Rais wa VICOBA Devotha Likokola amewaasa wafanyakazi waliopo kwenye ajira
hususani wanawake kujiunga
na vikundi vya VICOBA ili waweze kujikwamua kimaisha na kuboresha maisha ya
familia zao.
Bi.Likokola alitoa wito huu jana wakati wa mafunzo ya ujasiriamali kwa
wanawake wanaofanya kazi katika kampuni ya DarBrew inayotengeneza kinywaji cha
Chibuku iliyofanyika katika kiwanda cha Dar es Salaam.
Alisema kwa kujiunga na VICOBA wanawake hao watakuwa na uwezo wa kupata
mikopo yenye masharti nafuu na kupata mafunzo ya fursa mbalimbali za kibiashara
zilizopo na kuwakutanisha na wanawake wenzao ili waweze kubadilishana uzoefu wa
maisha.
“Kuna dhana kwamba VICOBA ni kwa ajili ya akina mama wasio na ajira na
wanawake wengi walioajiriwa kutotaka kujiunga na vikundi hivi kwa ajili ya kuwakwamua kiuchumi matokeo yake waajiriwa wengi wanaachwa nyuma kiuchumi kutokana
na kutegemea mshahara wa mwisho wa mwezi tu”.Alisema Likokola.
Aliwaasa wanawake kuchangamkia fursa hii ambayo pia imeanza kuchangamkiwa na wanaume na kuwataka waajiri kuwezesha wafanyakazi wao kupata
mafunzo ya ujasiriamali ili yawaandae kujiajiri baada ya muda wao wa ajira
kumalizika na hata wakiwa makazini bado kuna shughuli mbalimbali za
ujasiriamali wanaweza kuzifanya kwa ajili ya kuinua vipato vyao.
Katika mafunzo hayo wanawake wafanyakazi wa DARBREW walipatiwa mwongozo
wa kujiunga na vikundi vya VICOBA ambapo pia walipatiwa elimu ya
ujasiriamali,jinsi ya kuibua miradi na kuiendesha pia walipatiwa ushauri wa
jinsi ya kutumia fedha kwa malengo ya kufanikiwa na umuhimu wa kujiwekea akiba.
VICOBA ambayo ilianzishwa ikiwa na mtizamo wa kusaidia vikundi vya
wanawake wa vijijini kiuchumi imezidi kupanua huduma kwa wanawake wengi nchini
ambapo hivi sasa inao mtandao wa vikundi zaidi ya 10,000 nchi nzima vyenye
wanachama zaidi ya 500,000 na mtaji unaofikia zaidi ya shilingi bilioni 75
Rais wa Vicoba endelevu Tanzania, Devotha Likokola, akitoa mafunzo ya elimu ya vicoba kwa wafanyakazi wa
Kiwanda cha Chibuku (Darbrew Ltd) cha Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Vicoba mkoa wa Dar es Salaam, Amina Mkuwa (kulia) akigawa vipeperushi vya taasisi hiyo
wakati wa mafunzo hayo.
Wafanyakazi wa Chibuku (Darbrew Ltd)Ubungo jijini Dar es Salaam, wakiwa
katika picha ya pamoja
na Rais wa Vicoba endelevu Devotha Likokola mara baada ya kumalizika kwa mafunzo.
Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha Chibuku (Darbrew Ltd) wakisoma katiba ya Vicoba
0 comments:
Post a Comment