Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
(Meza Kuu-Katikati), akizungumza na wawakilishi wa Kampuni mbalimbali
zinazohusika kusambaza umeme vijijini kutoka India, China na Sri Lanka
zinazofanya kazi katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuhusu utekelezaji wa
miradi husika
Na Veronica Simba
Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo amezitaka Kampuni zilizopewa tenda kusambaza umeme
vijijini kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa
vinginevyo watanyang’anywa tenda hizo.
Aliyasema hayo mwishoni mwa
wiki mjini Dodoma katika Mkutano baina yake na wawakilishi wa Kampuni husika
kutoka India, China na Sri Lanka zinazofanya kazi katika mikoa ya Nyanda za Juu
Kusini Magharibi pamoja na Mameneja wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) wa
mikoa hiyo na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Profesa Muhongo aliitisha
Mkutano huo kwa lengo la kupokea taarifa kutoka kwa Watendaji wa Kampuni hizo kuhusu
hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini kabla ya
kutembelea miradi hiyo kwa mara nyingine kama ambavyo amekuwa akifanya mara kwa
mara kujiridhisha na maendeleo yake.
Akizungumza katika Mkutano huo
mara baada ya kupokea taarifa za utekelezaji kutoka pande zote, Waziri Muhongo
alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa REA, Dk. Lutengano Mwakahesya kuhakikisha
utekelezaji wa miradi hiyo unafuatiliwa kwa ukaribu na kusitisha tenda mara
moja kwa kampuni zitakazobainika kutotimiza makubaliano ya mkataba walioingia.
“Fuateni utaratibu wa kisheria
kwa kutumia vifungu vilivyomo kwenye mkataba vinavyoelekeza kuchukua hatua
stahiki kwa kampuni isiyotekeleza wajibu wake ipasavyo,” alisisitiza Muhongo.
Aliongeza kuwa Serikali
imedhamiria kuhakikisha inatimiza ahadi yake ya kuwapatia Watanzania umeme ili
wajikwamue katika lindi la umaskini kwa kukuza kipato chao na cha Taifa kwa
ujumla hali itakayofanya Tanzania kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo
mwaka 2025.
“Yeyote atakayetukwamisha au
kuturudisha nyuma katika kufikia malengo yetu ya kuwaondolea Watanzania
umaskini, tutapambana naye na kamwe hatutampa nafasi,” alisema Muhongo.
Vilevile, aliwataka Mameneja
na watendaji wengine wa Tanesco kuachana na utamaduni wa kukaa ofisini na
kusubiri ripoti za utekelezaji wa miradi badala yake watembelee miradi
wanayosimamia na kuhakikisha kazi inafanyika kama inavyotakiwa.
Aidha, Waziri Muhongo
aliwataka wakandarasi waliopewa tenda husika kuwa wakweli na waaminifu na
kuachana na tamaa hususan wanapopewa kazi ambayo wanajua hawana uwezo wa
kuitekeleza ipasavyo ili kuwapa nafasi wengine wenye uwezo huo.
Alisema ni bora kwa Mkandarasi
kukubali kazi anayoimudu ili aifanye kwa ubora unaotakiwa na hivyo kujiongezea
sifa za kupewa kazi nyingine kuliko kuomba kazi kubwa asiyoweza kuitekeleza
kikamilifu na matokeo yake anaharibu na kupoteza sifa ya kufikiriwa kupewa kazi
nyingine.
Kwa upande wake, Naibu Waziri
wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga aliwataka wote
wanaohusika na utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo ya kusambaza umeme
vijijini kutimiza wajibu wao kwa vitendo.
“Achaneni na maneno maneno,
mimi nataka kuona vitendo, nataka kuona matokeo,” alisisitiza na kuongeza
kwamba hakuna sababu ya Wakandarasi kusuasua katika utekelezaji wa miradi hiyo
kwani walioomba wenyewe wakijinadi kuwa wanaweza.
Naye Kamishna Msaidizi wa
Nishati Sehemu ya Umeme, Mhandisi Innocent Luoga aliwataka Wakandarasi hao
kujituma na kufanya kazi inavyostahili pasipo kusubiri kufuatwa-fuatwa na
kuhimizwa kwa suala ambalo ni wajibu wao.
Wakichangia mawazo katika
Mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Edmund Mkwawa na Mkurugenzi Mkuu wa
Wakala huo, Dk. Mwakahesya waliahidi kufanya kazi bega kwa bega na wadau
mbalimbali wa sekta hiyo ili kuhakikisha Watanzania hususan walioko vijijini
wanapatiwa nishati ya umeme kama Serikali ilivyodhamiria na kuahidi.
0 comments:
Post a Comment