Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue, amemsimamisha kazi kwa muda Ndugu
Eliakim Maswi, Katibu Mkuu ya Wizara ya Nishati
na Madini, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, kama ilivyoelekezwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Balozi
Sefue amemsimamisha kazi Ndugu Maswi kuanzia leo, Jumanne, Desemba 23, 2014,
kwa kutumia madaraka aliyonayo kama Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma
wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.
Taarifa
iliyotolewa na Ofisi ya Balozi Sefue mjini Dar es Salaam imesema kuwa amechukua
hatua hiyo “Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Na. 8
ya mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa)” ambapo “Katibu Mkuu Kiongozi ndiye
Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo
Makatibu Wakuu.”
Badala
yake, Balozi Sefue amesema kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini,
Mhandisi Ngosi C. Mwihava atakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na
Madini, hadi uchunguzi dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi utakapokamilika.
Taarifa
hiyo ya Balozi Sefue pia imekariri kauli ya Rais Kikwete katika hotuba yake kwa
Taifa jana, Jumatatu, Desemba 22, 2014 ambako Rais alisema:
“Kuhusu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni Mtumishi wa Umma,
anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, hivyo nimeshaelekeza
Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za
kinidhamu zitachukuliwa.”
Ndugu
Maswi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Ndugu Frederick Werema pamoja na Mawaziri
wawili walituhumiwa wakati wa Kikao cha Bunge kilichopita kuhusiana na Akaunti
ya Tegeta Escrow.
Wakati
huo huo, Rais Kikwete ameelekeza kuwa pamoja na hatua nyingine zinazochukuliwa,
Shirika la Umeme (TANESCO) waendelee na majadiliano na IPTL kuhusu uwezekano wa
kushusha tozo la uwekezaji (capacity
charge) zaidi ya punguzo la awali lililopatikana kupitia Kituo cha Kimataifa
cha Kusuluhisha Migogoro ya Kimataifa (ICSID).
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es
Salaam.
23
Disemba,2014
0 comments:
Post a Comment