Nafasi Ya Matangazo

December 13, 2013


Na kijiwechetu.blogspot.com
WATU Sita wamepoteza Maisha na wengine watatu wakijeruhiwa vibaya baada ya Ngema kukatika na kuwafukia wakiwa wanachimba mchanga katika machimbo ya Pumwani, wilaya ya Moshi vijijini, mkoani Kilimanjaro.

Watu hao ambao ni wachimbaji, walkikutwa na masaibu hayo jana majira ya saa 10:30 alasiri, wakati wakiwemo wanafunzi wawili, walikutwa na masaibu hayo wakati wakiwa wanapakiza mchanga kwenye gari aina ya Fuso, namba za usajili T167 AQG.
 
Mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, wananchi wakishirkiana na timu nzima ya ulinzi na usalama wa Mkoa, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama  walifika katika eneo la tukio na kuanza juhudi za kuwafukua wahanga hao.
 
Katika zoezi hilo lilichukua takribani masaa sita, miili ya watu sita iliondolewa katika Kifusi hicho, ikiwemo maiti ya wanafunzi wawili, David Macha (18), ambaye ni Mwanafunzi wa kidato cha pili, katika shule ya Sekondari ya Ebenezer-Sango, aliyekuwa anafanya kibarua kama mchimbaji katika Machimbo hayo na Marwa Mwita (14), ambaye alimaliza Darasa la Saba Mwaka huu, na kuchaguliwa kujiung ana shule ya Sekondari Uparo.
Watu wengine waliopoteza Maisha katika tukio hilo la pili kutokea kwenye machimbo hayo, katika kipindi cha Mwaka mmoja, ni Efrahim Assei (27), Mkazi wa Kawawa, Ludovick Venance (16), mkazi wa Pumwani, Omari Masoud (33), mkazi wa Pumwani na August Lyimo (26), Mkazi wa Pumwani.
Aidha watu watatu waliyojeruhiwa katika Maporomoko hayo ni pamoja na Dereva wa gari lililokuwa likipakiza mchanga katika Machimbo hayo wakati wa tukio, Antipus Babu (56), ambaye alipata majeraha kichwani na amelazwa katika Hopitali ya Rufaa ya KCMC.
Wengine ni Utingo wa gari hilo, Simon Mosha (21), ambaye alipata majeraha kidogo na kutibiwa papo hapo katika eneo la tukio pamoja na Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Charles (30), mkazi wa Sango, ambaye anaripotiwa kuwa katika hali mbaya na amelazwa katika chumba cha ungalizi wa Madaktari (ICU), katika Hopitali ya KCMC.
Akizungumza na Mamia ya Wananchi waliofika katika eneo hilo, kushiriki zoezi la uokoaji, Mkuu wa Mkoa wa huo, Leonidas Gama aliagiza kusitishwa kwa shughuli za uchimbaji katika Machimbo hayo pamoja na Machombo mengine Mkoania hapo, ikiwemo lile lililopo katika eneo la Uchira ambayo inasemekana kuwa katika hali mbaya.
Gama alisema pamoja na agizo hilo, tayari uongozi wa Mkoa umeshawasiliana na Wataalam wa Madini wa Kanda, kutoka MKoani Arusha kufika katika eneo hilo na kufanya ukaguzi wa kitaalam kabla ya kuruhusu zoezi la uchimbaji kuendelea.
“Hili ni pigo kubwa sana, poleni sana kwa janga hili lililowakuta, na ninatoa agizo kwamba ni marufuku kuendelea na shughuli za uchimbaji, Mkuu wa wilaya simamia hili na kuhakikisha Machimbo haya yanafungwa kuanzia sasa, tayari nimeshawasiliana na wataalamu wa Madini kutoka Arusha, kuja kukagua na kutathmini athari ambazo zinaweza kujitokeza tena”, alisema Gama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Robert Boaz, aliwataka wachimbaji katika Machimbo yote kuwa makini hasa katika kipindi hiki cha mvua kwani udongo sasa hivi unaingia maji kwa hiyo uwezekano wa kukatika na kusababisha maafa ni makubwa sana.

Kamanda Boaz alisema miili ya Marehemu imehifadhiwa katika Hopitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro (MAWENZI) na kwamba juhudi za kuhakikisha uhai wa waliojeruhiwa unaokolewa zinaendelea.
Posted by MROKI On Friday, December 13, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo