Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence
Milanzi (wa kwanza kushoto), hii leo akizindua Jarida Maalumu la Taasisi ya
Taaluma za Wanyamapori Pasiansi (Pasiansi Wildlife Training
Institute), iliyopo Jijini Mwanza. Shughuli hiyo imeambatana na
Uzinduzi wa Makala Maalumu ya Miaka 50 ya taasisi hiyo.
Askari wa Taasisi ya Wanyamapori Pasiansi Jijini Mwanza
Askari wa Taasisi ya Wanyamapori Pasiansi Jijini Mwanza. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
**************
Na BMG
SERIKALI imeahidi kuendelea kuijengea uwezo Taasisi ya Taaluma za
Wanyamapori iliyopo Pasiansi jijini Mwanza, ili kukabiliana na matukio ya
ujangili ambayo yametikisa nchi miaka ya karibuni.
Akizungumza na wanahabari katika uzinduzi wa Makala Maalumu ya
Maadhimisho ya miaka 50 na Jarida Maalum la taasisi hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya
Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, amesema taasisi hiyo
imetoa mchango mkubwa katika kufundisha askari wanyamapori ambao wamesaidia
kwenye vita dhidi ya ujangili na kupunguza matukio ya ujangili nchini.
Meja Jenerali Milanzi amesema katika miaka ya karibuni Tanzania
imetikiswa na matukio ya ujangili ambayo yamesababisha kuuawa kwa wanyamapori
wakiwemo tembo na kuhatarisha uwepo wa wanyama hao ambao ni kivutio kikubwa cha
watalii.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa Taasisi ya Wanyamapori Pasiansi na vyuo
vingine, serikali itaendelea kuvijengea uwezo wa kifedha na rasilimali watu ili
vitoe taaluma inayoendana na mahitaji katika kukabiliana na matukio ya
ujangili.
Mbali na kuvijengea uwezo vyuo hivyo, Meja Jenerali Milanzi, amesema
serikali pia inatambua umuhimu wa wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo ya
hifadhi na kwamba itaendelea kuwaelimisha wananchi hao ili washiriki kikamilifu
kwenye vita dhidi ya ujangili.
Taasisi ya Taaluma za Wanyamapori Pasiansi (Pasiansi Wildlife Training
Institute) ilianzishwa mwaka 1966 hivyo kesho june 15,2016 inatarajia
kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.
0 comments:
Post a Comment