauri za Mikoa ya Kigoma, Katavi na Kagera wakiendelea na mafunzo ya kutengeneza tovuti za Halmashauri na Mikoa kupitia mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) mjini Kigoma.
Maafisa
Habari na Tehama kutoka Halmashauri za Mikoa ya Kigoma, Katavi na Kagera
wakiendelea na mafunzo ya kutengeneza tovuti za Halmashauri na Mikoa
kupitia mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) mjini
Kigoma.
Na
Nashon Kennedy, Kigoma
MAAFISA
habari na Tehama nchini wametakiwa kufanya kazi zao kwa weledi ili kuhakikisha
taifa linakuwa na serikali yenye utendaji inayowajibika vyema kwa wananchi
wake.
Rai hiyo
imetolewa mjini hapa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Chalres Pallanjo
alipokuwa akifungua mafunzo ya siku saba kwa Maafisa Habari na watalaam wa
tehama wa mkoa na halmashauri kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi
yanayofadhiliwa na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma unaojulikana
kama Public Sector System Strengthening (PS3).
“Kupitia
kazi zenu, mnayo dhamana ya kuhakikisha kuwa tunakuwa na Serikali yenye
utendaji unaowajibika kwa wananchi wake”, alisema.
Alisema hali
hiyo itawezekana endapo taarifa sahihi zitawekwa mara kwa mara katika tovuti za
halmashauri na zile za mikoa na sio kusubiri hadi wananchi wapige kelele kwa
ajili ya kuhoji masuala wanayopaswa kufahamishwa tangu mwanzo.
Alisema
kwa kipindi kilichopita, maafisa habari na tehama wamekuwa na changamoto ya
namna gani ya kuhakikisha kuwa taarifa za maeneo yao zinatoka kwa wakati
lakini pia na utayarishaji wa tovuti kama sehemu ya njia ya mawasiliano.
“Ni
halmashauri chache zenye tovuti hapa nchini, na hata zile zenye tovuti, bado
ipo changamoto ya tovuti hizo kutofanana, kwa maana ya government Website
Framework na hivyo kukosa taarifa zingine muhimu”, alisema.
Aliushukuru
Mradi wa Ps3 kwa kufadhili mafunzo hayo kupitia Shirika la Maendeleo la
Kimataifa la Marekani (USAID) ambapo alisema Tanzania inaweza kuiga mfano wan
chi zilizoendelea kama Marekani ambayo imepiga hatua kubwa kwenye mambo ya
uwazi na utawala bora kwa kuwapa wananchi taarifa mbalimbali zinazohusu nchi na
maendeleo yao.
Akitoa
mfano, alisema serikali ya Marekani kupitia Ikulu yake imekuwa ikitoa taarifa
mbalimbali kila wiki kupitia kwa wanahabari pamoja na mitandao ambazo zimekuwa
zikifuatiliwa na kutumiwa kwa karibu na wananchi wake na duniani kote.
“ Huu ni mfano mzuri ambao hata
sisi tunaweza kuuiga. Tuanze basi
kulifanya hilo
kwa kutumia hizi tovuti katika maeneo yetu”,
Kwa
upande wake, Mratibu wa PS3 Mkoa wa Kigoma Simon Mabagala alisema lengo la
mafunzo hayo kwa maafisa habari na Tehama ni kuiwezesha serikali kuwasiliana na
wananchi wake katika masuala na taarifa muhimu za maendeleo kwenye maeneo yao.
Naye
Mwezeshaji Kiongozi wa Mafunzo hayo Joctan Bikombo alisema lengo la kutoa
mafunzo hayo ni kuwaunganisha maafisa hao ili waweze kutatua changamoto
zinazowakabili kwa njia ya mawasiliano kupitia tovuti zao.
Alisema mafunzo hayo yanafadhiliwa na PS3 kwa
kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA).
Lengo kuu
la mafunzo hayo ni kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza kupata taarifa
mbalimbali zinazohusu maeneo yao husika, kama
ilivyo haki yao
ya Kikatiba.
Mafunzo
hayo yaliyoanza leo(jana) ambayo ni ya awamu ya pili yanaenda sambamba katika
mikoa yote ya Tanzania Bara ambayo haijapata mafunzo hayo na kilele cha mafunzo
hayo ni Machi 27 mwaka huu, ambapo halmashauri zote na mikoa zilizo kwenye
mafunzo zitazindua tovuti zao kwa pamoja.
Kwa
upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, wamesema mafunzo hayo
yatawawezesha kupata ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi zao kwa haraka na kwa
wakati.
Kwa
upande wake, Kaimu Afisa Habari wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Gadi
Mwatebela alisema ameyapata mafunzo hayo kwa wakati muafaka na matarajio yake
ni kujua namna ya kufungua na kutumia tovuti.
“Jamii
sasa itakuwa na uwezo wa kupata taarifa nyingi za maendeleo za halmashauri
yangu baada ya mafunzo haya”, alisema.
Kwa
upande wake, Afisa Tehama Msaidizi kutoka Halmashauri ya Uvinza mkoani Kigoma
Grace Moshi alisema ana matarajio ya kujifunza namna ya kutengeneza tovuti ili
awe na uwezo wa kutengeneza tovuti kwenye halmashauri yake.
Naye
Afisa Tehama kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Halidi Nyange alisema
matarajio yake ni kujua namna ya kutengeneza tovuti kwa kuingiza taarifa
mbalimbali za maendeleo na kujua namna ya kuboresha tovuti kwa maslahi mapana
ya wananchi.
“
Matarajio yangu ni kutaka kujua namna ya kujaza au kuingiza taarifa na matukio
mbalimbali ya taasisi au halmashauri kwenye tovuti ili kuwawezesha wananchi
kupekua na kupata taarifa hizo”, alifafanua.
0 comments:
Post a Comment