Katibu Mtendaji wa
Baraza la Taifa la Uwezeshaji, Dk Anacleti Kashuliza (wa pili kulia) akiweka
saini makubaliano ya ushirikiano kati ya FCDL na TAWOFE katika kuboresha
utengenezaji wa samani nchini. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji
na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu (wa kwanza kulia) anayeshuhudia makubaliano hayo.
*******
KAMPUNI ya Furniture Centre
(FCDL), na Shirikisho la Watengenezaji Samani Nchini (TAWOFE), wamesaini
makubaliano (MoU) kuongeza ubora wa bidhaa za samani zinazotengenezwa nchini na
kuzifanya zipate soko ndani na nje ya nchi.
Makubaliano haya yamekamilika
ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
ikiwa ni mwendelezo wa Tathimini iliyofanywa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi kwa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani, katika
kuiwezesha sekta ya Samani nchini kupitia vikundi na makampuni ya ndani.
Tathimini hiyo ya Baraza ya mwaka
2008, ilijikita katika kubaini mahitaji na changamoto zinazoikabili sekta ya
samani hapa nchini. Baraza liliweza kuandaa warsha iliyohudhuriwa na wadau
mbalimbali na ambapo matokeo ya tathmini hiyo yaliwasilishwa na kupelekea
kuundwa kwa shirikisho la watengenezaji samani nchini (TAWOFE).
Washirika hao walisaini
makubaliano hayo katika hafla
iliyoshuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na
Uwekezaji), Dk Mary Nagu.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Dk Anacleti
Kashuliza, alisema pamoja na kuwepo kwa fursa kubwa ya soko la samani hapa
nchini bado ushiriki wa vikundi na makampuni ya ndani katika soko hilo ni mdogo
sana kulinganisha na samani zinazoagizwa kutoka
nje ya nchi.
Alisema tunatoa wito kwa
taasisi za Umma na Binafsi ziunge mkono
jitihada hizi kwa kununua samani toka kwa watengenezaji samani wa ndani na ili kuwapa ushirikiano zaidi
utakaowezesha kuimarisha sekta ya samani zitengenezwazo ndani ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
TAWOFE, Bw Fredrick Waibi, alielezea makubaliano kati ya FCDL na TAWOFE ni
mkakati mzuri utaomjengea uwezo fundi seremala kuweza kutengeneza bidhaa
zitakazoweza kukubalika kimataifa, kuongeza tija kazini na kupunguza umaskini
kati ya mafundi seremala.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa FCDL, Bw
Shafik Bhatia, alisema kama wadau muhimu wa samani nchini wameona umuhimu na
wanajivunia kushirikiana na TAWOFE
katika kuboresha huduma za samani nchini .
0 comments:
Post a Comment