Nafasi Ya Matangazo

October 27, 2016

Kaimu Afisa Habari na Mawasiliano ambaye pia Ofisa Misitu Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Nurdin chamuya (Kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Jijiji Dar es Salaam jana kuhusiana na kukamatwa kwa lori lenye namba za usajili T676 ANQ lililokuwa linasafirisha mbao kinyume cha sheria kutoka Mkoani Kigoma kuja Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa wa Himasheria wa Wakala huyo, Arjason Mloge. 
Kaimu Afisa Habari na Mawasiliano ambaye pia Ofisa Misitu Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Nurdin chamuya (Kushoto) na Afisa wa Himasheria wa Wakala huyo, Arjason Mloge wakionesha sehemu ya mbao zilizokuwa zimefunikwa na katoni za sabuni ndani ya lori lenye namba za usajili T676 ANQ lililokuwa linasafirisha mbao hizo kinyume cha sheria kutoka Mkoani Kigoma kuja Jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa sehemu ya mbao hizo zikiwa zimefunikwa na sabuni ndani ya lori hilo.
Maofisa wa kikosi Dhidi ya Ujangili kanda ya Dar es Salaam na kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania wakitumia mbwa maalum wa kunusa (Sniffer Dog) kwa ajili ya kutambua bidhaa haramu ndani ya lori hilo. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Muonekano wa nje wa Lori hilo.
***************
Kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa kushirikiana na Kikosi Dhidi ya Ujangili kanda ya Dar es Salaam kimefanikiwa kukamata lori lenye namba za usajili T 676 ANQ lililokuwa likisafirisha mbao kinyume cha sheria huku zikiwa zimefichwa kwa kufunikwa na bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni ili zisionekane kiurahisi kwenye vituo vya ukaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Afisa Habari wa Wakala huyo, Nurdin Chamuya alisema tukio hilo limetokea tarehe 14 Oktoba, 2016 majira ya saa kumi usiku maeneo ya Amana, Ilala Jijini Dar es Salaam baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya uwepo lori hilo katika maeneo hayo.

Chamuya alisema baada ya kupata taarifa hizo vikosi hivyo vilifika eneo la tukio na kufanya mahojiano na baadhi ya wananchi waliokuwa karibu na lori hilo ambapo mmoja kati ya wahudumu wa lori hilo alieleza kuwa lori hilo lilitokea Mkoani Kigoma na kwamba lilikuwa limepakia mzigo wa sabuni na chupa za maji zilizotumika. Dereva wa lori hilo hakuweza kupatikana.

“Wahudumu hao walipotakiwa kufungua mlango wa lori hilo kwa ajili ya upekuzi zaidi walisita kwa madai kuwa hawakuwa na funguo za lori hilo, Hatimaye   waliwasiliana na mmlikiwa wa eneo ambaye alikuwa amekabidhiwa funguo kwa ajili ya ulinzi” alisema Chamuya.

Alieleza kuwa mmiliki huyo alipofika alisema, anamfahamu mwenye gari ambaye ndiye mpangaji wa eneo lilipokutwa gari na kwamba anazo taarifa za  gari hilo,  na ameombwa apokee mzigo na kuutunza hadi atakaporudi kutoka safari ya  Mwanza kwa tatizo la msiba wa Baba yake.

Baada ya mmiliki wa eneo hilo kufanya mawasiliano na mwenye gari kuhusu mzigo uliokuwa kwenye gari hilo, mwenye gari alieleza kuwa kwa taarifa za dereva wake na ajenti aliyepakia mzigo Kigoma, gari lake lilikuwa na chupa chakavu na sabuni kutoka Kigoma na hakuna aina nyingine ya mzigo kwa ufahamu wake na akaruhusu gari hilo kufunguliwa mbele ya mwenye eneo.

“Baada ya gari hilo kufunguliwa, kilichoonekana kwa urahisi ni sabuni na mifuko michache inayosomeka kwa nje kuwa ni dawa ya kuku. Baada ya upekuzi ndipo zilionekana mbao zilizokuwa zimefichwa chini ya katoni za sabuni. Tumeshikilia Lori hilo kwa hatua zaidi za kisheria.

“Kufuatia tukio hili, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania tunatoa onyo kali kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu kinyume cha sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2004 na kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi” alisema Chamuya.

Akizungumzia athari mbalimbali za vitendo hivyo vya uvunaji holela wa mazao ya misitu bila ya kufuata taratibu za kisheria za uvunaji endelevu alisema vitendo hivyo vinatishia nchi kuwa jangwa ambapo takwimu zinaonyesha jumla ya hekta 372,000 za misitu nchini hupotea kila mwaka kutokana na matumizi makubwa ya rasilimali hizo ambayo yanazidi uzalishaji wake kwa ujazo wa mita 19.5 milioni kwa mwaka.

Chamuya ametoa wito kwa wananchi wote nchini kushirikiana na Serikali katika uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za misitu na kuacha fikra potofu kuwa kazi hiyo ni ya Serikali pekee na taasisi zake kwakuwa faida zake hunufaisha jamii yote na vivyo hivyo kama athari zitajitokeza basi zitaikumba jamii yote bila kubagua.

Posted by MROKI On Thursday, October 27, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo