Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Charles Boniface Mkwasa
amesema kwamba mchezo ujao kati ya Mapharao wa Misri na Taifa Stars,
utakuwa ni fainali ya kuamua taifa litakalofuzu katika fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika AFCON hapo mwakani kutoka kundi G.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo kati ya
Harambee Stars ya Kenya na Taifa Stars ya Tanzania Mei 29, 2016,
uliofanyika Uwanja wa Moi Kasarani, Mkwasa maarufu kama Master anasema
kwa msimamo na hali ilivyo kwa sasa, “Najua Misri wanatufuatilia. Na
hata Kenya kwa siku zote tatu walikuwako. Najua Misri wanahitaji sare
ili wafuzu kwa fainali hizi, lakini hawataipata Tanzania.”
Mkwasa anasema mchezo dhidi ya Misri, ana uhakika vijana wake
watajitahidi ili kupata matokeo mazuri baada ya Jumapili kufanya vema
dhidi ya Harambee Stars waliocheza mechi hiyo mbele ya mashabiki wao
wachache ambao pia hawakuchangamka kama wale wa Tanzania ambao licha ya
kuwa ugenini walichangamsha mji na uwanja.
Wakati Misri wana pointi saba, Taifa Stars ina pointi moja na hivyo
wa kuibania au kupindua matokeo ya Misri isiende AFCON mwakani, basi ni
Tanzania hasa kama itawafunga Mapharao Jumamosi kabla ya kwenda Nigeria
Septemba, mwaka huu kucheza na Nigeria.
“Kama nilivyosema, Misri wanakujawanahitaji pointi moja. Lakini sisi
tunahitaji pointi tatu. Mchezo wa leo unatosha kuona mapungufu
(upungufu). Maana ilikuwa mechi ngumu iliuyojaa nyota wote wa Kenya
ambao ni professionals, lakini mimi nilikuwa na local based players na
matokeo yamekuwa hayo.
“Tilianza kufunga bao, lakini wakarudisha. Bora mchezo umeishia hivi
maana najua Wakenya hawana uvumilivu, tungewafunga hapa sijui kama
tungetoka salama,” amesema Mkwasa ambaye baadhi ya waandishi, hususani
wale wa Kenya walianguka kicheko kuashiria kuwa kuna matatizo katika
utawala wa soka.
Mkwasa anasema ana taarifa namna ambavyo Misri wanaifuatilia Taifa
Star hususani ukusanyaji wa video kwa ajili ya kuona aina ya soka la
Tanzania, huku akisema: “Hawatafanikiwa kwa sababu soccer is the game of
different approach (Soka ni mchezo wenye mifumo tofauti). Hivyo
tulivyocheza na Kenya sivyo nitakavyocheza na Misri, nitakuwa na
approach yake.”
Anasema ushindi wa Jumamosi ijayo ni wa kuvuna pointi tatu ili kupata
kasi ya kushinda mchezo dhidi ya Nigeria na kufungua ukurasa mpya wa
Taifa Stars kutengeneza mazingira mazuri ya kuwashinda Nigeria katika
mchezo wa mwisho hatua ya makundi utakaofanyika Septemba, mwaka huu.
“Tunaomba Wakenya mtuombee. Nasi tunawaombea ili kama wote inatokea
mwaka huu tunakosa mafasi, basi iwe kheri kwa kipindi kijacho. Sisi
tumekuja kucheza kwenu katika mji wenu wenye baridi basi nanyi karibuni
siku moja dar es Salaam, Tanzania katika mji wetu wetu wenye joto,
huenda mkaambulia sare vile vile,” anasema.
Mkwasa alipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (FKF), kwa kuandaa
mchezo huo angalau kwa asilimia 70 kwa kushirikiana na Tanzania
iliyojazia gharama za juu sambamba vijana wake kwa kucheza kwa kujituma
licha ya kuwakosa nyota wake wa kulipwa na hivyo kupata picha na mbinu
sahihi za kuivaa Misri Jumamosi ijayo.
“Bado tunaendele kujenga timu yetu, wengi ni vijana kama mlivyoona na
wengine ni mara ya kwanza wanacheza. Nimewapa nafasi na mmeona uwezo
wao, bila shaka tutafanya vema maana wengine ni under 21 wako kwenye
kikosi. Huko mbele tutakuwa na timu nzuri,” anasema Mkwasa akimtolea
mfano Shiza Ramadhani ambaye alipewa nafasi kwa mara ya kanza katika
kikosi cha kwanza akichukua winga ya kulia.
0 comments:
Post a Comment