RAIS John Magufuli ametangaza kumteua Dk Jim James Yonazi kuwa Mhariri Mtendaji
wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).
Taarifa ya Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, Ikulu, iliyotolewa kwa vyombo vya habari Juni 21, 2016 ilimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ilieleza kuwa Rais
Magufuli amefanya uteuzi huo kuanzia Juni 18,2016.
Kabla ya uteuzi huo, Dk Yonazi alikuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya
Maarifa katika Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).
Dk Yonazi
anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Gabriel Nderumaki ambaye uteuzi wake
ulitenguliwa na Rais kuanzia Machi 18, mwaka huu.
Dk Yonazi amemshukuru Rais Magufuli kwa kumuona anaweza kumsaidia
kazi kupitia kampuni hii ya magazeti na kusema amepokea uteuzi huo kwa
moyo mkunjufu.
Ameahidi kufanya kazi kwa weledi, kama ambavyo Rais Magufuli amemtaka
afanye kuongoza kampuni hii, inayozalisha magazeti ya HabariLeo,
HabariLeo Jumapili, Daily News, Sunday News na SpotiLeo.
Alitoa mwito kwa wadau mbalimbali, kushirikiana na TSN kufanya
magazeti ya serikali kuwa bora na yenye kuleta changamoto katika tasnia
ya habari.
Alisema anatarajia kufanya kazi na watu mbalimbali na jambo
ambalo anatamani kuona, ni ubunifu, habari za kweli na zinazokwenda na
wakati.
Akieleza mtazamo wake kuhusu tasnia ya habari na mambo ambayo
analenga kuyafanya baada ya uteuzi, Dk Yonazi alisema wananchi na hata
dunia kwa ujumla, ina hamu ya habari za kutoka Tanzania.
Alisema panahitajika ubunifu na mikakati kuhakikisha magazeti ya TSN
yanapeleka habari, siyo tu hapa nchini, bali pia kufikia nchi za nje
kama ilivyo kwa mashirika ya habari ya kimataifa ya BBC na CNN.
Alisema wakati magazeti ya TSN sasa yanafika nchi za Afrika
Mashariki, yanatakiwa kufika pia kwenye masoko ya kanda nyingine na nje
ya Afrika.
“Tufike mahali, magazeti yawe kwenye viganja vyetu…ningependa
sana kufikia hatua hii,” alisema Dk Yonazi, akimaanisha Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (Tehama), hususan simu, kutumiwa na wananchi wengi
kupata habari.
Alisema anatamani hata watu wa mataifa mengine, waandike habari zao
kutoka kwenye magazeti ya nchini hususani ya serikali.
DK YONAZI NI NANI?
Dk Yonazi ana Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Serikali Mtandao ya
Chuo Kikuu Groningen cha Uholanzi na ana Shahada ya Uzamili katika
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama ) na Utawala kutoka Chuo
Kikuu cha Keele, Uingereza.
Amewahi kuwa mhadhiri mwandamizi, mtafiti na mshauri katika Chuo cha
Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar es Salaam. Pia amefanya utafiti katika
masuala mbalimbali kuhusu uvumbuzi, mipango mikakati ya kiutawala katika
Tehama.
Aidha, amebobea katika masuala ya mipango ya kiutawala katika Tehama,
Uvumbuzi katika Utawala, Serikali Mtandao na Marekebisho ya Sekta ya
Umma, Tehama katika Maendeleo na uvumbuzi katika Tehama. Vile vile
amehusika katika mikakati mbalimbali ya Tehama hapa nchini na Nchi za
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
Pia amewahi kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za kimataifa na za
nchini katika ngazi za Umeneja na majukumu makubwa ya usimamizi wa
kitaaluma. Dk Yonazi alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Kompyuta katika
chuo cha IFM, akisimamia maendeleo katika ugunduzi na ubunifu,
iliyowezesha chuo hicho kufanya vizuri katika eneo hilo.
Amewahi kuwa mjumbe wa bodi kadhaa, ikiwamo Bodi ya Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyovunjwa na Rais Magufuli mwishoni mwa
Aprili mwaka huu na Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Arusha. Pia ni
mjumbe wa Kamati ya Ushauri ya Tehama katika Baraza la Taifa la Mitihani
(Necta) na Mratibu wa Kituo cha Tehama cha Utafiti na Ubunifu (CiRi). Source: Habarileo;Picha:FK Blog - 2014.
0 comments:
Post a Comment