Nafasi Ya Matangazo

September 04, 2015

DAR ES SALAAM, Septemba 4, 2015—Zaidi ya wawakilishi 400 kutoka kwenye serikali, vyuoni, sekta binafsi, asasi za kiraia na mashirika ya kimataifa ya maendeleo wanakutana katika jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kongamano la siku mbili kubadilishana uzoefu na utendaji bora ili kukuza uzalishaji na matumizi ya data za umma katika bara la Afrika, na kuongeza mchango wake katika maendeleo ndani ya bara.

“Uwazi na uwajibikaji ni mambo muhimu sana kwa Serikali na watu wake kwa sababu Serikali inapokuwa wazi, watu wanajua ni kitu gani kinachoendelea, na wanaweza kuiwajibisha Serikali yao, na Serikali itakuwa na azma ya kutoa huduma,” alitamka Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. 

Ili kuadhimisha ufunguzi rasmi wa Kongamano la Afrika la Data za Umma, lililoandaliwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atatoa hotuba adhimu ya kuelezea umuhimu wa data za umma kwa maendeleo ya Bara la Afrika kwa washiriki kutoka nchi zaidi ya 30.    

“Data za umma” ni data zinazotolewa bila gharama na ambazo umma unaweza kuzipata, zinazoweza kutumika, kurudiwa na kusambazwa tena na tena. Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kutumia mbinu ya Tathmini ya Utayari wa Data za Umma mnamo Juni, 2013 na kuanzia hapo, nchi nyingine za Kiafrika, pamoja na Nigeria, Afrika Kusini, Uganda, Kenya, Rwanda, Ghana, Burkina Faso, Sierra Leone, Senegal, Morocco, Misri, Tunisia, na Ethiopia, nazo zimeanzisha programu zao wenyewe za data za umma. Mnamo Machi 2015, nchi kadhaa za Kiafrika zilikutana kusaini Makubaliano ya Afrika kuhusu Data na kuendeleza misingi ya takwimu rasmi pia na uwazi.

Katika kujenga juu ya msukumo huu, Kongamano la Afrika la Data za Umma linatoa fursa kwa washiriki kushirikishana uzoefu wao wa kitendaji na programu za data za umma katika nchi za Kiafrika, kuendeleza mifumo kwa ajili ya ushiriki wa wananchi, uboreshaji na ufuatiliaji wa shughuli za serikali na utoaji wa huduma. Wataalamu pia watashirikishana mikakati yao ya data za umma kama kichocheo cha ukuaji wa sekta binafsi, ajira na ubunifu. 

Ili kusaidia juhudi hizi, programu ya awali kabla ta mkutano iliandaa warsha na mafunzo ya kitaalamu kuhusu mada mbalimbali, pamoja na mafunzo mafupi ya stadi za data na darasa kuu la data za umma. 

“Katika nchi nyingi za dunia, serikali ya uwazi na data za umma zimeleta mageuzi katika ukuaji uchumi, kutengeneza ajira, na jinsi wananchi wanavyojishughulisha na serikali yao, na ni jambo la kufurahisha kuona jambo hili linafanikiwa hapa nchini,” anasema Bi. Bella Bird, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania. “Mkusanyiko huu unatoa fursa bora zaidi katika kuwaleta pamoja jamii ya wataalamu wa data za umma ili kuendeleza mbinu bunifu kwa ajili ya kuleta maendeleo ya bara la Afrika.”

Benki ya Dunia kupitia kitengo chake cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, pia na Mifumo ya Utawala Duniani, imedhamiria kuvuna uwezo wa data za umma kwa ajili ya kupunguza umasikini na kuchochea maendeleo, pia kukidhi malengo mapya ya maendeleo endelevu ambayo yataidhinishwa na Umoja wa Mataifa mnamo Septemba 2015.
Posted by MROKI On Friday, September 04, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo