Usiku wa jana ulikuwa ni wa furaha ya aina yake kwa wadau mbalimbali waliokuwa wakiwania tuzo kwenye tamasha la kimataifa la filamu la ZIFF lililofanyika Zanzibar na miongoni mwa washindi hao ni Amil Shivji,ambaye pia ni mwalimu wa masuala ya uandaaji filamu kwenye idara ya sanaa ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.
Bw.Amil kupitia filamu ya AISHA iliyotengenezwa na kampuni ya Kijiweni Production kwa ushirikiano na shirika la Uzima kwa Sanaa(UZIKWASA) lilipo Tanga,kwa ujumla ilijishindia tuzo takriban nne katika kipengele kilichoshindanisha filamu za kiswahili, maarufu kama "bongo movie".
Filamu ya AISHA iliyotengenezwa Pangani-Tanga, imekwishachezwa kwenye zaidi ya matamasha thelathini(30) duniani, iliweza kuibuka kinara kwenye ZIFF kwa kutoa muongozaji bora(Omar Chande), muigizaji bora wa kike(Godliver Gordian), filamu bora(AISHA) na mhariri bora wa filamu(Momose Cheyo).
Mtengenezaji huyo wa filamu aliyewahi kujinyakulia tuzo kadhaa kupitia filamu za SHOESHINE pamoja na SAMAKI MCHANGANI, akitoa ushauri kwa vijana, wasanii chipukizi na pia wasanii wakongwe aliwasihi wasidharau umuhimu wa kuingia darasani kujinoa zaidi na kupata maarifa.
Bw.Amil aliongeza,"hata kama chuo si chaguo la kwanza ama hauchukulii kwa uzito, kuna warsha nyingi sana ambazo zinasaidia kukuza kipaji na uzoefu katika utengenezaji wa filamu. Tafadhalini endeleni kusoma, kudadisi mambo mbalimbali yanayoendelea ulimwenguni, na daima ujiulize filamu zako zitaongelea kuhusu nini".
Akiwashukuru wadau wa filamu alisiwasisitiza wajue tu kwamba Kijiweni productions ipo, na itaendelea kupambana na mifumo inayokandamiza na kunyanyasa watanzania na watu wote bila kujali rika, rangi au jinsia ya mtu.
Tamasha hilo la filamu huandaliwa kila mwaka na kushirikisha maonesho ya filamu na sanaa mbalimbali, utoaji tuzo na mafunzo kwa watengenezaji wa filamu.
Amil Shivji akipokea tuzo kwenye tamasha la ZIFF baada ya filamu AISHA kutangazwa filamu bora
0 comments:
Post a Comment