Sehemu ya
wanachuo wa ADEM wakimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano Bw. Cosmas
Mwaisobwa (haonekani kwenye picha hii).
********
Uelewa mdogo wa masuala ya utoaji
wa mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu umeendelea kuwa chanzo cha baadhi ya
wahitaji wa mikopo kulalamika bila kwanza kutafuta chanzo cha wao kutopata
mikopo hiyo.
Hayo yamebainika hii leo katika
ziara ya mafunzo ya wanachuo 147 kutoka Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu
(ADEM) unaoendeshea shughuli zake Bagamoyo mkoani Pwani waliofika Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa ziara ya mafunzo.
Miongoni mwa maswali yaliyoulizwa
na wanachuo hao ni pamoja na uwezekano wa wafanyakazi kupatiwa mikopo, vigezo
vya utoaji mikopo na jinsi ya kubaini waombaji wa mikopo wenye sifa za kupata
mikopo hiyo. Maswali mengine yalilenga kujua jinsi Bodi inavyowatambua
wanufaika wa mikopo ambao mikopo yao imeiva tayari kurejeshwa.
Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa
Habari, Elimu na Mawasiliano Bw. Cosmas Mwaisobwa aliwasilisha mada
iliyojumuisha historia fupi ya Bodi,
Sera ya Uchangiaji, Muundo wa Uongozi, Utaratibu wa Utoaji Mikopo na Utaratibu
wa Urejeshwaji wa mikopo ya elimu ya juu.
Akitoa shukrani kwa niaba ya
wanachuo hao, Mkufunzi aliyeandamana nao
Bibi Rhoda Samwepa, ameelezea kufurahishwa kwake na jinsi Bw. Mwaisobwa ambaye
pia ni Msemaji wa Bodi, alivyotolea ufafanuzi kwa ufasaha masuala yanayoonekana
kuwa na utata kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na kwamba anaona
umuhimu wa wanufaika kurejesha mikopo hiyo ili wahitaji wengine waweze
kunufaika.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu imekuwa ikipokea makundi mbalimbali ya wadau wa elimu wanaofika
kwa lengo la kujifunza masuala ya utoaji mikopo, vigezo na masharti ya utoaji
mikopo na utaratibu wa kurejesha mikopo hiyo na hivyo kuendelea kuongeza uelewa
wa mikopo ya wanafunzi kwa idadi kubwa zaidi ya wadau.
0 comments:
Post a Comment